Ulinganisho kati ya Bi Fatimah Zahraa (Amani iwe juu yake) na Bi Maryam binti Imran

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Ulinganisho kati ya Bi Fatimah Zahraa (Amani iwe juu yake) na Bi Maryam binti Imran*
Sisi wafuasi wa Ahlulbayt (a.s) tuna mahusiano maalumu na bi Maryam binti wa nabii Imran kwa sababu ya kushabihiana na bi Fatimah Zahraa (a.s) katika sifa nyingi, licha ya kuwa bi Fatimah Zahraa kampita bi Maryam katika sifa hizo.
Bi Maryam alichukua sehemu ya nuru ya bi Bi Fatimah Zahraa (a.s), na kwa sababu hiyo akawa ni mwenye kumeremeta kwa nuru pale awapo mihirabuni mwake. Na kwa mujibu wa hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Imam Baaqir (a.s) ni kuwa: (Bi Maryam alikuwa ni mzuri kuliko wanawake wote, alikuwa anaposwali nuru yake huiangazia mihirabu)[1].
Bi Maryam alikuwa ni (Muhaddathah), jina ambalo ni moja ya majina ya bibi Fatimah Zahraa (a.s) kwa maana kwamba alikuwa akizungumzishwa na malaika kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kitukufu cha Qur’ani:
(وَإِذْ قَالَتِ الْمَلائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَاكِ وَطَهَّرَكِ وَاصْطَفَاكِ عَلَى نِسَاء الْعَالَمِينَ)[2]
(Na angalia pale Malaika walipo sema: Ewe Maryam! Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuteuwa, na akakutakasa, na akakutukuza kuliko wanawake wote)
(فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا)[3]
(Tukampelekea Roho wetu)
Na imepokelewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) kwamba alisema: (Kwa hakika Bi Fatimah Zahraa aliitwa kwa jina hili la (Muhaddathah) kwa sababu malaika walikuwa wakishuka kutoka mbinguni kisha wakimwita kama alivyokuwa wakifanya kwa bi Maryam binti wa Imrani, wakisema: Ewe Fatimah! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteuwa na kukutakasa, na amekuteuwa juu ya wanawake wa ulimwenguni, hivyo kunuti kwa ajili ya Mola wako mlezi, sujudu na urukuu pamoja na wenyekurukuu, akawa akiwazungumzisha nao wakimzungumzisha. Siku moja bi Fatimah Zahraa (a.s) akamwambia malaika wale kuwa: Je bi Maryam sindio mwanamke bora kuliko wanawake wote wa ulimwengu? Wakasema: Hakika Maryam alikuwa ni mwanamke bora kwa wanawake wa zama zake, na wenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka amekufanya wewe kuwa mbora wa wanawake wa zama zako na zama zake, na mbora wa wanawake wa mwanzo na mwisho)[4].
Na kuhusiana na sifa ya utakaso, Mwenyezi Mungu anasema kumhusu Bi Maryam (na amekutakasa), wakati kuhusu Ahlul-bayt (amani iwe juu yao) aliteremsha aya ya utakaso akasema:
(إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا) [5]
(Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara)
Na katika kuchaguliwa na ubora, Mwenyezi Mungu memfanya bi Maryam kuwa mbora wa wanawake wa ulimwengu kama alivyokuwa kwa bi Fatimah (amani iwe juu yake). Sema kwamba tofauti iliyopo kati ya wawili hao ni kama ilivyotajwa katika hadithi kutoka kwa Al-Mudhal bin Omar, alisema: (Nilimwambia Abu Abdillah Swaadiq (amani iwe juu yake) niambie kuhusu kauli ya mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) juu ya Fatimah kwamba ni mbora wa wanawake wa ulimwenguni, je yeye ni mbora wa wanawake wa ulimwengu wake pekee? Akasema: hilo ni kuhusiana na Maryam ndiye alikuwa mbora wa wanawake wa ulimwengu wake, ama Fatimah ni mbora wa wanawake wa ulimwengu toka wamwazo mpaka mwisho)[6]. Na ukiashilia upana wa kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema (juu ya wanawake wa ulimwengu), ubora wa bi Maryam hautakuwa mahsusi kwa zama zake tu kama ilivyo katika tafsiri Al-Mizan! Tunasema ndio, lakini uchaguaji huo ni mahsusi kwa aya maalumu, kama vile Aya iliyoambatana na ujauzito wake na namna ya kuzaliwa kwake, wakati kwa bi Fatimah Al-Zahraa (amani iwe juu yake) uchaguzi huo ni mutlaki (wa moja kwa moja) na usio na kikomo maalumu. Na hii ndio totauti kati ya kuchaguliwa kunakoambatana herufi (a’laa) kama ilivyo kwa bi Maryam na kuchaguliwa kusiko na ukomo kama ilivyo kwa bi Fatimah (as). Kama kadhalika, kuchaguliwa kunakofungamana na herufi (a’laa) kunamanisha kutangulia, na kwamba sio kule kuchaguliwa kusiko na kikomo ambako humanisha kujisalimisha. Na kwa sababu hii, kuchaguliwa kwa bi Maryam juu ya wanawake wa ulimwenguni, kuna maana ya kuwatangulia. Na kuwatangilia kwake kulikuwa katika baadhi ya sekta, (kwa sababu hakuwa na jambo (kitu) miongoni mwa vile vinavyowahusu wanawake wengine, isipokuwa ni lile jambo lake la kustaajabisha, la kumzaa nabii Issa (amani iwe juu yake) na kwamba hii ndio ilikuwa sababu ya kuchaguliwa kwake, na kutangulizwa juu ya wanawake wa ulimwegu)[7].
Ama juu ya suala la kuzaliwa kwa maasumina wakasifu (amani iwe juu yao), Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwakinga na shetani aliyelaniwa. imekuja katika hadithi kutoka kwa Amiril-muunina (amani iwe juu yake) kuhusiana tukio la kumuowa bi Fatimah (amani iwe juu yake) na dua waliyosomewa na bwana Mtume (s.a.w.w) kwamba alisema: “Simama kwa jina la Mwenyezi Mungu na useme: Kwa baraka ya Mwenyezi Mungu, na kwa alitakalo Mwenyezi Mungu, hapana nguvu isipokuwa zake Mwenyezi Mungu, nimemtegemea Mwenyezi Mungu, kisha aliponikalisha kwa Fatimah akanijia na kusema: Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika wawili hawa ni viumbe wapendwa kwangu basi wapende, na ukibariki kizazi chao na uwape ulinzi utokao kwako, na kwa hakika ninawalinda wawili hawa na kizazi chao kutokana na shetani aliyelaniwa na kutwengwa mbali rehema zako)[8]
Ama kuhusiana na riziki iliyokuwa ikimjia bi Maryam mihirabuni kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, imekuja katika riwaya iliyopokelewa kutoka kwa sahaba mtukufu Hudhaifa bin Al-Yaman juu ya chakula alichokikuta bwana Mtume (s.a.w.w) na masahaba wake katika nyumba ya bi Fatimah, chakula ambacho hawakupata kukitambua kabla ya hapo, akaendelea kusimulia mpaka aliposema: kisha Mtume (s.a.w.w) akasimama mpaka akaingia kwa bi Fatimah (amani iwe juu yake) akasema: (chakula hiki umekitoa wapi ewe Fatimah?) Bi Fatima akamjibu hali ya kuwa nasi tukisikia mazungumzo yao, akasema:
(هو من عند الله إن الله يرزق من يشاء بغير حساب)
(Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.)
Mtume (s.a.w.w) akatoka akibubujikwa na machozi huku akisema:
(الحمد لله الذي لم يمتني حتى رأيت لابنتي ما رأى زكريا لمريم كان إذا دخل عليها المحراب وجد عندها رزقا فيقول: (يَا مَرْيَمُ أَنَّى لَكِ هَذَا قَالَتْ هُوَ مِنْ عِندِ اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ يَرْزُقُ مَن يَشَاء بِغَيْرِ حِسَابٍ)
(Kila sifa njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye hajanifisha mpaka nimeona kwa binti yangu yale aliyoyaona nabii Zakariya kwa Maryam. Alikuwa akiingia kwake humkuta na chakula kisha akimuuliza:
(Ewe Maryam! Chakula hiki umekitoa wapi? Akisema: hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa hakika Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila hisabu)[9]
Ninafurahi kunukuu beti hizi za mashairi zenye kutoa ulingano kati ya baadhi ya hali za Swiddiqah al-Kubraa Fatimah al-Zahraa (amani iwe juu yake) na Swiddiqah Maryam:
إن قِـيـلَ حَــوّا قُـلـتَ فـاطـمُ فَـخرُها *** أو قـيـلَ مـريـمُ قـلـتُ فـاطـمُ أفـضلُ
Ikisemwa Hawa, nitasema Fatimah ndio fakhari yake*** au ikisemwa Maryam, nitasema Fatimah ni mbora zaidi
أفــهـلْ لـمـريـم والـــدٌ كـمـحـمدٍ *** أم هَــلْ لـمـريمَ مـثـلُ فـاطـمَ أشـبلُ
Je Maryam ana baba kama Muhammad? *** au ana vinaja masimba mfano wa Fatimah?
كـــلٌ لــهـا عـنـدَ الــولادةِ حـالـةٌ *** فـيـها عـقـولُ بـنـي الـبصائرِ تـذهَلُ
Kila mmoja wao wakati kuzaa ana hali maalumu *** kwazo akili za welevu huondoka
هـــذي لـنـخلتِها الـتَـجَتْ فَـتَـساقَطَتْ *** رُطَــبَـاً جَـنـياً فـهـي مـنـه تـأكُـلُ
Huyu (bi Maryam) aliuelekea mtende wake ukaangusha *** tende nzuri zilizo mbivu naye akizila.
ولــدت بـعـيسى وهــي غـيرُ مـروعةٍ *** أنَّـــى وحـارسُـها الـسّـري الأبـسـلُ
Alimzaa Issa naye akiwa si mwenye kuhofishwa *** siyo tu hakuhofishwa, bali mlinzi wake ni watu wema na majasiri
وإلــى الـجدارِ وصـفحةِ الـبابِ الـتَجت *** بـنـتُ الـنَّـبي فـأسـقَطَتْ مــا تَـحمِلُ
(Fatima) aliekea kwenye ukuta na upande wa mlango*** binti wa Mtume akaporomoa alichokibeba
سَـقَـطت وأسـقَـطَتِ الـجـنينَ وحـولَها*** مــن كــلِّ ذي حـسـبٍ لـئـيمٍ جَـحفل
Akaanguka na akaporomoa kichanga na pembeni yake *** kukiwa na kundi la waovu madhalili
هــــذا يـعـنـفـها وذاكَ يــدُعُّـهـا*** ويــردهـا هـــذا وهـــذا يــركُـلُ
Huyu akiamiliana naye kwa nguvu na yule akimsukuma kwa nguvu *** na huyu akimrudisha nyuma na mwengine akimpiga mateke
وأمـامَـهـا أســـدُ الأســـودِ يـقـودُهُ *** بـالـحبل قـنـفذ هــل كـهـذا مـعضَلُ
Na mbele yake yupo simba wa masimba akimburuza*** mkabala wake akiwepo samba wa masimba akimvuta. Je kuna msiba mfano wa huu?!
ولـسـوفَ تـأتـي فــي الـقـيامةِ فـاطمٌ *** تـشـكـوا إلــى ربِّ الـسـماءِ وتـعـولُ
bila shaka siku ya kiyama atakuja Fatimah *** akimshtakia Mola wa mbingu na kulia kwa sauti.
ولـتَـرفَـعَـنَّ جـنـيـنَـها وحـنـيـنَها *** بـشـكـايةٍ مـنـهـا الـسـماءُ تَـزلزَلُ
Bila shaka atakiinua kichanga chake na kuinua kilio chake*** kwa mashtaka ambayo kwayo mbingu zitatetemeka[10]
------------------
* Makala haya yalichapishwa katika gazeti la Al-Sadiqin, toleo la 202, ukurasa wa pili, iliyotolewa mnamo 27,Dhul-Qaadah 1441
[1] . Al-Burhan fii tafsir al-Qur'an: 2/33 kutoka katika tafsiri ya Ayyashy: 1/193.
[2] . Surat al-Imran: 42.
[3] . Surat Maryam: 17.
[4] . I’lal ash-Sharai’i: 1/216, Tafsir Nur al-Thaqalin 1/337.
[5] . Surat al-Ahzab: 33.
[6] . Al-Burhan fii tafsir al-Qur'an: 2/216 hadidhi: 7 kutoka Maanil Akhbaar cha Saduq: 107 hadithi:1.
[7] . Al-Mizan fii tafsir al-Qur'an: 3/218.
[8] . Amali Al-Sheikh Al-Tusi: 40, Tafsir Nur Al-Thaqalin: 1/333.
[9] . Al-Burhan fii tafsir al-Qur'an: 2/216 hadithi:8, kutoka katika Amali cha Sheikh Tusi: 2/227.
[10] . Diwan ya Sheikh Mohsen Abu Al-Kabeer / uk. 128.