MTUME (s.a.w.w) NA AHLUL-BAYT (a.s) KUIPA UMUHIMU QUR’ANI
MTUME (s.a.w.w) NA AHLUL-BAYT (a.s) KUIPA UMUHIMU QUR’ANI
Hakika umuhimu utolewao na Ahlul-bayt kwa Qur’ani ni wa hali ya juu sana, kiasi kwamba imefikia hadi Imamu Sajadi (a.s) anasema:
(لو مات من بين المشرق والمغرب لما استوحشت بعد أن يكون القرآن معي).
“Lau wangalikufa watu wote waliopo baina ya mashariki na magharibi nisingeli ogopa kuwa mpweke maadamu nina Qur’ani”[1]. Na bwana mtume (a.s.w.w) aliamrishwa na Mwenyezi Mungu kuisoma Qur’ani pale aliposema:
[وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلاً]
“Na soma Qur’ani kwa utaratibu na utungo”[2], vilevile akamuamuru kufanya maandalizi ya kuibeba Qur’ani kwa kusali sala ya usiku bila kuacha, asema MwenyeziMungu:
[إِنَّا سَنُلْقِي عَلَيْكَ قَوْلاً ثَقِيلاً، إِنَّ نَاشِئَةَ اللَّيْلِ هِيَ أَشَدُّ وَطْئاً وَأَقْوَمُ قِيلاً]
“Hakika sisi tutakuteremshia kauli nzito, hakika kuamka usiku kunafiakiana zaidi na moyo, na maneno yake yanatua zaidi”[3]. Kisha bwana mtume (s.a.w.w) hakutosheka na kuisoma Qur’ani tu, bali alikuwa akimtaka Abdullah bin Masoud amsomee Qur’ani, lakini Abdullah akawa anatoa udhuru kwa mtume akisema: “Ewe mjumbe wa Allah! Hakika Qur’ani imeshuka kwako, sasa unataka uisikie kutoka kwangu”. Kisha bwana mtume (s.a.w.w) akawa akisema: “Mimi ninapenda kuisikia kutoka kwako”. Hapo ndipo Abdallah alikuwa akisoma Qur’ani huku macho ya bwana mtume (s.a.w.w) yakibubujikwa na machozi. Akitakata kwa kitendo hicho kuviburudisha viungo vyake vyote kwa Qur’ani: macho yake, masikio yake, moyo wake na ulimi wake, kwakuwa alikuwa akitambua kwamba kila kiungo kina njia yake ya kuhamisha elimu na maarifa. Hivyo licha ya mtume (s.a.w.w) kuwa mbora wa viumbe, lakini alitaka kwa njia hiyo zimkamilikie sababu zote za maarifa. Hata imepokelewa hadithi ambayo maana yake ni kwamba: (mweye kukosa moja ya hisia tano, kwa hakika atakuwa amekosa elimu), ndio maana bwana mtume (s.a.w.w) akawa ananufaika na maarifa ya Qur’ani kwa kutumia viungo vyake vyote. Hali kadhalika imepokewa kuwa ni mustahabu (suna) kusoma Qur’ani kwa sauti inayo sikika, ukiachilia mbali fadhila na thawabu zilizo pokelewa kuhusu kunyamaa pindi isomwapo, na kutazama kwenye msahafu hata kama msomaji amehifadhi kile akisomacho, hata kama ni ndani ya sala, kama itakavyokuja katika orodha ya hadithi hapo baadae inshaa Allah.
Mtume (s.a.w.w) alikua akiathirika kwa Qur’ani. Aliwasomea waislamu surat Ar-Rahman hali ya kuwa wamekaa kimya wakimsikiliza, mtume (s.a.w.w) akawaambia: Niliwasomea majini sura hii lakini wakawa ni wasikivu zaidi yenu. Kivipi ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu? Wakauliza. Akasema (s.a.w.w): Kila nilipo soma:
[فَبِأَيِّ آلاء رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ]
“Basi ni ipi katika neema za Mola wenu mlezi mnayo ikanusha?” walikuwa wakisema: Hakuna chochote katika neema za Mola wetu Mlezi tunacho kikanusha. Na alikuwa akisoma kauli yake Mwenyezi Mungu:
[أَلَيْسَ ذَلِكَ بِقَادِرٍ عَلَى أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَى]
“Je huyo hakuwa ni muweza wa kufufua wafu?”, akisema: Ndio, umetakasika ewe Mwenyezi Mungu. Kwakuwa kupitia aya zile alikuwa akisikia moja kwa moja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na itakuja huko mbele kwamba Imamu Kadhim (a.s) alikuwa akisoma Qur’ani kana kwamba anamhutubia mwanadamu.
Mtume (s.a.w.w) alimsomea surat Az- Zumar kijana mmoja aliyekuwa na moyo safi na nia njema, alipo fika kwenye aya zifuatazo:
[وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَى جَهَنَّمَ زُمَراً]
“Na walio kufuru wataongozwa kuendea Jahannamu kwa makundi”[4] na kauli yake Mwenyezi Mungu:
وقوله تعالى:[وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَراً]
“Na walio mcha Mola wao Mlezi wataongozwa kuendea peponi kwa makundi”[5], alitoa kwikwi kubwa iliyo pelekea kufariki dunia.
Na alisoma surat Al-Insaan wakati imemteremkia akiwa na mtu mmoja mweusi, alipo fika kwenye sifa za pepo, yule mtu alipepesuka mpepesuko ulio sababisha kuiaga dunia, na hapo bwana mtume (s.a.w.w) akasema: Kilichoitoa nafsi ya ndugu yenu ni shauku ya pepo. Hawa ndio wale ambao aya hii tukufu iliwasifu kwa kwa kauli yake Allah (s.w.t):
[الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلاَوَتِهِ أُوْلَئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ وَمن يَكْفُرْ بِهِ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ]
“Wale tulio wapa kitabu wakakisoma kama ipasavyo kusomwa, hao ndio kweli wanao kiamini. Na wanao kikataa, basi hao ndio wenye kukhasirika”[6].
[1]. Al-Kafii: 2/602.
[2]. Suurat Al-Muzzammil: 4.
[3]. Suurat Al-Muzzammil: 5-6.
[4]. Surat Az-Zumar: 71.
[5]. Surat Az-Zumar: 73.
[6]. Surat Al-Baqarah: 121.