Ayatollah Yaqoobi: Kufanya Marasimu ya Imam Hussein (a.s) katika kipindi cha janga la Corona (Covid: 19)

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye kurehemu
Ayatollah Yaqoobi: Kufanya Marasimu ya Imam Hussein (a.s) katika kipindi cha janga la Corona (Covid: 19)
Ni jambo lisilo na shaka ndani yake kwamba, kuomboleza na kufanya marasimu ya Imam Hussein (a.s) ni moja ya ibada tukufu za kidini ambayo inashabihiana na zile ibada tukufu za wajibu katika baraka zake, athari zake katika kulinda na kuhifadhi dini ya kweli, kuimarisha mafunzo ya dini katika nyoyo za waumini, na kuwalingania wanadamu kwa Mwenyezi Mungu aliyetukuka.
Hivyo, kuifanya ibada hiyo na kuipa umuhimu unaostahili ni mfano uliowazi kabisa wa maneno ya Mwenyezi Mungu yasemayo:
(وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ).
(Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo.) Surat Al-Hajj: 32.
Isipokuwa kuenea kwa janga hili la Corona ambalo mataifa yote yanaliishi kwa sasa, na mamilioni ya watu kuambukizwa virusi hivi hatari, kiasi cha shirika la afya dunia (WHO) kutangaza kuwa ni janga liangamizalo, kunatulazimisha kisheria na kiakili, ikiwa ni katika kile kijulikanacho kuwa: “mlango wa ulazima wa kulinda nafsi na kuwalinda wengine”, kuzingatia maelekezo ya kiafya ambayo yatazuia kuenea na kusambaa ugonjwa huu.
Hivyo basi, wajibu wa waumini ni kuchunga maelekezo ya kukaa mbalimbali, kuvaa barakoa, kupulizia dawa maeneo na kunawa mikono pindi wagusanapo. Wajiepushe na mikusanyiko ya watu wasio chunga umbali unaostahili wakati wa kufanya marasimu za Imam Hussein (a.s) na ibada nyinginezo za kidini. Na ikiwa kutapatikana vifaa vya kupimia, basi ni vyema kufanya vipimo kwanza na kuhakikisha usalama wa watu, na kuonyesha vielelezo vya usalama iwapo mtu ataingia kwenye eneo la watu wengi ambalo masharti yake ni kuonyesha vielelezo hivyo.
Na iwapo waumini hawataweza kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, basi wafanye marasimu hayo majumbani mwao na familia zao tu, na wasikilize mihadhara ya makhatwibu wajuzi, nayo kwa fadhila za Mwenyezi Mungu inapatikana kwa wingi kwenye mitandao ya kijamii.
Waumini wazingatie kusoma Ziaratu A’shuraa kila siku; kwani imethibitishwa kuwa ni sababu madhubuti ya kukidhi mahitaji, kuondoa balaa, kutatua matatizo, na kupata thawabu na uombezi wa maasumina (Amani iwe juu yao) siku ya Mwisho.
Lakini pia, tusisahau kuhuisha utajo wa Abu Abdillah Al-Hussein (Amani iwe juu yake) kwa namna mbalimbali na kudumisha marasimu yake kwa njia kama vile kujitolea damu, na kwa wale waliopata ahuweni kutokana na Corona wajitolee damu. Tuwatembelee wenye maambukizi waliotengwa majumbani mwao, tusaidie vifaa vya kuzalisha hewa ya oksijeni kwa wagonjwa na mahospitali, ikiwa ni pamoja na kuandaa dawa zinazohitajika. Tuingize furaha kwa mayatima na kuwafariji waliopatwa na matazizo na kuwasaidia wenye shida na uhitaji kwa namna ambayo italinda heshima yao, yote hayo tuyafanye kwa jina la Imam Hussein (Amani iwe juu yake). Hali kadhalika, vigawiwe vipeperushi, na yabandikwe mabango yenye maneno ya Imam Hussein (Amani iwe juu yake) ili yauangazie umma njia ya uongofu. Vile vile, yaonyeshwe makatuni yanayotoa utatuzi wa matatizo na maovu ya kijamii, na kusisitizwe mambo mazuri; ili kutimiza dhamira ya kutoka kwa Imam Hussein (Amani iwe juu yake) ambayo ilikuwa ni kusimamia na kudumisha faradhi ya kuamrisha mema na kukataza maovu.
Bila shaka wairaki wameona kwamba, pale walipojizatiti kutekeleza na kufuata miongozo ya kisheria na maelekezo ya kiafya mwanzoni mwa kudhihiri virusi vya Corona, ambako kulisadifiana na kuandama mwezi wa Rajabu, maambukizi yalikuwa ni kidogo sana na ikiwa ni fahari kwa ulimwengu mpaka mashirika ya mataifa yanayohusika na mambo ya afya yakawa yakijiuliza ni nini siri ya kutoenea Corona katika nchi ya Iraki licha ya kuzungukwa na nchi zilizokuwa na maambukizi, hali ikaendelea hivyo kwa kipindi cha miezi mitatu, lakini ilipoingia idil-fitr watu wakakeuka na kukhalifu miongozo, na hatima yake idadi ya waathirika ikazidia kipimo, hali ya kuwa Iraki haikuwa na uwezo wa kukabiliana na mfano wa mabalaa hayo kwa sababu ya wingi wa majeraha iliyonayo ambayo hayajapona.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atuondolee mambo mabaya na yenye madhara, na atunemeshe kwa afya katika mambo yetu, na atuwafikishe kumtii na kupata radhi zake; kwani yeye ndiye mmiliki wa neema.
Muhammad Yaqoobi
19/Dhul-hijjah/1441
09/08/2020