SABABU ZA KUIPA UMUHIMU QUR’ANI
SABABU ZA KUIPA UMUHIMU QUR’ANI
Hakika sababu nyingi zinatusukuma kuipa Qur’ani umuhimu zimedhihiri. Hapa, Mwenyezi Mungu akipenda nitajaribu kuziorodhesha, pamoja na kuongeza nukta mpya tofauti na ulizo zisikia katika aya za Qur’ani na hadithi kama ifuatavyo:
1. Kuipa umuhimu Qur’ani ni tiba kamili na ya uhakika kwa ajili ya maradhi ya binadamu: maradhi ya kinafsi, kijamii, kiroho bali hata yale ya kimwili pia, kama itakavyo kuja katika baadhi ya hadithi.
2. Mtafuta ukamilifu na furaha yakudumu duniani na akhera– ambalo ndio lengo la juu na mama wa malengo- anahitajia Qur’ani ili kumuongoza kwenye njia sahihi. Na mwanadamu hupanda daraja na kukamilika zaidi kila anavyo nufaika na Qur’ani zaidi.
3. Kuipa umuhimu Qur’ani ni kumfuata mtume (s.a.w.w) na Ahlul-bayt wake watukufu. Na Mwenyezi Mungu ametuamuru hivyo alipo sema:
[لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الآخِرَ وَذَكَرَ اللَّهَ كَثِيراً]
“Hakika nyinyi mnacho kigezo chema kwa mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mugu na siku ya mwisho na akamtaja Mwenyezi Mungu sana”[1].
4. Qur’ani ni barua na ujumbe wa mpendwa asiye na ukomo. Na mwanadamu huwa hachoki kusoma ujumbe wa mpendwa wake, kuuchunguza kwa kina na kutafakari juu ya maana za maneno yake. Mwenyezi Mungu aliyetukuka ndiye mpendwa wa kweli, kwani kila sababu ya kupendwa anayo. Kwa sababu upendo unaweza kusababishwa na ukamilifu na uzuri wa mpendwa, na kwake Mwenyezi Mungu kumejumuika sifa za ukamilifu na majina mazuri. Au sababu ya upendo inaweza kuwa ni fadhila na wema aufanyao mpendwa, na Mwenyezi Mungu ndio mnemeshaji na mwenye kutoa hata kwa wasiostahiki, yeye hutoa hata kwa waja wake waasi:
[وَإِن تَعُدُّواْ نِعْمَةَ اللّهِ لاَ تُحْصُوهَا]
“Na mkizihesabu neema za Mwenyezi Mungu hamwezi kuzidhibiti”[2].
Na maana hii imekuja katika hadithi, iliyopokelewa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s), alisema:
(القرآن عهد الله إلى خلقه فقد ينبغي للمرء المسلم أن ينظر في عهده وان يقرأ منه كل يوم خمسين آية).
“Qur’ani ni ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake, hivyo yafaa kwa muislamu aiangalie ahadi yake na asome kila siku aya hamsini”[3].
5. Kuna thawabu nyingi na malipo makubwa yasiyo na ukomo, anayo pewa msoma Qur’ani na mwenye kutafakari katika aya zake, kama tutakavyo soma katika hadithi tukufu panapo majaliwa.
6. Kwa kuwa Qur’ani ni kitabu hai chenye kudumu kwa ajili ya kila zama na kila sehemu, hivyo mambo iliyo yatolea ufumbuzi, na matatizo iliyo yakabili sio maalumu kwa ajili ya zama fulani. Hivyo, utatuzi tuupatao ndani ya Qur’ani ni utatuzi wa kudumu na endelevu unaofaa kutatua matatizo mapya, na tutataja mifano mingi katika uchunguzi huu. Kama vile: suala la kulinganisha baina ya ujahilia wa kale na ujahilia mpya au ujahilia mambo leo. Ipo hadithi iliyo pokelewa kutoka kwa Harithi Al-a’war, alisema: Niliingia msikitini mara nikawakuta watu wameshughilishwa na mazungumzo (yasiyo husiana na msikiti), nikaenda kwa Imamu Ali (a.s) nikamwambia: Je, huoni kwamba watu wanashughulishwa na mazungumzo msikitini? Wamefanya hivyo? Akauliza Imamu. Nikasema: Ndio. Imamu akasema: Kwa hakika nimemsikia mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akisema: Itatokea fitina, nikamuuliza: Ni ipi njia ya kutoka katika fitina hiyo? Akasema: Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ndani yake kuna habari za waliokuwa kabla yenu na watakuja baada yenu na kuna hukumu za yaliyo baina yenu. Qur’ani ni upambanuo wa haki na batili na ndani yake hakuna mzaha. Dhalimu atakae ipa mgonga Mwenyezi Mungu atamuangamiza, na yeyote atakae tafuta uongofu kwengine Mwenyezi Mungu atampoteza. Yenyewe ni kamba ya Mwenyezi Mungu madhubuti, nayo ni ukumbusho wenye hekima na njia iliyo nyooka...”[4].
7. Tunajifunza maarifa, elimu mbali mbali na siri zilizo hifadhiwa ndani yake. Kiasi kwamba mtu kama Imamu Ali (a.s) ambaye Ibin Abbasi anayejulikana kama kamba ya Umma na mfasiri wa Qur’ani, anasifia elimu kwakusema: “Elimu yangu na elimu ya masahaba wa mtume (s.a.w.w) si chochote ikilinganishwa na elimu ya Ali (a.s) isipokuwa ni kama tone la maji baharini”. Imamu Ali (a.s) na wingi wa elimu yake, alipo ulizwa: Je una elimu yoyote itokanayo na wahyi (ufunuo)? Alisema: Hapana. Ninamuapa ambaye aliye otesha mmea na akaumba mwandamu, hafahamu elimu yoyote itokanayo na wahyi (ufunuo), isipokuwa mja aliye pewa na Mwenyezi Mungu ufahamu wa kitabu chake”[5].
Ndani ya kitabu hiki cha Qur’ani kuna kila mahitaji. Kuna itikadi sahihi, maadili mema, sheria zenye hekima na busara, nukta za kibalagha na mchanganuo mzuri wa mambo. Ndani ya Qur’ani kuna siri za viumbe na maajabu yao. Maajabu yaliyomo katika mwili wa mwandamu, katika ulimwengu na hata katika mazingira. Ndani yake kuna mambo ambayo akili za wafumbuzi haziyafikii. Lakini hii haina maana kwamba Qur’ani ni kitabu cha elimu ya fizikia, au elimu ya kemia, au unajimu wa elimu ya utabibu, hadi ifikie hatua za kasoro zinazo nasibishwa kwenye elimu hizo zihamishiwe kwe Qur’ani. La hasha, Qur’ani ni kitabu cha hidaya na uongofu. Hutumia nyenzo zote ili kulifikia lengo lake. Na elimu zote hizi zinajikita katika lengo hili, na Qur’ani huchukua katika elimu hizi kiwango kinacho hakikisha lengo lake.
8. Kuipa umuhimu Qur’ani ni kujivua dhima kutokana na malalamiko yake pindi itakapo achwa, kama ilivyo tajwa katika hadithi iliyo tangulia huko nyuma: “Vitu vitatu vitamlalamikia Mwenyezi Mungu...”. Bila kusahau kwamba mashtaka ya Qur’ani hayatapingwa mbele ya Mwenyezi Mungu aliye tukuka, kama ilivyo elezea hadithi kwamba: “Qur’ani ni mtoa ripoti anaye kubaliwa”, kwa maana kwamba yenyewe ni mshitaki mkweli na atakae pewa haki. Na hasa ikizingatiwa kuwa shahidi wa malalamiko ya hatakuwa isipokuwa mtume (s.a.w.w), anasema Mwenyezi Mungu:
[وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَذَا الْقُرْآنَ مَهْجُوراً]
“Na mtume atasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wameifanya Qur’ani hii yenye kuhamwa”[6].
9. Kufaulu kwa kupata uombezi na shafaa ya Qur’ani. Hadithi imeisifia Qur’ani kuwa ni “mwombezi mwenye kukubaliwa oumbezi wake”. Hadithi nyingine katika kuelezea uombezi wa Qur’ani inasema:
(وكان القرآن حجيزاً عنه - أي حاجزاً وساتراً عن قارئ القرآن - يوم القيامة، يقول: يا رب إن كل عامل أصاب أجر عمله غير عاملي فبلّغ به أكرم عطائك، قال: فيكسوه الله العزيز الجبار حلتين من حلل الجنة ويوضع على رأسه تاج الكرامة ثم يقال له: هل أرضيناك فيه؟ فيقول القرآن: يا رب قد كنت أرغب له فيما هو أفضل من هذين قال: فيُعطى الأمن بيمينه والخلد بيساره ثم يدخل الجنة فيقال له: اقرأ آية فاصعد درجة ثم يقال له هل بلغنا به وأرضيناك؟ فيقول: نعم).
“Na Qur’ani siku ya Kiyama itakuwa ni kiziwizi chake –yaani kinga na kiziwizi cha msoma Qur’ani-. Itasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika kila aliye tenda jambo atapata malipo ya kazi yake, isipokuwa aliye nifanyia kazi mimi. Mpe malipo yako yaliyo bora zaidi. Mwenyezi Mungu mwenye nguvu na afanyae alitakalo, atamvisha mavazi mawili mazuri katika mavazi ya peponi, na atawekewa taji la utukufu kichwani mwake, kisha Qur’ani itaulizwa: Je tumekuridhisha kwa mtu huyo? Qura’ani itasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nilikuwa nikimtakia kilicho bora zaidi ya hivyo viwili ulivyo mpa. Kisha atapewa amani kuliani kwake na kuishi milele kushotoni kwake, kisha ataingizwa peponi na ataambiwa: Soma aya ya Qur’ani upande daraja. Hapo ndipo Qur’ani itaulizwa: Je tumemfikisha (ulipo pataka afike) na je tumekuridhsha? Ndio. Qur’ani itajibu”[7].
Na kuna faida nyingine nyingi zisizo kuwa hizi. Kama uonavyo baadhi ya faida hizo sio maalumu kwa waislamu tu, ndio maana utaona mwitiko wa wanafikra, wasomi na viongozi mbali mbali wakiielekea Qur’ani na kuchukua ndani yake wakitakacho, hata kama sio waislamu.
Mpaka hapa nadhani sababu nilizo zitaja zinatosha kumwamsha mwanadamu na kumsukuma kuielekea Qur’ani na kuipa umuhimu, stahiki kiasi cha nyama na damu yake kuchanganyikana na Qur’ani. Na mimi hapa, ninamuhimiza[8] kila anaye jua kuwa nina haki juu yake, sawa wasa haki hiyo iwe kisheria au kimaadili, ahitimishe Qur’ani kwa uchache ndani ya mwaka mara mbili. Kiasi hiki ni rahisi sana, hasa ikizingatiwa kuwa ndani ya mwezi wa Ramadhani pekee huwa ikisomwa nusu ya kiasi hiki au zaidi.
Na sababu muhimu zaidi nilizo zitaja ni zile zilizo pokelewa katika hadithi nilizo zichagua kwa ajili yako, kiasi kwamba hadithi hizo zinazidi arobaini, ikiwa ni katika kufuata suna ya wanazuoni wema walio pita ya kutunga vitabu vyenye anwani ya hadithi arobaini kwenye nyanja mbalimbali za elimu na maarifa. Ni matarajio yangu wasomi hao nami nikiwa nao tuwe ni miongini mwa watu walio lengwa na hadithi hii kutoka kwa mtume (s.a.w.w), alisema:
(من حفظ عني من أمتي أربعين حديثاً في أمر دينه يريد به وجه الله عز وجل والدار الآخرة بعثه الله يوم القيامة فقيها عالماً)
“Yeyote katika umma wangu, atakae hifadhi hadithi arobaini katika jambo la dini yake, kwa kitendo hicho akawa anatafuta radhi za Mwenyezi Mungu aliye tukuka, na nyumba ya akhera, Mwenyezi Mungu atamfufua siku ya Kiyama hali ya kuwa ni mwanazuoni msomi”[9].
[1]. Surat Al-Ahzab: 21.
[2]. Surat An-Nahl: 18.
[3]. Al-Kafii: 2/609.
[4]. Sunan Ad-Daarimi: 2/435, kitab fadhailil-qur’an, na mfano wa hadithi hii ipo katika vitabu vya Kishia.
[5]. Hadithi hii imetajwa katika Al-Mizan, jz:3, akinukuu kutoka kwenye baadi ya vyanzo, katika tafsiri ya aya 7-9 ya surat Al-Imran.
[6]. Surat Al-Furqan: 30.
[7]. Al-Kafii: 2/604.
[8]. Muhimizo huu umekuwa na msukumo mkubwa kwa walio wengi katika kuifanyia kazi Qur’ani. Mwenyezi Mungu awalipe malipo bora zaidi ya wafanya mema.
[9]. Al-Khisal: 2/542, mlango wa (Al-arbau’n).