MAISHA KATIKA HIMAYA YA QUR’ANI
MAISHA KATIKA HIMAYA YA QUR’ANI
Kwa hakika nimeyapitia maisha nikiwa katika himaya ya Qur’ani na kiashi katika ulinzi wake kwa miaka kadhaa. Ujanani mwangu nilikuwa nikihitimisha Qur’ani mara ishirini mpaka mara ishini na moja kwa mwaka. Mpaka ilifikia hatua nyama yangu, na damu yangu, na fikra zangu, ulimi wangu na moyo wangu vikachanganyikana na Qur’ani. Lakini pia, pamoja na kuisoma, nilikuwa nikisoma kwa umakini tafsiri mbili za Qur’ani, ambazo mwenyewe ninakiri wazi kwamba, zilikuwa na mchango mkubwa katika kujenga shakhsia yangu kielemu na kifikra, tafsiri hizo ni Al-Mizan na Fii dhilaalil Qur’an, nilizisoma hadi nikazimaliza na nikaandika muhtasari wa vichwa vya habari vya fikra zilizomo ndani ya tafsiri hizo ili kuzirejea kila mara, na hivyo zile fikra hujapika akilini mwangu kama zilivyo kuwa nikinijia zile nyakati zenye kufurahisha.
Lakini kipi nilicho kipata katika himaya ya Qur’ani? na kipi atakacho kipata atakaye ishi katika ulinzi wake? Bila shaka atauona ukubwa na utukufu wa Mwenyezi Mungu aliye tukuka ukidhihiri katika aya zake, na katika sheria zake, na katika miongozo yake na uwezo wake juu ya kila kitu, kwani ardhi yote iko mikononi mwake, mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kulia, na utukufu wote ni wake, na ufalme ni wake peke yake, yeye ndiye anaye irithi ardhi na walio juu yake na kwake ndiko watarejeshwa waja, naye yuko karibu nao kuliko mshipa wa shingoni mwao, naye huingia kati ya mtu na moyo wake, na hakuna anaye miliki manufaa wala madhara kwa ajili ya kitu chochote isipokuwa kwa idhini yake. Basi kila kitu hudogeka mbele ya mbeba Qur’ani. Kila kisicho kuwa Mwenyezi Mungu hata kama dhahi yake itafikia adhama gani, au watawala na wafuasi wake wakamkuza na kumtukuza kiasi gani, lakini uwezo wa Mwenyezi Mungu utavimeza vyote walivyo vibuni, si Iram wenye majumba marefu, wala Firauni mwenye vigingi, wala watu wenye mahazina ambayo funguo zake hubebwa na watu wenye nguvu. Ama mtu wa Qur’ani nguvu yake imeunganika na nguvu ya Mwenyezi Mungu, hivyo hamuogopi asiye kuwa yeye. Mwenyezi Mungu anasema:
[مَثَلُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّهِ أَوْلِيَاء كَمَثَلِ الْعَنكَبُوتِ اتَّخَذَتْ بَيْتًا وَإِنَّ أَوْهَنَ الْبُيُوتِ لَبَيْتُ الْعَنكَبُوتِ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ]
“Mfano wa wale waliofanya waungu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kama mfano wa buibui ajitandiaye nyumba, na bila shaka nyumba iliyo mbovu kuliko zote ni nyumba ya buibui, laiti wangelijua”[1], na “mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu atakifanya kila kitu kumuogopa”[2].
na hapo ndipo utayaona hayo madola yenye nguvu ambayo: “zikaoenekana mbele yake, kwa uchawi wao zikienda mbio”[3], na kuwa yanaweza kufanya kila yakitacho, yakiporomoka na kuyeyuka kama chumvi ndani ya maji, bila ya vita wala adui kudhihiri. Lakini Mwenyezi Mungu anakueleza sababu ya kuteketea kwao kwa kusema:
[فَأَتَى اللّهُ بُنْيَانَهُم مِّنَ الْقَوَاعِدِ فَخَرَّ عَلَيْهِمُ السَّقْفُ مِن فَوْقِهِمْ وَأَتَاهُمُ الْعَذَابُ مِنْ حَيْثُ لاَ يَشْعُرُونَ، ثُمَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يُخْزِيهِمْ وَيَقُولُ أَيْنَ شُرَكَآئِيَ الَّذِينَ كُنتُمْ تُشَاقُّونَ فِيهِمْ قَالَ الَّذِينَ أُوتُواْ الْعِلْمَ إِنَّ الْخِزْيَ الْيَوْمَ وَالْسُّوءَ عَلَى الْكَافِرِينَ]
“Walifanya vitimbi wale walio kuwa kabla yao, basi Mwenyezi Mungu akayasukua majengo yao kwenye misingi, ndipo dari zikawaangukia kutoka juu yao na ikawafikia adhabu kutoka wasiko kujua. Kisha siku ya Kiyama atawahizi na atasema: Wako wapi hao washirika wangu kwa ajili yao mlikuwa mkigombana (na manabii?) Watasema wale walio pewa elimu: Hakika hizaya na msiba mkubwa leo vitawafikia makafiri”[4].
Na ataiona ahadi ya Mwenyezi Mungu na utulivu wake kwa waumini kwamba mwisho mwema utakuwa wao, lakini hiyo ni baada ya:
[مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاء وَالضَّرَّاء وَزُلْزِلُواْ حَتَّى يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُواْ مَعَهُ مَتَى نَصْرُ اللّهِ أَلا إِنَّ نَصْرَ اللّهِ قَرِيبٌ]
“iliwapata shida na madhara na wakatikiswa hata mtume na wale walio amini pamaoja naye wakasema: Lini nusura ya Mwenyezi Mungu itakuja? Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu ipo karibu.”[5], na ni lazima wapatwe na fitina na majaribu ili Mwenyezi Mungu awasafishe wale walio amini:
[ألم، أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَ هُمْ لا يُفْتَنُونَ، وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ]
“Alif Lam Mim,Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe? Hakika tuliwajaribu walio kuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo”[6]. Hapo ndipo hali ya muumini hutulia, hata kama atawajihi ugumu na shida, kwani hiyo ndio kanuni ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake, kwamba lazima muumini asimame imara katika matati na athibitishe ukweli na Imani yake, na Mwenyezi Mungu huwalipa wakweli, na atamrahisishia muumini yale yanayo msibu, kwa sababu muumini huwa katika ulinzi wa Mwenyezi Mungu aliye takasika. Mwenyezi Mungu anasema:
[فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا]
“Hakika wewe uko mbele ya macho yetu”[7], na:
،[ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ لاَ يُصِيبُهُمْ ظَمَأٌ وَلاَ نَصَبٌ وَلاَ مَخْمَصَةٌ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَلاَ يَطَؤُونَ مَوْطِئًا يَغِيظُ الْكُفَّارَ وَلاَ يَنَالُونَ مِنْ عَدُوٍّ نَّيْلاً إِلاَّ كُتِبَ لَهُم بِهِ عَمَلٌ صَالِحٌ إِنَّ اللّهَ لاَ يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ]
“Hayo ni kwa sababu hawafikii kiu wala taabu wala njaa katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakanyagi njia iwachukizayo makafiri, wala hawapati taabu yoyote kwa adui, ila huandikiwa kitendo chema. Hakika Mwenyezi Mungu haupotezi malipo ya watendao mema”[8].
Ataona ukubwa wa imani ambayo huujenga moyo na atayaona mafunzo ya juu ambayo inayabeba kwa wanadamu walio potea, wale ambao wanafuata sarabi (mazigazi) na kuishi kwa malengo mabaya, huku wakizitamisha nafsi zao kwa matamanio ya batili yanayo pendezeshwa kwao na wafuasi shetani, kama vile: mali, na vyeo na mambo ya anasa, wakivishindania na kupigana kwa vitu ambavyo havitadumu kwa ajili yao, na badala yake vitakuwa ni mzigo juu yao. Wanajifanyia waungu kasha huanza kuwaabudu na kuwatii na wanawapa mamlaka, basi huwafanyia waungu hao minasaba, na sherehe na makongamano, huwatolea makafara, sio tu ya wanyama bali hata ya binadamu na hutumia kwa waungu hao mabilioni ya fedha.
Kisha ataona kuwa hayupo peke yake kiasi cha kuhisi udhaifu, na udhalili, na kunyenyekea na kusalimu amri. Wala hatahisi kuwa matukio yanayo msibu, na anayo yashudia na kuyaishi ni kirojo na kwamba yeye ni wapekee. Mwenyezi Mungu anasema:
[قُلْ مَا كُنتُ بِدْعاً مِّنْ الرُّسُلِ وَمَا أَدْرِي مَا يُفْعَلُ بِي وَلا بِكُمْ إِنْ أَتَّبِعُ إِلا مَا يُوحَى إِلَيَّ وَمَا أَنَا إِلا نَذِيرٌ مُّبِينٌ]
“Mimi si kiroja miongoni mwa mitume. Wala sijui nitakavyo fanywa wala nyinyi. Mimi sifuati ila yaliyo funuliwa kwangu, wala mimi siye ila ni muonyaji dhahiri”[9]. Hivyo mitume wakubwa na mawalii wema wamekwisha mtangulia kwenye njia hii, hali kadhalika wabeba ujumbe wa Mwenyezi Mungu, na wasuluhishi na waja wema, wote walikabiliwa na haya yanayo mkabili, wakafanya subira kubwa, na wakakabiliwa na jamii zao kwa makubwa kuliko, lakini radiamali yao ilikuwa kama anavyo iakisi Mwenyezi Mungu katika aya hii:
[فَمِنْهُم مُّهْتَدٍ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ]
“Basi wengi wao ni waongofu na wengi wao ni waasi”[10]. Kisha akasema:
[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ لاَ يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إذا اهْتَدَيْتُمْ]
“Enyi mlio amini! Lililo lazima juu yenu ni nafsi zenu. Hawakudhuruni walio potoka ikiwa nyinyi mmeongoka”[11].
Ndani ya Qur’ani ataona namna Mwenyezi Mungu alivyo mtukuza mwanadamu pindi alipo wazungumzisha yeye mwenyewe na akawaelekezea maneno yake moja kwa moja. Mwenyezi Mungu aliye tukuka ndiye muumba wa mbingu na ardhi, mwenye majina mazuri, ndiye anaye upeleka ujumbe kwao na kuwapa ahadi yake. Ni utukuzaji upi ulio bora kuliko huu ambao Mweneyzi Mungu anasema:
[وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَى كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلاً]
“Na hakika tumewatukuza wanadamu na tumewabeba nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku katika vitu vizuri, na tumewatukuza kuliko wengi wa wale tulio waumba, kwa utukufu mkubwa”[12]. Unadhani ni nini zitakuwa hisia za mwanadamu hali ya kuwa akiusoma ujumbe wa mpendwa wake, tena mpendwa asiye na ukomo, “hakika Qura’ni ni agano la Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake, hivyo inafaa kwa kila muumini kuingalia kilichoko ndani ya ahahi hiyo”[13].
Vile vile atakiona kila katika ulimwengu huu ikikiwa kwa kiwango maalumu na hesabu makini, Mwenyezi Mungu: “Kwa hakika sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo”[14], “wala sisi hatukiteremshi isipokuwa kwa kipimo maalumu”[15], “ Nasi tumeweka mizani ya uadilifu”[16], na viumbe vyote kikiwa pekee au kwa makundi hufuata kanuni madhubuti za Mwenyezi Mungu: “nyendo wa wale walio kuwa kabla yenu”[17] na:
[وَمَا مِن دَآبَّةٍ فِي الأَرْضِ وَلاَ طَائِرٍ يَطِيرُ بِجَنَاحَيْهِ إِلاَّ أُمَمٌ أَمْثَالُكُم مَّا فَرَّطْنَا فِي الكِتَابِ مِن شَيْءٍ ثُمَّ إِلَى رَبِّهِمْ يُحْشَرُونَ]
“Na hapana mnyama katika ardhi, wala ndege anaye ruka kwa mbawa zake mbili, ila ni umma kama nyinyi. Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote. Kisha watakusanywa kwa Mola wao Mlezi”[18].
Hivyo, hakuna awezaye kutoka nje ya kanuni hii madhubuti ya Mwenyezi Mungu: “Basi hutapatamabadiliko katika kawaida ya Mwenyezi Mungu, wala hautakuta mageuko katika kawaida (mwendo) ya Mwenyezi Mungu”[19]. Basi ni vipi mwanadamu amwabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu wakati hawezi kutoka mkono wa kawaida na kanuni zake! Hapa si sehemu ya kufanya mchezo wala upuzi: “Ewe Mola wetu mlezi! Hakika hukuviumba hivi bure, utukufu ni wako”[20], “Na sikuumba majini na watu ila wapate kuniabudu”[21], “Kama tungali taka kufanya mchezo, hakika tungeufanya Sisi wenyewe, lau tungeli kuwa ni wafanyao mchezo”[22]. Wala hakuna nafasi ya kusema kwamba vitu vilijitokeza tu bila ya kuwepo aliye vifanya vitokee, jambo ambalo walilishikilia mulhidina (wasio amini uwepo wa Mwenyezi Mungu) dhidi ya kanuni za Mwenyezi Mungu, na wakazicheka kwalo akili za watu kwa muda mrefu, na wakawapotosha wengi, hakaki ameangamia mpotoshaji na mpotoshwaji. Kwani kuumbwa kwa mwanadamu kuna lengo ambalo ndio mwanadamu huyo anapaswa kuishi kwalo na kutumia kipawa na nguvu zake ili kulifanikisha lengo hilo. Na lengo si lingine ila Mwenyezi Mungu aliye tukuka.
Mwenye kuiweka Qur’ani maishani mwake, atakuta ndani yake ahadi ya Mwenyezi Mungu kumsaidia kwa nguvu ya ghaibu katika kila tukio, na katika shida na katika mtengo na vita dhidi ya nafsi yenye kuamrisha maovu au dhidi ya shetani, na atamkuta Mwenyezi Mungu akiwa naye, na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mtetezi wake bora kabisa madaamu atakuwa na naye. Anasema Mwenyezi Mungu:
[إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلائِكَةُ أَلا تَخَافُوا وَلا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ، نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ، نُزُلا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ، وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلاً مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحاً وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ]
“Hakika wale wanosema: Mola wetu mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; na furahieni Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa. Sisi ni walinzi wenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinacho tamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyo vitaka. Ni takrima itokayo kwa Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu. Na ni nani asemaye kauli bora zaidi kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na kufanya vitendo vizuri na akasema: Hakika mimi ni miongoni watii (waislamu)?”[23], na aya ziko nyingi zinazo elezea kuteremkiwa nyoyo za waumini na utulivu, na kushuka msaada wa malaika wenye kushambulia kwa nguvu nk.
Lakini pia mwenye kuishi katika himaya ya Qur’ani atapata utulivu. Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu, nyoyo hutulia”. Atapata poza ya yale yaliyomo katika vifua, na muongozo, na baraka na kila kheri ambayo Qur’ani imejifu nayo.
Hivyo, msomaji wa Qur’ani na mwenye kuiweka maishani mwake, akishayapata yote, azma yake huimarika, na moyo wake hupata nguvu, na nafsi yake husafika, na wakti huo huo hima yake huzidi na hekima yake hudhihirika. Akishafikia hapo, huwa ni chanzo na chemchem ya kheri kwake na kwa jamii nzima kama ilivyo sifa ya wasuluhishi wakubwa, wakiongozwa na bwana mtume (s.a.w.w) na Amirul muuminina (a.s).
[1]. Surat Al-ankabuut: 41.
[2]. Man layhdhuruhu Alfaqiih: 4/410.
[3]. Surat Taha: 66.
[4]. Surat An-Nahli: 26-27.
[5]. Surat Al-Baqarah: 214.
[6]. Surat Al-An’kabut: 1-3.
[7]. Surat Tur: 48.
[8]. Surat Tawba: 120.
[9]. Surat Al-Ah’qaaf: 9.
[10]. Surat Al-Hadid: 26.
[11]. Surat Al-Maidah: 105.
[12]. Surat Al-Isaraa: 70.
[13]. Al-Kafii: 2/609, mlango wa fii qiraatihi, hadithi: 1.
[14]. Surat Al-Qamar: 49.
[15]. Surat Al-Hij’ri: 21.
[16]. Surat Al-Anbiyaa: 47.
[17]. Surat An-Nisaa: 26.
[18]. Surat Al-An’aam: 38.
[19]. Surat Al-Faatir: 43.
[20]. Surat Al-Imraan: 191.
[21]. Surat Adh-Adhariyaat: 56.
[22] . Surat Al-Anbiyaa: 17.
[23]. Surat Fussilat: 30-33.