MANENO MAFUPI YA ASHURAA

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye kurehemu
MANENO MAFUPI YA ASHURAA
1. Umri wenye kheri nyingi wa Imamu Hussein Bwana wa mashahidi (Amani iwe juu yake)
Hakika kuamiliana kwetu na siku moja ya maisha matukufu ya Imamu Hussein (Amani iwe juu yake) ambayo ni siku ya Ashuraa kumetoa tija kubwa ambayo athari zake zilishuhudiwa na ulimwengu wote… ikiwa hali ndio hiyo, unadhani umri wa miaka (57) ya maisha unaweza kutoa matokeo gani iwapo utasomwa kwa kina katika nyanja zake mbalimbali?
2. Mpango wa urekebishaji wa Imamu Hussein (Amani iwe juu yake)
Hakika sheria ya Kiislamu ambayo ndio sheria ya mwisho na kamilifu zaidi ya Mwenyezi Mungu haikuishia kujenga na kurekebisha mambo ya kidini pekee, bali kanuni na hukumu zake zilienea kwenye mambo yote ya maisha na masuala ya wanadamu. Imamu Hussein (Amani iwe juu yake) akiwa ni mrithi wa manabii na aliyebeba bendera ya risala na ujumbe wao wote ameuelezea mpango huu mpana wa urekebishaji na kuashiria nyanja zake mbalimbali katika maneno yake matukufu. Katika uga wa kufanya marekebisho ya kidini amesema:
(Na hakika Mimi sikutoka kwa ajili ya kutafuta shari wala kutaka kufanya uharibifu, wala kufanya ufisadi wala kufanya dhulma, isipokuwa Mimi nimetoka kwa ajili ya kutaka marekebosho na islahi katika umma wa babu yangu (s.a.w.w), ninataka niamrishe mambo mema na nikataze mambo mauvu. Ninataka niende na mwenendo wa babu yangu na baba yangu Ali bin Abi Talib (Amani iwe juu yake)).
Ama katika uwanja wa kurekebisha kanuni amesema kuwa:
(Nami ninakuiteni kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu na suna ya mtume wake, kwa hakika suna imefishwa na uzushi na bidaa vimehuishwa, ikiwa mtasikiliza maneno yangu na mkatii amri yangu nitakuongozeni njia ya uongofu). Kwa maana ya kwamba waovu hao walikuwa hawatendi kwa mujibu wa katiba, ndio maana Imamu (Amani iwe juu yake) akawa akiwaita warejee kwenye utendaji unaofuata katiba –ambayo ni Qur’an tukufu- na watende kwa mujibu wa kanuni zinazoifafanua katiba hiyo –ambazo ni suna ya bwana mtume (s.a.w.w)-.
Hali kadhalika Imamu Hussein (Amani iwe juu yake) kuhusiana na marekebisho ya kisiasa na kubainisha sifa za wastahiki wa uongozi na utawala wa mambo ya umma amesema:
(Ninaapa kwa nafsi yangu kwamba, Imamu (kiongozi) hawezi kuwa isipokuwa yule atendaye kwa mujibu wa kitabu –cha Mwenyezi Mungu, Qur’ani- afanyae uadilifu, na anayefuata dini ya haki na mwenye kuizuia nafsi yake katika matashi ya Mwenyezi Mungu).
Hivyo Imamu anaona kuwa sababu ya uharibifu na ufisadi wa kiuchumi, kijamii, kimaadili na kidini na upotezaji wa haki na uadilifu, vyote vinarejea kwenye utawala na uongozi usikuwa wa haki na wakisheria unaosimamia mambo ya watu. Imamu Hussein (Amani iwe juu yake) baada ya waislamu kumkabidhi majukumu ya kuleta mabadiliko alisema:
(Yeyote atakayemuona mtawala muovu mwenye kuhalalisha haramu ya Mwenyezi Mungu, au mwenye kuiacha ahadi ya Mwenyezi Mungu, mwenye kupinga suna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kisha akawatendea waja wa Mwenyezi Mungu uovu na uadui, akawa hakuibadili hali hiyo kwa kusema wala kutenda, basi itakuwa ni haki ya Mwenyezi Mungu kumuingiza sehemu sawa na ya kiongozi huyo).
Kisha katika kufafanua maneno yake akaendela kusema:
(Kwa hakika mnajua kuwa hawa wamejilazimisha kumtii shetani na wameupa mgongo utii wa Mwenyezi Mungu, wamefanya ufisadi ardhini na wamesitisha hukumu na sheria za Mwenyezi Mungu, na mali za umma wamejimilikisha –wamezifanya kuwa zao-, wamehalalisha haramu ya Mwenyezi Mungu na kuharamisha haramu yake, na Mimi kwa ukuruba wangu kwa mtume (s.a.w.w) ndio msitahiki na mwenye haki zaidi ya uongozi).
Na katika riwaya nyingine amesema kuwa:
(Na Mimi ndiye mtu mbora zaidi aliyesimama kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu, kuihuisha sheria yake na kupigana katika njia yake, ili neno la Mwenyezi Mungu ndio liwe juu zaidi).[1]
3. Kuomba usaidizi kwa Imamu Hussein (Amani iwe juu yake) ni endelevu
Imamu Hussein (Amani iwe juu yake) katika siku ya Ashuraa alipokuwa akikariri maneno ya (Je yupo mwenye kunusuru aninusuru) hakuwa akitegemea kuongoka na kurekebika kwa waovu wale ambao Mwenyezi Mungu kashaziziba nyoyo zao, isipokuwa alikuwa anataka maneno hayo yabakie ni wito kwa vizazi vya zama zote ili vimsaidie katika kuyafikia malengo yake matukufu, na wito huo undelee kubakia kipindi chote ambacho ufisadi na dhulma aliyosimama kuibadilisha na kuanzisha mbadala ulio mwema- ili kila mmoja amnusuru na kumsaidia kwa uwezo wake na nafasi yeke. Kwani aina fulani ya kuhuisha marasimu ya Imamu Hussein (Amani iwe juu yake) inaweza kukubalika kwa baadhi ya watu na isikubaliwe kwa wengine, kwa sababu huwenda kinacho hitajika kwa hawa kikawa sio kile walichokifanya wengine, hivyo kuweni makini.
4. Usaidizi wa kweli wa Imamu Hussein (Amani iwe juu yake)
Ili kuimarisha misingi ya mapinduzi ya Imamu Hussein (Amani iwe juu yake) na kuyafanikisha malengo yake, wito wa Imamu (Amani iwe juu yake) kwamba (Je yupo mwenye kunusuru aninusuru) bado unaendelea kutolewa katika pande zote za dunia, na ukweli ni kuwa Imamu (Amani iwe juu yake) hahitaji wanusuru na wasaidizi watakao msaidia kwa mapanga na mfano, kwani utashi wa Mwenyezi Mungu ulikuwa ni yeye na familia yake wafe kishahidi katika ardhi ya Karbara, isipkuwa akitakacho ni wasaidizi watakao msaidia katika kufanikisha mpango wake, na kukamilisha ujumbe wake wa kurekebisha umma na kuamrisha mambo mema, na kukataza maovu ikiwa ni pamoja na kusimama kidete mbele ya uso wa viongozi wa upotevu, na watawala waovu na kuwakomboa watu kutokana na utumwa wa watu waovu na mashetani wa kibinadamu na wale wa kimajini.
5. Tunawezaje kuwa miongoni mwa wale wanao tamani kuwa na Imamu Hussein (Amani iwe juu yake) na maswahaba zake?
Sote kumuongelesha Imamu Hussein (Amani iwe juu yake) na maswahaba wake wema kwa ndimi zetu na mioyo yetu tukisema:
(Laiti tungelikuwa nanyi tukafaulu ufaulu ulio mkubwa kabisa) na tunasikitika kwamba ni kwanini hatukuwa ni miongoni wa kizazi kile kilichoishi zama za maasumina (Amani iwe juu yao) tukapata bahati ya kuonana nao na tukafaulu kwa kuwanusuru na kwakupata shahada tukiwa mbele yao. Tunaamini kwamba Mwenyezi Mungu ni mwadilifu na huwapa waja wake fursa zilizo sawa ili kwazo wajikurubishe kwake, lakini swali kuwa je Mwenyezi Mungu alikipa kizazi kile fursa ile adhimu na Sisi akatunyima? Bila shaka jambo hili litakuwa ni kinyume na ukweli uliothibiti kwamba Mwenyezi Mungu ni mwadilifu. Sasa fursa yetu inayoendana na ile ya wale ni ipi? Bila shaka kwa mujibu wa maneno ya Imamu Ali bin Abi Talib (Amani iwe juu yake) fursa hiyo ni kutekeleza wajibu wa kuamrisha mambo mema na kukataza mambo maovu, alisema:
(Hayakuwa matendo mema yote, wala kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu vikilinganishwa na kuamrisha mambo mema na kutakaza mambo maovu isipokuwa ni kama kupuliza kwenye bahari yenye kina kirefu).
[1]. Qabasat min Nuur a-Qur’an, qabas: 58.