HADITHI ARUBAINI KATIKA FADHILA YA QUR’ANI NA ATHARI NA DESTURI ZA KUISOMA
HADITHI ARUBAINI KATIKA FADHILA YA QUR’ANI NA ATHARI NA DESTURI ZA KUISOMA
Na nitatosheka hapa na kutaja nasi (mapokezi) za hadithi sambamba na kuweka anuani inayohusiana na maudhui husika. Na pia kubainisha hadithi kwa mujibu wa malengo yake. Hata hivyo ufafanuzi wake na kubainisha nukta zilizomo, ni suala linaweza kutengewa eneo jingine. Na sitoweka ukomo wa idadi 40, kwa kuwa mapokezi ambayo yamehimiza juu ya kuzingatiwa hadithi 40 hatuyafahamu juu yake iwapo yanahusu sharti na si kuhusiana na ziada, hivyo ziada itakuwa kheri.
1-Ulazima wa kujifundisha (Qur’ani).
Imepokelewa kutoka kwa Abu Abdillah (a.s) amesema: “Inatakiwa kwa muumini asife hadi akiwa amejifundisha Qur’ani au awe katika kujifundisha.[1]” Na imepokewa kutoka kwa Mtume wa Allah (saw) akisema: “Mwenyezi Mungu hatouadhibu moyo ulioifahamu Qur’ani.[2]”
Na kutoka kwa Mtume wa Allah amesema: “Mtu bora kwenu ni atakayejifundisha Qur’ani na akaifundisha.[3]” Na imepokewa kutoka kwa Mtume wa Allah (saw) akisema: “Wabebaji wa Qur’ani (vifuani) duniani, wanawafahamu watu wa peponi siku ya Kiama.[4]”
Na kutoka kwake (saw) amesema: “Qur’ani ni utajiri ambao hakuna utajiri zaidi yake na hakuna umasikini baada yake.[5]” Na pia kutoka kwa Mtume wa Allah (saw) amesema: “Mwalimu anapomwambia mtoto, Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwenye Kurehemu, Mwingi wa Rehma, (kisha) mtoto akasema, Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwenye Kurehemu, Mwingi wa Rehma, Mwenyezi Mungu huandika kumuepusha na (moto) mtoto, na kuwaepusha na (moto) wazazi wake, na kumuepusha na (moto) mwalimu.[6]”
Na kutoka kwa Abu Abdillah (a.s) amesema: “Mtu mwenye kuhifadhi Qur’ani, anayeifanyia kazi watakuwa pamoja na watukufu wema”.[7]
2-Kujifundisha Qur’ani ni neema kubwa.
Imepokewa kutoka kwa Mtume (saw) akisema: “Atakayesoma Qur’ani akadhani kwamba kuna mtu aliyepewa jambo bora kuliko yeye, atakuwa amedharau kile alichokitukuza Mwenyezi Mungu, na kutukuza kile alichokidharau Mwenyezi Mungu.[8]”
3-Qur’ani ni muombezi, shifaa na mtetezi mkweli
Imepokewa kutoka kwa Mtume (saw), akisema kwenye hadithi kwamba: “Mtakapopatwa na fitina kama kipande cha usiku wenye giza, basi shikamaneni na Qur’ani, kwani yenyewe ni muombezi, shifaa na mtetezi mkweli. Atakayeitanguliza itamuongoza peponi, na atakayeiweka nyuma, itamuongoza motoni, nayo ni muongozaji kwenye njia ya heri. Nacho ni kitabu chenye ufafanuzi na ubainifu ndani yake”, pia akasema: “hayahesabiki maajabu yake na haufichuki ugeni wake. Ni taa za wongofu na mwanga wa hekima”.[9]
4-Sifa ya msomaji wa Qur’ani
Imepokewa kutoka kwa Abu Abdillah (a.s) akisema: “Inatakiwa kwa anayesoma Qur’ani wakati anapopita kwenye aya ndani ya Qur’ani inayozungumzia suala la hofu, amuombe kwayo Mwenyezi Mungu heri anayoitarajia na amuombe kuepushwa na moto na adhabu”.[10]
Na kutoka kwa Mtume wa Allah (saw) amesema: “Ninashangaa ni kwa nini siwi mzee wakati ninaposoma Qur’ani.[11]” Na katika hotuba ya Amirul-Muunina Ali (a.s) kwenye kuwataja wachamungu alisema: “Ama usiku wameweka safu kwa miguu yao wakisoma juzu za Kitabu, wanasoma taratibu, wanazihuisha nafsi zao kwa hicho kitabu, na wanaibua (kwa kitabu hicho) hamasa ya huzuni wakilia kwa dhambi zao kwa uchungu mithili ya maumivu ya jeraha zao. Wanapopita kwenye aya ambayo inatia hofu, wanaielekezea masikio, mioyo na macho yao, pia ikasisimka kwayo ngozi zao, na mioyo yao ikaogopa, mithili ya ukelele wa Jehannam na mipapatiko na mikoromo yake kwenye masikio yao. Na wanapopita kwenye aya yenye kuvutia, huitegemea kwa tamaa na kufungamana nafsi zao kwa mvuto”.[12]
5-Wajibu wa kuwakirimu wabeba Qur’ani na uharamu wa kuwadharau
Imepokewa kutoka kwa Mtume (saw) akisema: “Hakika watu wa Qur’ani wako kwenye daraja ya juu kati ya wanadamu ispokuwa Manabii na Mitume. Msipuuze haki za watu wa Qur’ani kwani wana nafasi mbele ya Mwenyezi Mungu Mukufu Mtenza nguvu.[13]”
6-Thawabu za yule inayemuwea vigumu kujifunza Qur’ani na kuihifadhi
Imepokewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) akisema: “Yule ambaye Qur’ani itamuwea ngumu, atakuwa na malipo ya aina mbili na yule ambaye itamuwea nyepesi, atakuwa pamoja na mwanzo.[14]” Na kutoka kwake (Imam Swadiq-A.S) pia amesema: “Hakika yule anayeweza (kuisoma) Qur’ani na anaihifadhi kwa matatizo kutoka kwake na kutokana na uwezo mdogo wa kuhifadhi, atakuwa na malipo ya aina mbili[15]”.
7-Wajibu wa kusoma Bismillah kabla ya kila sura
Imepokewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) akisema: “Wakati mtu anapowasalisha watu, huja shetani kwa shetani (mkuu) ambaye huwa karibu na imam na kusema, je amemtaja Mwenyezi Mungu? Yaani amesoma, ‘Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema mwenye kurehemu’ ikiwa atasema ndio, basi hukimbia. Na akisema, hapana basi hupanda shingo ya imamu na kunyoosha miguu yake kwenye kifua cha (Imamu). Basi shetani ataendelea kubakia mbele ya watu hadi watakapomaliza swala yao”.[16]
8-Suna ya kusoma Qur’ani wakati wa kutembelea makaburi
Katika kitabu cha (Man laa Yahdhurul-Faqih) imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Ridha (a.s) akisema: “Hakuna mja muumini atatembelea kaburi la muumini akasoma kwenye kaburi (surat) Qadr mara 7, ispokuwa Mwenyezi Mungu atamsamehe (yeye) na yule aliye ndani ya kaburi”.[17]
Na katika riwaya nyingine inasema: “Atapata amani kutokana na hofu kubwa.” Na katika maana hiyo kuna riwaya nyingi. na sehemu nyingine inazungumzia suala la sunna ya kuzidisha Surat Al-Faatiha, Muawwadhataini, Tauhidi na Ayat Kurusiyyu kila moja mara tatu. Na imepokewa kuhusu thawabu zake kwamba: “Hakika Mwenyezi Mungu, humtumia malaika anayemwabudu Allah kwenye kaburi yake, na kumuandikia yeye (msomaji) na maiti thawabu zinazotokana na ibada ya yule malaika. Na Mwenyezi Mungu atakapomfufua kutoka katika kaburi yake hatokumbwa na hofu ispokuwa Mwenyezi Mungu atamuepusha nayo kutokana na (ibada za) yule malaika aliyewakilishwa, hadi atakapomuingiza peponi”. [18]
9-Fadhila za kujifundisha Qur’ani katika rika la ujana na athari zake
Kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) amesema: “Atakayesoma Qur’ani naye akiwa ni muumini, basi Qur’ani itachanganyika na nyama na damu yake na Mwenyezi Mungu atamfanya kuwa pamoja na watukufu na wema. Na Qur’ani itakuwa kwake mtetezi siku ya Kiyama. Itasema: Ewe Mola wangu hakika kila mtendaji amepata ujira wa matendo yake ispokuwa aliyenishughulikia, hivyo mkirimu kwa malipo yaliyo bora. Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu mtenza nguvu, atamvisha mavazi mawili miongoni mwa mavazi ya peponi, na kutawekwa kichwani kwake taji takatifu, kisha atasema kuiambia je, tumekuridhisha ndani yake (kwa malipo ya huyu mtu?) kisha Qur’ani itasema: “Ewe Mola wangu nilikuwa ninamtakia yaliyo bora zaidi ya haya. Anasema (as), basi atapewa amani upande wake wa kulia na kubakia milele upande wake wa kushoto, kisha ataingia peponi na ataambiwa soma aya upande daraja, kisha ataambiwa, je tumekutosheleza kwa hayo na kukuridhisha? Itasema, ndio.[19]”
10-Ulazima wa kuwafundisha watoto Qur’ani
Imepokelewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) katika hadithi akisema: “Watavishwa wazazi wake- yaani wazazi wa aliyehifadhi Qur’ani, mavazi mawili iwapo watakuwa waumini kisha wataambiwa, haya ni malipo ya mliyomfundisha Qur’ani”.[20] Na katika hadithi nyingine iliyopokelewa kutoka kwa Amirul-Muuminina Ali (a.s) imesema: “Hakika Mwenyezi Mungu hajali kuwaadhibu watu wote wa ardhini hata asiepukwe kati yao yeyote iwapo watafanya maasi na watatenda makosa. Lakini anapowaangalia wazee wakiielekeza miguu yao kuelekea kwenye swala, na watoto wakijifundisha Qur’ani, huwarehemu na kuwacheleweshea (adhabu)”.[21]
11-Aina za wasomi wa Qur’ani na sifa ya msomi wa kweli
Imepokelewa kutoka kwa Abu Ja’far (a.s) amesema: “Wasomaji wamegawanyika sehemu tatu; mtu aliyesoma Qur’ani akaichukulia kuwa ni bidhaa akajikaribisha kwayo kwa wafalme na akapata umashuhuri kwa watu, na mtu aliyesoma Qur’ani akahifadhi herufi zake lakini akapoteza sheria zake[22] na akaichukulia kwa namna mbaya, basi Mwenyezi Mungu asiwajaalie hao kuwa wabebaji wa Qur’ani, na mtu ambaye aliisoma Qur’ani akaweka ponyo ya Qur’ani juu ya ponyo la moyo wake, akakesha usiku na akashinda nayo mchana wake, akaidumisha katika maeneo ya ibada, kwa watu hao Mwenyezi Mungu huondoa balaa na kwa wao Mwenyezi Mungu huwashinda maadui na kwa wao Mwenyezi Mungu huteremsha mvua kutoka mbinguni. Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu! Wasomi hao wa Qur’ani ni watakatifu kuliko (madini) ya kibiriti nyekundu”.[23]
Na imepokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) amesema: “Ewe uliyebeba Qur’ani (uliyehifadhi) kuwa mnyenyekevu kwake Mwenyezi Mungu atakuinua. Usijitweze kwake Mwenyezi Mungu akakudhalilisha. Ewe uliyebeba Qur’ani jipambe nayo kwa Mwenyezi Mungu, naye atakupamba kwayo. Na usijipambe nayo kwa watu akakuchafua nayo Mwenyezi Mungu”.[24]
12-Kuifahamu Qur’ani ni daraja iliyo karibu na utume
Imepokelewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema: “Atakayehitimisha Qur’ani, basi atakuwa amepiga hatua za Utume kati ya pande zake, ispokuwa tu hashushiwi wahyi”.[25]
13-Njia kamilifu kwa wasomaji wa Qur’ani, waanze mwanzo wake hadi mwisho wake na sio kusoma sura tofauti.
Imepokewa kutoka kwa Al-Zuhri amesema: “NIlisema kumwambia Ali bin Hussein (a.s), ni matendo gani yaliyo bora? Akasema; (Muhitimishaji muanzishaji) nikasema, na ni nini maana ya Muhitimishaji muanzishaji, akasema (a.s), anayeifungua Qur’ani na kuihitimisha, kila atakapoanzia mwanzo wake, anakwenda hadi mwisho wake.[26] Na mwishoni akaulizwa; ni matendo gani yaliyobora akasema: ni (Muhitimishaji muanzishaji) ikasema, ni nani huyo? Akasema; Muhitimishaji muanzishaji, ni yule ambaye anahitimisha Qur’ani kwa kuisoma kisha anaanza usomaji mwanzoni mwake. Alimfananisha na msafiri anayefika nyumbani akakaa hapo kisha akaanzisha upya safari nyingine yaani anaianzisha. Na kadhalika kisomo cha watu wa Makkah wanapohitimisha Qur’ani kwa kisomo huanza (tena) wakasoma Al-Fatiha na aya tano za mwanzo wa surat Al-Baqarah hadi kauli ya Allah inayosema; (hao ndo waliofaulu.) Kisha wanasimama na kumtaja anayefanya hivyo kuwa ni muhitimishaji muanzishaji, yaani kwamba anahitimisha Qur’ani na akaanza tena mwanzo wake bila kutenganisha muda mrefu”.
Na kwa maana ya hadithi hiyo imepokewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) akisema: “Ikasemwa ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni watu gani wabora? Akasema (a.s) ni (Muhitimishaji muanzishaji), ikasemwa ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ni nani huyo muhitimishaji muanzishaji? Akasema (a.s); muanzishaji na muhitimishaji ni ambaye anasoma Qur’ani na anaihitimisha, huyo atakuwa na maombi yenye kupokelewa mbele ya Mwenyezi Mungu”.[27]
14-Usia kwa kukithirisha kuisoma Qur’ani
Na katika usia wa Mtume (saw) kwa Ali (a.s) alisema: “Jibidishe kusoma Qur’ani katika hali yoyote”.[28]
15-Thawabu za kusoma Qur’ani
Imepokewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) akisema: “Jibidisheni kusoma Qur’ani hakika daraja za pepo ziko kwenye idadi ya aya za Qur’ani. Itakapokuwa siku ya Kiama itaambiwa msomaji wa Qur’ani, soma na upande daraja, kila anaposoma aya, anapanda daraja”.[29]
Na imepokewa kutoka kwa Abu Ja’far (a.s) amesema: “Alisema Mtume (saw); atakayesoma aya 10 usiku, hatoandikwa miongoni mwa wasahaulifu. Na atakayesoma aya 50 ataandikwa ni miongoni mwa wakumbukaji. Na atakayesoma aya 100 ataandikwa miongoni mwa watiifu. Na atakayesoma aya 200 ataandikwa miongoni mwa wanyenyekevu. Na atakayesoma aya 300 ataandikwa miongoni mwa waliofaulu. Na atakayesoma aya 500 ataandikwa miongoni mwa wenye kujitahidi. Na atakayesoma aya 1000 ataandikiwa fungu, na fungu la uzito wa elfu 15 (au elfu 50) la dhahabu. Uzito wa fungu la elfu 24, uchache wake unalingana na mlima wa Uhud na zaidi yake ni kati ya mbingu na ardhi”.[30]
16-Umuhimu wa kuhifadhi yale unayojifundisha katika Qur’ani na asiache kwa kiasi cha kusahau
Imepokelewa hadithi kutoka kwa Ya’qub Al-Ahmar amesema: “Nilisema kumwambia Abu Abdillah (a.s), nina dinar nyingi na nimeingiwa na kitu ambacho kimekaribia kuifanya Qur’ani iniondoke. Akasema Abu Abdillah (a.s); Qur’ani Qur’ani, hakika aya za Qur’ani na sura zitakuja siku ya Kiama hadi zitapanda daraja 1000-yaani peponi- na zitasema; lau kama ungenihifadhi ningekufikisha hapa”.[31]
Nami nasema kwamba, huko nyuma ulitangulia kusoma kwamba kuhifadhi Qur’ani kimaanawi, kuna maana ya kuchunga mipaka na maana zake sambamba na kuzingatia maamrisho na makatazo yake.
17-Suna ya kusoma Qur’ani ukiwa na udhu
Imepokewa kutoka kwa Muhammad Ibn Al-Fudhail kutoka kwa Abul-Hassan (a.s) amesema: “NIlimuuliza (kwamba) huwa ninasoma msahafu kisha natokwa na haja ndogo kisha ninasimama na kujisaidia haja ndogo, kujisafisha na kuosha mikono, halafu ninarudi kwenye msahafu na kusoma ndani yake? Akasema; hapana (utatawadha) hadi pale ukiwa unasali.[32]” na kutoka kwao (Maimamu watoharifu-as) wamesema: “Msomaji wa Qur’ani ana malipo ya mema 100 kwa kila herufi atakayoisoma katika swala akiwa amesimama, na mema 50 akiwa amekaa na mema 25 akiwa na tohara katika swala zisizo (swala) tano, na mema 10 iwapo hatokuwa na tohara.” Lakini mimi nasema; kusoma herufi za Alif, Lam, Mim, Ra utapata thawabu 10 kwa Ali, 10 kwa lam, 10 kwa Mim na 10 kwa Ra.[33]
18-Suna ya kujitenga mbali na shetani wakati wa kusoma Qur’ani
Imeokewa kutoka kwa Al-Halabi kutoka kwa Abu Abdillah (a.s) akisema: “NIlimuuliza kuhusu kujitenga mbali na shetani wakati wa kusoma kila sura itakayoanziwa. Akasema; ndio, utajikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kutokana na shetani mlaaniwa.[34]”
Na imepokelewa kutoka kwa Amirul-Muminina Imamu Ali (a.s) amesema: “Na kujitenga mbali (na shetani) ni vile ambavyo Mwenyezi Mungu amewaamrisha waja wake wakati wa kusoma kwao Qur’ani, kwa kusema: (Na ukisoma Qur’ani Muombe Mwenyezi Mungu akulinde na shetani aliyelaaniwa.). Hivyo atakayejifunza desturi hii kwa ajili ya Mwenyezi Mungu itampelekea kufaulu milele.[35]”
19-Qur’ani ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, ni mara ngapi Mwislamu anatakiwa kuisoma kwa siku
Imepokewa kutoka kwa Abu Abdillah (a.s) amesema: “Qur’ani ni ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake, hivyo inatakiwa kwa Mwislamu kuangalia katika ahadi yake na asome aya 50 kwa kila siku.[36]”
Mimi ninasema; kwa mahesabu mepesi inapatikana natija kwamba kiwango kidogo anachotakiwa muumini kuhitimisha Qur’ani kwa mwaka ni mara tatu. Kwa kuwa idadi ya aya za Qur’ani ni zaidi ya 6000 ambazo atazigawa kwa siku 120, yaani kwa kila baada ya miezi minne, kwa kufumbia macho juhudi zaidi za mwezi wa Ramadhani.
20-Aya za Qur’ani ni hazina hivyo nufaika nazo zote
Imepokewa kutoka kwa Ali Bin Hussein (a.s) akisema: “Aya za Qur’ani ni hazina, (hivyo) kila unapofungua hazina, unatakiwa uangalie yaliyo ndani yake.[37]”
21-Suna ya kusoma Qur’ani majumbani
Imepokewa kutoka kwa Abu Abdillah (a.s) akisema: alisema Amirul-Muuminina Ali (a.s) kwamba: “Nyumba ambayo husomwa Qur’ani ndani yake na anatajwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani yake, huzidi baraka zake na hutembelewa na malaika na kukimbiwa na shetani. Huwaangazia watu wa mbinguni kama vile nyota zinavyowamulikia watu wa dunia. Na nyumba ambayo haisomwi Qur’ani ndani yake na hatajwi Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani yake, huwa na baraka kidogo na hukimbiwa na malaika na kutembelewa na mashetani.[38]”
22-Kupata na kutafuta rizki, hakumzuii mtu kuzingatia usomaji wa Qur’ani
Imepokewa kutoka kwa Abu Abdilla- (a.s) amesema: “Hazuiwi mfanyabiashara kati yenu anayejishughulisha sokoni, wakati anaporejea nyumbani kwake asilale hadi atakaposoma sura katika Qur’ani, basi huandikiwa mema 10 kwa kila mahala pa aya anayoisoma na kufutiwa machafu 10.[39]”
23-Suna ya kusoma kwenye Msahafu, hata kama (msomaji) amehifadhi yale anayoyasoma
Imepokewa kutoka kwa Abu Abdilllah (a.s) akisema: “Atakayesoma Qur’ani katika msahafu, hustarehesha macho yake na wazazi wake wanapunguziwa dhambi hata kama watakuwa makafiri.[40]”
Na kutoka kwa Mtume (saw) amesema: “Hakuna kitu kinamuweza uzito shetani kama mtu kusoma katika Msahafu akitazama.[41]”
Na katika hadithi nyingine anasema: “Kutazama kwenye msahafu (hata) bila ya kusoma, ni ibada.[42]”
Ninasema: na huu ni wadhifa mdogo anaotakiwa kuufanya yule asiyeweza kusoma Qur’ani, lakini tofauti na hapo anatakiwa kusikiliza. Na imepokewa kutoka kwa Is’haq Ibn Ammar kutoka kwa Abu Abdillah (a.s) amesema: “Nilimwambia, niwe fidia kwako, mimi nimehifadhi Qur’ani juu ya mgongo wa moyo wangu, je kuisoma juu ya mgongo wa moyo wangu ni bora au kuangalia kwenye Msahafu? Akasema kuniambia: bali ukiisoma kwa kuangalia kwenye Msahafu ndio bora. Je hujapata kusikia kwamba kuangalia kwenye Msahafu ni ibada?[43]”
24-Suna ya kuwa na nakala ya Msahafu ndani ya nyumba
Kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) amesema; “Inanivutia kuwepo Msahafu ndani ya nyumba, ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu anawafukuzia mashetani.[44]”
25-Suna ya kusoma taratibu na karaka kusoma kwa harakaharaka
Imepokewa kutoka kwa Abdullah Bin Sulaiman amesema: “Nilimuuliza Aba Abdillah (a.s) kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu unayosema (Na soma Qur’ani taratibu) akasema; amesema Amirul-Muuminina (Ali-as) kwamba; aliibainisha kwa uwazi, wala usiiharakishe mithili ya shairi wala kuisoma kwa vina vilivyoparaganyika, lakini ziamsheni kwayo (Qur’ani) nyoyo yenu migumu, na isijekuwa huzuni ya mmoja wenu mwishoni mwa sura.[45]”
Na katika tafsiri ya kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: (Wale tuliowapa kitabu, wakakisoma kama ipasavyo kusomwa….) imepokewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) kwamba: usomaji wa kweli ni kusimama (kidogo) wakati kunapotajwa pepo na moto, akaomba dua sehemu ya kwanza (pepo) na kujiepusha sehemu nyingine (moto).[46]”
Na katika hadithi nyingine kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) amesema: “Hakika Qur’ani haisomwi harakaharaka, bali inasomwa taratibu, na unapopita kwenye aya inayozungumzia pepo, simama kwenye aya hiyo na umuombe pepo Mwenyezi Mungu, na unapopita kwenye aya inayozungumzia moto, simama kwenye aya hiyo na umuombe Mwenyezi Mungu akuepushe na moto.[47]”
26-Suna ya kuisoma kwa huzuni kama vile inamuhutubu mwanadamu na kuheshimu wanayoyafanya watu wa jamii ya Sufiyah kwa kuzimia
Imepokewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) akisema: “Hakika Qur’ani ilishuka kwa huzuni, hivyo isome kwa huzuni.[48]” Na kutoka kwa Hafs amesema: “Sikuona mtu mwenye hofu kubwa kwa nafsi yake kama (Imam) Musa Ibn Ja’far (a.s) wala mtu mwenye kutaraji (pepo) kama yeye. Kisomo chake kilikuwa cha huzuni, na anaposoma ni kama vile anamuhutubu mwanadamu.[49]”
Na kutoka kwa Jabir kutoka kwa Abu Ja’far (a.s) amesema: “Nilisema, (kuna) watu wanaposoma sehemu ya Qur’ani au wanapoizungumzia baadhi yao huzimia kiasi kwamba lau mmoja wao akikatwa mkono au mguu wake hawezi kuhisi (uchungu wake), akasema; subhanallah! Ni watu gani hawa, hakika hali hiyo ni ulaini, wepesi, kutokwa na machozi na hofu.[50]”
27-Suna ya kuinua sauti wakati wa kusoma Qur’ani
Imepokewa kutoka kwa Muawiyah Bin Ammar akisema: “Nilisema kumwambia Abu Abdillah (a.s); (kuna) mtu anayeona kuwa hajafanya chochote katika dua na katika kisomo hadi ainue sauti, akasema; hakuna ubaya. Hakika Ali Ibn Hussein (a.s) alikuwa ana sauti nzuri (sana) katika kusoma Qur’ani na alikuwa akiinua sauti yake hadi wanamsikia watu wa nyumbani kwake. Naye Abu Ja’far (a.s) alikuwa ana sauti nzuri (sa) katika kusoma Qur’ani n alikuwa anaposimama (katika swala) ya usiku na akasoma Qur’ani, huinua sauti yake (kiasi kwamba) mtu aliyepita njiani miongoni mwa wenye kuomba maji na wengineo, walikuwa wanasimama na kusikiliza kisomo chake.[51]”
28-Uharamu wa kusoma Qur’ani kwa sauti mbaya
Kutoka kwa Abu Abdillah (a.s) amesema: “Alisema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw); someni Qur’ani kwa mahadhi ya Kiarabu na sauti zake. Na ole wenu na kusoma kwa mahadhi ya watu wa ufuska na watu wa madhambi makubwa, kwani baada yangu watakuja watu watakuwa wanaikariri Qur’ani mithili ya nyimbo, makelele na sauti za vilio, lakini Qur’ani haitapanda kufika mioyo yao iliyopinduka na hata mioyo ya wafuasi wao.[52]”
29-Wajibu wa kunyamanza kwa ajili ya kisomo cha Qur’ani, kiakhlaqi na suna, ispokuwa kwenye swala
Imepokewa kutoka kwa Abu Abdillah Ibn Abi Ya’fur kutoka kwa Abu Abdillah (a.s) amesema: “Nilimwambia, (kuna) mtu anasoma Qur’ani, je ni lazima kwa anayemsikiliza kusalia kimya na kuisikiliza? Akasema, ndio! Itakaposomwa Qur’ani karibu yako ni lazima unyamanze na kuisikiliza.[53]”
Na katika hadithi ya Zurarah kutoka kwa Abu Ja’far (a.s) amesema: “Itakaposomwa Qur’ani katika swala ya faradhi nyuma ya imam, isikilizeni na msalie kimya, ili mrehemewe.[54]”
30-Ni suna kuhitimisha Qur’ani mara moja ndani ya kila mwezi
Imepokewa kutoka kwa Muhammad Ibn Abdillah amesema: “Nilimwambia Abu Abdillah (a.s) kwamba; Nisome Qur’ani usiku? Akasema (sipendelei uisome katika muda ulio chini ya mwezi.[55])”
31-Ni suna kutoa thawabu za kisomo kwa Maasumina (a.s) ili kuzidisha malipo
Imepokewa kutoka kwa Ali Ibn Al-Mughira kutoka kwa Abul-Hassan (a.s) kwamba: “Nilisema inapofika siku ya (Idi) Al-Fitri huwa ninahitimisha Qur’ani kwa ajili ya Mtume[56] (saw), na Ali (a.s), na Fatwimah (a.s) kisha kwa maimamu (a.s) hadi ninapomalizia kwako…. Ni hali gani hiyo inayonipata? Akasema; ni vyema kwako uwe nao (maasumina) siku ya Kiama. Nikasema, Mwenyezi Mungu ni Mkubwa, hivi kweli ninastahiki haya? Akasema; ndio mara tatu.[57]“
32-Ni suna kulia au kujiliza wakati wa kusikiliza Qur’ani
Imepokewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) amesema: “Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwajia vijana wa kabila la Answar akasema: ninataka nikusomeeni (Qur’ani) atakayelia basi atalipwa pepo. Akasoma sehemu ya mwisho wa surat Zumar inayosema: (Na waliokufuru wataongozwa kuelekea Jahannamu kwa makundi…..) Hadi mwisho wa sura hiyo, vijana wale wakalia wote ispokuwa kijana mmoja. Akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nimejililisha lakini macho yangu hayakutoa machozi. Mtume akasema: mimi nitarejea tena (kusoma), (hivyo) atakayejiliza basi ataingia peponi, akarejea tena kusoma, wakalia watu wote na yule kijana akajililisha, (hivyo) wakawa wameingia wote peponi.[58]”
33-Elimu yote imo ndani ya Qur’ani
Imepokewa kutoka kwa Imam Ali (a.s) kwamba aliambiwa: “Je mnacho chochote katika wahyi? Akasema: hapana, ninaapa kwa yule aliyepasua mbegu na akaumba viumbe, ispokuwa Mwenyezi humpa (wahyi) mja mwenye uelewa katika kitabu chake.[59]”
Imepokewa kutoka kwa Ibrahim Ibn Abbas amesema: “Sikuwahi kumuona Imam Ridha (a.s) akiulizwa kitu chochote ispokuwa alikuwa anajua elimu yake. Na sikuona mtu mwenye uelewa zaidi yake wa vitu vilivyokuwa zama za mwanzoni hadi katika zama na kipindi chake. Na Ma’mun alikuwa akimjaribu kwa maswali kuhusu kila jambo na alikuwa akimjibu. Na maneno yake yote, majibu na mifano vilikuwa vinatokana na Qur’ani.[60]” Na katika kitabu cha Nahjul-Balaghah imepokewa kwamba: “Hiyo ndio Qur’ani zungumzisheni, haitozungumza, ninakuelezeni kuihusu (hiyo Qur’ani), Ndio! Hakika ndani yake kuna elimu za yajayo na hadithi za waliopita na tiba ya maradhi yenu na mpingilio kati yenu.[61]”
34-Qur’ani ni tiba kwa kila ugonjwa
Imepokewa kutoka kwa Abu Abdillah (a.s) amesema: “Lau kama utasoma Al-Hamdu kwa maiti mara sabini kisha akarejeshwa roho (uhai) haitakuwa kitu cha kushangaza.[62]”
35-Ndani ya Qur’ani kuna usafishaji wa mioyo
Imepokewa kutoka kwa Mtume (saw) akisema: “Hakika hii mioyo hupata kutu kama vile chuma kinavyopata kutu, na kuzitakatisha, ni kusoma Qur’ani.[63]”
36-Kuzidisha kuisoma ndani ya mwezi wa Ramadhani
Imepokewa kutoka kwa Abu Ja’far (a.s) amesema: “Kila kitu kina msimu, na msimu wa Qur’ani ni mwezi wa Ramadhani.[64]”
Na imepokewa kutoka kwa Ali Ibn Hamzah amesema: “NIliingia kwa Abu Abdillah (a.s) Abu Basir akamwambi: niwe fidia yako, nisome Qur’ani (mara moja) ndani ya Ramadhani usiku? Akasema: hapana. Akasema, (kwa) nyusiku mbili? Akasema: hapana. Akasema: (kwa) nyusiku tatu? Akaashiria kwenye mkono wake kisha akasema: ewe Aba Muhammad hakika Ramadhani ina haki na heshima hailingani chochote na miezi mingine.[65]”
37-Kusoma Qur’ani kufanyike ipasavyo
Katika tafsiri ya Mwenyezi Mungu inayosema: “Wale tuliowapa Kitabu wakakisoma ipasavyo…Surat Baqara aya ya 121. Amesema Imam Swadiq (a.s): Wanasoma taratibu aya zake, wanaelewa na wanafahamu hukumu zake, na wanataraji ahadi zake (njema) na wanaogopa indhari zake huku wakizingatia visa vyake. Na wanaamrishika kwa amri zake na wanakatazika kwa makatazo yake, Wallahi sio kuhifadhi aya zake na kutalii herufi zake na kusoma sura zake, wala kutalii mafungu na khumusi zake. Kwa kuhifadhi herufi zake na wakapoteza sheria zake, bali ni kuzingatia aya zake na kutekeleza hukumu zake kama Mwenyezi Mungu alivyosema: (Hiki Kitabu tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazingatie aya zake…[66]”
38-Maulama hawaishibi Qur’ani
Imepokewa kutoka kwa Mtume (saw) amesema katika hadithi inayozungumzia Qur’ani kwamba: “Ni kamba imara ya Mwenyezi Mungu, ni ukumbusho thabiti, njia iliyo nyoka nayo ndio ambayo haipotei kwayo mioyo na hawaishibi maulama na ndimi hazihitilafiani kwayo…Na hayaishi maajabu yake, atakayeizungumzia mwamini na atakayehukumu kwayo (Qur’ani) atapatia atakayeifanyia kazi atalipwa na atakayelingania (watu) kwenye Qur’ani) ataongozwa kwenye njia iliyo nyooka.[67]”
39-Qur’ani katika Nahajul-Balaghah
Inasema: “Jifundisheni Qur’ani kwani yenyewe ni hadithi bora, na jielimisheni ndani yake kwani yenyewe ni msimu wa mioyo, na jiponyeni kwa nuru yake kwani yenyewe ni ponyo ya mioyo na isomeni vizuri hakika yenyewe ina visa vyenye manufaa. Na hakika mtendaji asiyefuata elimu yake (ya Qura’n) ni sawa na mjinga aliyetahayari ambaye hazinduki kutoka katika ujinga wake, bali hoja juu yake itakuwa kubwa na hasara yake haiepukiki naye atalaumiwa kwa Mwenyezi Mungu.[68]”
40-Dua ya Imam Sajjad (a.s) wakati wa kuhitimisha Qur’ani
اللهم إنك أعنتني على ختم كتابك الذي أنزلته نوراً وجعلته مهيمناً على كل كتاب أنزلته وفضلته على كل حديث قصصته وفرقاناً فرقت بين حلالك وحرامك وقرآناً أعربت به عن شرايع أحكامك وكتاباً فصّلته لعبادك تفصيلاً.
Ewe Mola wangu! Hakika umenisaidia kuhitimisha Kitabu chako ambacho ulikiteremsha kuwa ni nuru na umekifanya mlinzi wa kila kitabu ulichokiteremsha. Na umekiboresha juu ya kila hadithi uliyoisimulia. Na ni kitenganishi kwacho umetenganisha kati ya halali yako na haramu yako. Qur’ani ambayo kwayo umeiweka wazi sheria ya hukumu yako. Kitabu umekipambanuwa kwa waja wako upambanuzi wa wazi.
ووحياً أنزلته على نبيك محمد صلواتك عليه وآله تنزيلاً وجعلته نوراً نهتدي من ظلم الضلالة والجهالة باتباعه وشفاء لمن أنصت بفهم التصديق إلى استماعه وميزان قسط لا يحيف عن الحق لسانه، ونور هدى لا يطفأ عن الشاهدين برهانه وعلم نجاة لا يضل من أمَّ قصد سنته، ولا تنال أيدي الهلكات من تعلق بعروة عصمته،
Ni Wahyi ulio uteremsha uteremsho kwa Nabii wako Muhammad Rehma Zako zimfikie na ziwafikiye Aali zake. Umeifanya kuwa nuru ituongoze katika giza ya upotevu na ujinga kwa kuifuata. Kiponyesho kwa mwenye kuisikiliza kwa kuifahamu na kuisadiki. Ni mizani ya kiadilifu isiyopotoka ulimi wake na kuwa mbali na haki. Nuru ya uongofu ambayo Burhani yake haiwazimikii watizamaji wake. Na alama ya uokovu ambayo hapotei mwenye kufuata mafunzo yake. Wala haitomfikia mikono ya maangamizi mwenye kujiambatanisha na kishiko chake cha ulinzi.
اللهم فإذا أفدتنا المعونة على تلاوته، وسهلت حواسي ألسنتنا بحسن عبارته، فاجعلنا ممن يرعاه حق رعايته، ويدين لك باعتقاد التسليم لمحكم آياته، ويفزع إلى الإقرار بمتشابهه وموضحات بيّناته،
Ewe Mola wangu! kwa vile umetusaidia kuisoma. Na umeturahisishia ugumu wa ndimi zetu kwa uzuri wa ibara yake hivyo basi tufanye tuwe miongoni mwa wanaoichunga haki ya kuichunga na wakutumikia kwa itikadi ya kusalimu amri ya aya zake zilizothabiti waombao kimbilio kwa kuzikubali zile aya mutashabih na zile ufafanuzi wake uko bayana.
اللهم إنك أنزلته على نبيك محمد صلى الله عليه وآله مجملاً، وألهمته علم عجائبه مكملاً وورثتنا علمه مفسراً وفضلتنا على من جهل علمه، وقويتنا عليه لترفعنا فوق من لم يطق حمله،
Ewe Mola wangu! Hakika wewe umeiteremsha kwa Nabii wako Muhammad Rehema za mungu zimfikiye yeye na Aali zake kwa ujumla. Na umeturithisha sisi Elimu yake tukiwa wafasiri. Na umetuboresha juu ya wasioijuwa elimu yake. Umetupa nguvu juu yake ili utunyanyuwe juu ya wasio weza kuibeba.
اللهم فكما جعلت قلوبنا له حملة وعرفتنا برحمتك شرفه وفضله، فصل على محمد الخطيب به، وعلى آله الخزّان له، واجعلنا ممن يعترف بأنه من عندك، حتى لا يعارضنا الشك في تصديقه، ولا يختلجنا الزيغ عن قصد طريقه،
Ewe Mola wangu! kama vile umezifanya nyoyo zetu kuwa zenye kuibeba. Na kwa rehema zako umetutambulisha utukufu na ubora wake. Basi msaliye Muhammad, muhubiri wake na Aali zake wahifadhi wa Qur’ani. Utujaalie kuwa miongoni mwa wanaotambuwa kuwa yatoka kwako. Ili isituzukiye shaka katika kuisadiki. Wala upotovu usitutikise na kututowa nje ya njia yake nyofu.
اللهم صلّ على محمد وآله واجعلنا ممن يعتصم بحبله، ويأوي من المتشابهات إلى حرز معقله، ويسكن في ظل جناحه، ويهتدي بضوء صباحه، ويقتدي بتبلج أسفاره، ويستصبح بمصباحه ولا يلتمس الهدى في غيره،
Ewe Mola wangu!, mswaliye Muhammad na Aali Zake. Na tujaaliye sisi kuwa miongoni mwa wanaoshikamana na kamba yako, na wakimbiliao kutoka kwenye aya mutashabihati kwenda kwenye ngome yake madhubuti na kuketi kwenye kivuli cha bawa lake, na aongokaye na mwanga wake wa asubuhi. Aongokaye na kuchomoza kwa mng'aro wake. Anamulika kwa taa yake. Wala hatafuti uongofu katika kitu kingine.
اللهم وكما نصبت به محمداً عَلَماً للدلالة عليك وأنهجت بآله سُبل الرضا إليك، فصلّ على محمد وآله، واجعل القرآن وسيلة لنا إلى اشرف منازل الكرامة، وسُلّماً نعرج فيه إلى محل السلامة وسبباً نجزي به النجاة في عرصة القيامة، وذريعة نقدم بها على نعيم دار المقامة،
Ewe Mola wangu! Kwa hiyo Qur’ani umemweka Muhammad kuwa alama ya kukujuwa wewe. Na kupitia Ahlul-Bayt wake umeweka wazi njia za ridhaa zako. Msaliye Muhammad na Aali Zake na ifanye Qur’ani kwetu kuwa njia za kwenye daraja la utukufu. Na iwe ngazi tuipandayo kwenda mahali pa salama. Na iwe sababu tutakayolipwa uokovu kwenye uwanja wa kiyama. Na njia ambayo kwayo tutazifikia neema za nyumba ya kudumu.
اللهم صل على محمد وآله، واحطط بالقرآن عنا ثقل الأوزار، وهب لنا حسن شمائل الإبرار، واقف بنا آثار الذين قاموا لك به آناء الليل وأطراف النهار، حتى تطهرنا من كل دنس بتطهيره، وتقفوا بنا آثار الذين استضاؤوا بنوره، ولم يلْههم الأمل عن العمل فيقطعهم بخدع غروره،
Ewe Mola wangu! Msaliye Muhammad na Aali Zake. Kwa Qur’ani tupunguziye uzito wa dhana utupe sifa njema za watu wema na tufanye tufate athari za waliosimama kwa ajili yako nyakati za usiku na mwisho wa mchana. Ili ututakase na kila uchafu kwa utakaso wake. Utufanye tufate athari ya walioangaza kwa nuru yake. Wala matumaini hayakuwa zuiya kutenda kazi iliyowatenga mbali kwa vitimbi vya udanganyifu wake.
اللهم صل على محمد وآله، واجعل القرآن لنا في ظلم الليالي مؤنساً، ومن نزعات الشيطان وخطرات الوساوس حارساً، ولأقدامنا عن نقلها إلى المعاصي حابساً، ولألسنتنا عن الخوض في الباطل من غير ما آفة مخرساً، ولجوارحنا عن اقتراف الآثام زاجراً، ولما طوت الغفلة عنا من تصفح الاعتبار ناشراً، حتى توصل إلى قلوبنا فهم عجائبه، وزواجرَ أمثاله التي ضعفت الجبال الرواسي على صلابتها عن احتماله،
Ewe Mola wangu! Ijaliye Qur’ani iwe yenyekutuliwaza katika kiza cha usiku. Na yenye kutuhifadhi na upotevu wa shetani na hatari ya wasiwasi. Na yenye kuzuiya nyayo zetu zisiende kwenye maasi. Na yenye kuzuiya ndimi zetu kuingia kwenye batili bila kupatwa na maradhi. Na yenye kukemea na kutuzuia viungo vyetu kutenda madhambi. Na yenye kutuzindua kutokana na yale yaliyotughafilisha kuzingatia. Ili uufikishe ufahamu wa maajabu yake kwenye nyoyo zetu. Na tuifahamu mifano ambayo majabali thabiti yalishindwa kuibeba kwa ugumu wake.
اللهم صل على محمد وآله وأدم بالقرآن صلاح ظاهرنا، واحجب به خطرات الوساوس عن صحة ضمائرنا واغسل به درن قلوبنا، وعلائق أوزارنا، واجمع به منتشر أمورنا وارو به في موقف العرض عليك ظمأ هواجرنا، واكسنا به حلل الأمان يوم الفزع الأكبر في نشورنا،
Ewe Mola wetu! Idumushe kheri ya dhahiri yetu kwa Qur’ani. Na kwayo izuiye hatari ya wasiwasi kwenye usalama wa dhamiri zetu, na uondoshe uchafu wa nyoyo zetu na vikwazo vya madhambi yetu kwa Qur’ani. Na kwayo uyakusanye mambo yetu yaliyo sambaratika, na utuondolee kiu katika kisimamo siku ya kuja kwako. Na utuvishe kwa Qur’ani mapambo ya Amani siku ya mfadhaiko mkubwa katika kufufuliwa kwetu.
اللهم صل على محمد وآله، واجبر بالقرآن خلتنا من عدم الإملاق، وسق به ألينا رغد العيش خصب سعة الأرزاق وجنبنا به الضرائب المذمومة، ومداني الأخلاق، واعصمنا به من هوة الكفر ودواعي النفاق، حتى يكون لنا في القيامة إلى رضوانك وجنانك قائداً، ولنا في الدنيا عن سخطك وتعدي حدودك ذائداً، ولما عندك بتحليل حلاله وتحريم حرامه شاهداً،
Ewe Mola wangu! Mrehemu Muhammad na Ali Zake. Rekebisha kwa Qur’ani upungufu wetu tusiwe mafakiri. Kwa Qur’ani tusukumiye maisha ya raha na wasaa wa riziki. Tuepushe kwayo na tabia mbaya na mwenendo duni. Tuhifadhi kwa Qur’ani tusiingiye ndani ya shimo la maangamizi kufuru na mwendo wa kinafiki. Ili iwe mwongozo uelekezao kwenye maridhawa yako na bustani zako siku ya kiyama. Na iwe kwetu mlinzi hapa duniani dhidi ya makasiriko yako na kukiuka mipaka yako. Na iwe kwa yale uliyonayo kwa kuhalalisha halali yake na kuharamisha haramu yake shahidi.
اللهم صل على محمد وآله، وهوّن بالقرآن عند الموت على أنفسنا كرب السياق وجهد الأنين، وترادف الحشارج، إذا بلغت النفوس التراقي[وَقِيلَ مَنْ رَاقٍ]، وتجلّى ملك الموت لقبضها من حجب الغيوب ورماها عن قوس المنايا بأسهم وحشة الفراق، وداف لها من دعاف مرارة الموت كأساً مسمومة المذاق، ودنا منا إلى الآخرة رحيل وانطلاق، وصارت الأعمال قلائد في الأعناق، وكانت القبور هي المأوى إلى ميقات يوم التلاق،
Ewe Mola wangu! Mrehemu Muhammad na Aali Zake na kwa Qur’ani urahisishe umauti nafsini mwetu wakati wa kufa. Na usumbufu wa kukokotwa (Roho) Uuguaji. Na taabu ya mauguzi, na mfuatano wa kutatarika. (Ifikapo roho kooni na itasemwa: Mganga ni nani?) Atajitokeza Malaika wa umauti ili aichukue toka nyuma ya pazia ya mambo yasiyojulikana. Na kuitupa toka upinde wa umauti kwa mshale wa kuachwa peka na kuwa changanyiya sumu iuwayo kwenye kikombe chenye mwonjo wa sumu wakati msafara wa kuelekea akhera ukitusogelea. Kazi zitakuwa ukosi wa shingo makaburi yatakuwa ndio kimbilio mpaka wakati wa siku ya kukutana.
اللهم صل على محمد وآله، وبارك لنا في حلول دار البلى، وطول المقامة بين أطباق الثرى، واجعل القبور بعد فراق الدنيا خير منازلنا، وافسح لنا برحمتك في ضيق ملاحدنا، ولا تفضحنا في حاضر القيامة بموبقات آثامنا، وارحم بالقرآن في موقف العرض عليك ذلّ مقامنا، وثبت به عند اضطراب جسر جهنم يوم المجاز عليها زلل أقدامنا، ونجنا به من كل كرب يوم القيامة، وشدائد أهوال يوم الطامة وبيّض وجوهنا يوم تسود وجوه الظلمة في يوم الحسرة والندامة، واجعل لنا في صدور المؤمنين وداً، ولا تجعل الحياة علينا نكداً،
Ewe Mola wangu! Mrehemu Muhammad na Aali zake. Na utubariki wakati wa kuingia nyumba ya kuoza na makazi ya muda mrefu kati ya tabaka za udongo. Yajaaliye makaburi baada ya kuiaga dunia yawe mafikio yetu mema tupanulie mbano wa mwana ndani zetu kwa rehema zako. Usitufedheheshe mbele ya walio hudhudhiria siku ya Kiyama kwa sababu ya madhambi yetu ya angamizayo. Kwa Qur’ani irehemu hali yetu duni katika kikao cha kuletwa mbele yako. Kwa Qur’ani zithibitishe nyayo zetu zisiteleze wakati daraja la Jehannam litakapoyumba yumba. Kwayo ing'arishe giza ya makaburi yetu kabla ya kufufuka. Utuokowe kwa Qur’ani na kila taabu ya siku ya Kiyama na shida za kutisha siku ya maafa. Zing'arishe nyuso zetu siku ambayo nyuso za wadhalimu zitakuwa nyeusi siku ya kuhasirika na majuto. Utujaaliye upendo ndani ya nyoyo za waumini. Usiyafanye maisha kwetu kuwa ya shida.
اللهم صل على محمد عبدك ورسولك، كما بلغ رسالتك، وصدع بأمرك ونصح لعبادك. اللهم اجعل نبينا صلواتك عليه وعلى آله يوم القيامة أقرب النبيين منك مجلساً، وأمكنهم منك شفاعة، وأجلّهم عندك قدراً، وأوجههم عندك جاهاً،
Ewe Mola wangu! mrehemu Muhammad mja wako na mjumbe wako kwa vile ameifikisha risala yako na alitekeleza amri yako. Aliwanasihi waja wako. Ewe Mola wangu! Mjaaliye Nabii wetu Rehema Zako ziwe juu yake, na juu ya Aali zake - Awe karibu mno na wewe siku ya kiyama miongoni mwa Manabii watakaokuwa karibu ya kikao. Na mwenye uwezo mkubwa sana kwako wakuombea. Mwenye Enzi kubwa miongoni mwao kwako. Mwenye cheo kikubwa mno mbele yako.
اللهم صل على محمد وآل محمد، وشرّف بنيانه، وعظم برهانه، وثقل ميزانه، وتقبل شفاعته وقرب وسيلته، وبيض وجهه وأتم نوره وارفع درجته، وأحينا على سنته وتوفّنا على ملته، وخذ بنا منهاجه، واسلك بنا سبيله، واجعلنا من أهل طاعته، واحشرنا في زمرته، وأوردنا حوضه، واسقنا بكأسه، وصل اللهم على محمد وآله صلاة تبلغه بها أفضل ما يأمل من خيرك وفضلك وكرامتك إنك ذو رحمة واسعة وفضل كريم،
Ewe Mola wangu! Mrehemu Muhammad na Aali wa Muhammad. Itukuze nyumba yake, Bur'hani yake itukuze, Mizani yake ipe uzito, ya kubali maombezi yake usogeze karibu wasila wake, ufanye uwe mweupe uso wake, ikamilishe nuru yake iinue daraja yake. Tufanye sisi tuishi na sunna yake, tufishe tukiwa katika mila yake, tupeleke tufikishe kwenye njia yake. Tupitishe njia yake. Tujaaliye tuwe miongoni mwa watu watii wake. Tufufuwe katika kikundi chake tuelekeze kwenye dimbwi lake, tunyweshe kwa bilauri yake. Rehemu Muhammad na Aali zake. Rehema ambayo utamfikisha nayo kwenye ubora asio uwazia miongoni mwa kheri na fadhila zako, na heshima zako. Hakika wewe ni mwenye Rehma kubwa na fadhila tukufu
اللهم اجزه بما بلّغ من رسالاتك وأدّى من آياتك، ونصح لعبادتك، وجاهد في سبيلك، أفضل ما جزيت أحداً من ملائكتك المقربين، وأنبيائك المرسلين المصطفين، والسلام عليه وعلى آله الطاهرين ورحمة الله وبركاته
Ewe Mola wangu! mlipe kwa aliyoyafikisha katika jumbe zako. Na amefikisha aya zako, amepigana jihadi katika njia yako malipo yaliyo bora umepata kumlipa yeyote miongoni mwa Malaika wako wa karibu na Manabii wako walio Mursali wateule. Amani imfikie yeye na iwafikiye watoto wake watakatifu wema, na rehema za Mungu na baraka zake[69].
Kimeandikwa na:
Ayatollah, Sheikh Muhammad Yaqoobi
Kimetarjumiwa na:
Ustadhi, Abdallah Khamis Salum
Box, 113, Kalenge Kigoma Tanzania.
[1]. Wasaailush-Shia, Kiatabu Al-Swalat Abewaabu Qira’atul-Qur’ani walaw fi ghairi al-Swalat. Mlango wa 1, hadithi ya 4,5,6,15,11,16 kwa Utaratibu.
[2]. Wasaailush-Shia, Kiatabu Al-Swalat Abewaabu Qira’atul-Qur’ani walaw fi ghairi al-Swalat. Mlango wa 1, hadithi ya 4,5,6,15,11,16 kwa Utaratibu.
[4]. Wasaailush-Shia, Kiatabu Al-Swalat Abewaabu Qira’atul-Qur’ani walaw fi ghairi al-Swalat. Mlango wa 1, hadithi ya 4,5,6,15,11,16 kwa Utaratibu.
[5]. Wasaailush-Shia, Kiatabu Al-Swalat Abewaabu Qira’atul-Qur’ani walaw fi ghairi al-Swalat. Mlango wa 1, hadithi ya 4,5,6,15,11,16 kwa Utaratibu.
[6]. Wasaailush-Shia, Kiatabu Al-Swalat Abewaabu Qira’atul-Qur’ani walaw fi ghairi al-Swalat. Mlango wa 1, hadithi ya 4,5,6,15,11,16 kwa Utaratibu.
[7]. Ushahidi uliotangulia.
[8]. Ushahidi uliotangulia.
[9]. Ushahidi uliotangulia, kwenye hadithi ya 2,3,6 kwa utaratibu.
[10]. Ushahidi yliotangulia, kwenye mlango wa 5 hadithi ya 3.
[11]. Ushahidi uliotangulia, hadithi ya 2.
[12]. Ushahidi uliotangulia, hadithi ya 6.
[13]. Ushahidi uliotangua mlango wa 4 hadithi ya 1.
[14]-Ushahidi uliotangulia mlango wa 5 hadithi ya 3.
[15]. Ushahidi uliotangulia, hadithi ya 2.
[16]. Bihaarul-Anwaar 82/20.
[17]-Wasaailush-Shia, Kitabu al-Twaharah, Abewaabu Swalaatil-Janaazah, mlango wa 57, hadithi ya 5.
[18]-Jaamiul-Ahaadithush-Shia, Kiatabus-Swalat, Abewaabu Ziyaaratul-Qubuur, mlango wa 2, na humu kuna makumi ya hadithi.
[19]-Al-Kaafi juzu ya 2 ukurasa wa 604.
[20]-Nahajuls-Saadah juzu ya 7 ukurasa wa 223.
[21]-Wasaailush-Shia, Kitabus-Swalaat Abewabu Ahkamul-Masaajid, mlango wa 3 hadithi ya 3.
[22]-Nao ni wale ambao wanafuatilia sana sheria za tajweed walizoziweka wao, na wakasahau maana ya kile wanachokisema.
[23]- Wasaailush-Shia, Kitabus-Swalaat Abewabu Qurraul-Qur’ani walau fii ghairis-Swalaat, mlaango wa 8 hadithi ya 1-3.
[24]-Dalili iliyotangulia, mlango wa 11 hadithi ya 18.
[25].
[26]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 11, hadithi ya 2.
[27]. Dalili iliyotangulia, hadithi ya 8.
[28]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 11, hadithi ya 1.
[29]. Dalili iliyotangulia, hadithi ya 10.
[30]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 17, hadithi ya 2.
[31]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 12, hadithi ya 3.
[32]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 13, hadithi ya 1.
[33]. Dalili iliyotangulia hadithi ya 3.
[34]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 14, hadithi ya 2.
[35]. Dalili iliyotangulia, hadithi ya 1.
[36]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 15, hadithi ya 1.
[37]. Dalili iliyotangulia, hadithi ya 6.
[38]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 16, hadithi ya 2.
[39]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 11, hadithi ya 6.
[40]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 19, hadithi ya 1.
[41]. Dalili iliyotagulia, hadithi ya 2.
[42]. Dalili iliyotangulia, hadithi ya 6.
[43]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 19, hadithi ya 4.
[44]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 20, hadithi ya 1.
[45]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 21, hadithi ya 1.
[46]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 27, hadithi ya 7.
[47]. Dalili iliyotangulia, hadithi ya 3.
[48]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 22, hadithi ya 1.
[49]. Dalili iliyotangulia, hadithi ya 3.
[50]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 25, hadithi ya 1
[51]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 23, hadithi ya 2.
[52]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 24, hadithi ya 1.
[53]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 26, hadithi ya 4.
[54]. Dalili iliyotangulia, hadithi ya 4.
[55]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 27, hadithi ya 1.
[56]. Miongoni mwa aliyoyasoma ndani ya mwezi wa Ramadhan.
[57]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 28, hadithi ya 1.
[58]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 29, hadithi ya 1.
[59]. Tafsiru al-Swafi juzu ya 1 ukurasa wa 39.
[60]. Dalili iliyotangulia, mlango wa 27, hadithi ya 6.
[61]. Hotuba ya 158 katika juzu ya kwanza.
[62]. Al-Kafi juzu ya 2 ukurasa 624.
[63]. Irshaadul-Quluub ukurasa wa 78.
[64]. Thawaabul-A’maal juzu ya 1 ukurasa 129, mlango wa thawabu za kusoma Qur’ani.
[65]. Wasaailush-Shia, Kitabus-Swalat, Abewaabu Qiraatul-Qur’ani fii Ghairis-Swalaat, mlango wa 27, hadithi ya 3.
[66]. Mizanul Fi Tafsiril-Qur’ani juzu ya 1 ukurasa wa 260.
[67]. Sunanud-Darimi juzu ya 2 ukurasa wa 435, kitabu cha fadhila za Qur’ani, na mfano wake katika vitabu maalumu.
[68]. Nahajul-Balagha juzu ya 1 hotuba ya 110.
[69]. Asw-Swahiifat As-Sajjadiyah, Dua yake pindi anahittmishapo Qur’ani.