KUWAACHA AHLUL-BAYT (A.S) NI KUTOSHIKAMANA NA QUR’ANI
KUWAACHA AHLUL-BAYT (A.S) NI KUTOSHIKAMANA NA QUR’ANI
Kwa bahati mbaya umma wa kiislamu ulikiacha kitabu cha Mwenyezi Mungu na ukajitenga nacho mbali pale ulipowaengua Ahlul-bayt kwenye nafasi yao ambayo Mwenyezi Mungu aliwachagulia, kwa kuwa ni jambo lisilowezekana kuvitenganisha viwili hivyo. Ambapo, kwa kuwaondoa Ahlul-bayt kwenye nafasi yao, waliacha na kuipinga kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
[وَرَبُّكَ يَخْلُقُ مَا يَشَاء وَيَخْتَارُ مَا كَانَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ]
"Na Mola wako Mlezi huumba na huteuwa atakavyo. Viumbe hawana khiari"[1].
Kama ni kauli mbovu, ushawishi wa shetani na matamanio mabaya yatokanayo na nafsi inayo amrisha uovu maneno ya anayesema: "Kinatutosha kitabu cha Mwenyezi Mungu", maneno ambayo bado yanakaririwa na kupitishwa na shetani kwenye ulimi wa kila anayetaka kubomoa Uislamu, kuanzia kwenye misingi na mihimili yake, Qur’ani ikiwa ni moja ya misingi hiyo, kwa madai eti Qur’ani hiyo inamtosha, wakati anatambua wazi kabisa kwamba, Qur’ani haiwezi kutekeleza jukumu lake la hidaya la (uongofu) isipokuwa itakaposimimwa na msimamizi wenye ufahamu wa hukumu na mafunzo yake, msimamizi ambaye si mwingine isipokuwa Ahlul-bayt na kizazi kitakatifu cha bwana mtume (s.a.w.w).
Ukweli ni kuwa fitina hii ya kutenganisha Qur’ani na msemaji wake (msimamizi wake) ina historia ndefu, na Amiirul muumina Ali (a.s) ni miongoni mwa waliopatwa na fitina hii, pale alipolazimishwa usuluhishi na Muawiya na Qur’ani kufanywa ndio hakimu baina yao, hapo ndipo Amiirul muumina (a.s) aliposema:
(هذا القرآن إنما هو خط مستور بين الدفتين لا ينطق بلسان ولا بد له من ترجمان وإنما ينطق عنه الرجال)
“Hakika Qur’ani hii ni maandishi yaliyo andikwa kwenye karatasi, haiongei kwa ulimi na inahitaji wakuifasiri na wanaoitafsiri ni watu waliyo ifahamu”[2].
Hivyo, Qur’ani na Ahlul-bayt (a.s) ni mihimili miwili isiyo achana wala kutengana, na haiwezekani kudai eti nimeshikamana na kimoja hali yakuwa kingine umekitelekeza. Hakika Ahlul-bayt ndio ule mlango wa Mwenyezi Mungu ambao haiwezekani kuingia kwake isipokuwa kupitia mlango huo, na Mwenyezi Mungu ametuamuru tusiingie kwenye majumba isipokuwa kwa kupitia kwenye milango yake.
Kwa minajili hiyo, madai ya wapinzani wetu kuwa wao ndio wenye kuipa umuhimu Qur’ani zaidi yetu, ni madai batili na yasio na msingi kabisa. Ni kweli kwamba wao wamejishulisha na utamkaji wa herufi zake, kuipendezesha sauti kiasi hadi ikafikia kama wanaimba waisomapo, na kuhifadhi kanuni na hukumu za tajuwidi walizoweka wenyewe, ambapo baadhi ya kanuni hizo hupingana na hukumu ya dini, lakini kutilia umuhimu vyote hivyo ni marembo tu, jambo la muhimu zaidi ni kufahamu na kuelewa malengo na madhumuni ya Qur’ani na kuyafanyia kazi, kwa sababu neno ni vazi la maana na maana ndio kiini cha lengo, na msemaji huwa haliangalii neno kama lenyewe, bali kuliangalia kama chombo cha kubebea maana na zana ya kufikishia maana ile kwa hadhira, hivyo maana ndio lengo na kusudio halisi la msemaji.
Zimepokewa hadithi nyingi zikiwalaumu wenye kung'ang'ania matamshi ya Qur’ani na herufi zake hali ya kuwa wanapoteza maana na hukumu zake. Imekuja katika hadithi maarufu kwamba:
(كم من قارئ للقرآن والقرآن يلعنه)
"Ni wasomaji wangapi Qur’ani wanaoisoma huku ikiwalaani!",[3]
Wakati huyo msomaji huwa ni mpinzani wa Qur’ani, kwa sababu hatendi kwa mujibu wa mafundisho yake. Na hadithi nyingine kutoka kwa Abu Ja'fari alisema:
(قرّاء القرآن ثلاثة: رجل قرأ القرآن فاتخذه بضاعة واستدر به الملوك واستطال به على الناس فذاك من أهل النار، ورجل قرأ القرآن فحفظ حروفه وضيع حدوده فذاك من أهل النار، ورجل قرأ القرآن فوضع دواء القرآن على داء قلبه فأسهر به ليله وأظمأ به نهاره وقام به في مساجده وتجافى به عن فرشه فبأولئك يدفع الله العزيز الجبار البلاء، وبأولئك يديل الله من الأعداء-أي ينصرهم على الأعداء- وبأولئك ينزل الله الغيث من السماء فوالله هؤلاء قراء القرآن أعز من الكبريت الأحمر)[4].
“Wasomaji wa Qur’ani wako makundi matatu:
1. Ni wale wanao soma Qur’ani na kuifanya ni mtaji wao, na kupokea ajira kutoka kwa wafalme (watawala) na wanajikweza kwa watu, hawa ni watu wa motoni.
2. Ni wale watu wanao soma Qur’ani wakahifadhi herufi zake na kupoteza hukumu zake, hawa nao ni watu wa motoni, na
3. Wengine ni wale wanao soma Qur’ani, wakaifanya Qur’ani kuwa dawa ya maradhi ya mioyo yao, wakasimama usiku kusali kupitia Qur’ani, na wakafunga na kuvumilia kiu ya mchana kupitia Qur’ani, wakasimamisha sala misikini kupitia Qur’ani na wakaachana na magodoro yao kupitia Qur’ani. Mwenyezi Mungu kwa sababu ya watu hawa huondoa mabalaa, hutoa ushindi dhidi ya maadui na hushusha mvua. Ninamuapa Mwenyezi Mungu kwamba wasomaji hawa ni adimu kupatikana kuliko kibiriti chekundu”.
Imekuja katika hadithi yingine kutoka kwa Imamu Hassan (a.s) kwamba:
(وإن أحق الناس بالقرآن من عمل به وإن لم يحفظه وأبعدهم منه من لم يعمل به وإن كان يقرأه)
“Na hakika watu walio karibu zaidi na Qur’ani, ni wale wanaifanyia kazi hata kama hawakuihifadhi (aya zake), walioko mbali zaidi na Qur’ani, ni wale wasio tenda kwa mujibu wa Qur’ani hata kama wanaisoma”.[5]
Hivyo, inadhihiri wazi kabisa kwa mkakati wa kutenganisha Qur’ani na Ahlul-bayt (a.s) ili kwa njia hiyo kuikosesha Qur’ani malengo na madhumuni yake na kufanya ushawishi wa kuyapa umuhimu maneno yake tu ni mkakati wenye muda mrefu, na maimamu walio takasika (a.s) walitabahisha wafuasi wao juu ya jambo hilo. Ni umuhimu upi huo inaopewa Qur’ani pale isomwapo kauli yake Mwenyezi Mungu:
[وَرَبُّكَ يَخْلُقُ مَا يَشَاء وَيَخْتَارُ مَا كَانَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ]
“Na Mola wako Mlezi huumba na huteuwa atakavyo. Viumbe hawana khiari”[6].
Kisha wakaachwa walioteuliwa na Mwenyezi Mungu, na kutangulizwa wasiokuwa wao? ili hali Mwenyezi Mungu kaupa uteuzi wao hadhi sawa na risala nzima ya Uislamu, pale aliposema:
[يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ واللهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ]
“Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu.[7]”
Ni umuhimu upi huo wanaoipa Qur’ani pale inapopaza sauti ikisema:
[قُل لا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْراً إِلا الْمَوَدَّةَ فِي الْقُرْبَى]
“Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi kwa jamaa zangu wa karibu (Ahlul-bayt wangu)”[8],
ili hali wakifanya uadui kwa watu wa nyumba ya mtume (s.a.w.w), na kuwafuatilia kwa ubaya kila mahali? Laiti wangelikuwa wakiipa umuhmu Qur’ani, wangeliweka aya hiyo pamoja na hii:
[قُلْ مَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِلا مَن شَاء أَن يَتَّخِذَ إِلَى رَبِّهِ سَبِيلاً]
“Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi”[9],
ili wapate ukweli kwamba Ahlul-bayt (a.s), ndio ile njia ambayo Mwenyezi Mungu aliamrisha ifuatwe, ni pale aliposema:
[وَأَنَّ هَذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيماً فَاتَّبِعُوهُ وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ]
“Na kwa hakika hii ndiyo njia yangu Iliyo nyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na njia yake. Haya amekuusieni ili mpate kumcha Mungu.”[10], na hivyo Imamu Baqir (a.s) alivyoifasiri aya hiyo, akasema:
(نحن السبيل فمن أبى هذه السبل فقد كفر).
“Sisi ni njia, na yeyote mwenye kupinga njia hizi, atakuwa amekufuru.[11]”
Maneno yasemayo: “Kinatutosha kibatu cha Mwenyezi Mungu” na wapambe wa maneno hayo ambao wamekuwa wakiyakariri hadi leo hii na kuhitaji dalili ya kila kitu kutoka ndani ya Qur’ani tu, sisemi wala kuyaita kuwa ni maneno ya haki yenye malengo ya batili (kama wasemavyo wengine), bali hayo ni maneno ya batili yaliyolenga batili. Na wafuasi wa maneno hayo hawataki kingine zaidi ya kubomoa, na kuvunja misingi ya Uislamu kwa madai kuwa Qur’ani inajitosheleza. Kwani madai hayo maaa yake kutokuwa na haja hata ya mtume (s.a.w.w)! ambako kuna manisha kubaki na ujinga wa ufafanuzi wote wa sheria ya Uislamu, kwa sababu mtume (s.a.w.w) na maimamu (a.s) ndio wasimizi wa Qur’ani, wasemaji na wenye kufafanua hukumu zake.
Leo hii angalia elimu zilizo enea ulimweguni, je unaweza ukawa dakitari au muhandisi bila kujifunza kwa wataalamu na wajuzi wa elimu za udakitari na uhandisi? Ikiwa hilo haliwezekani, inakuwaje kupata ujuzi wa Qur’ani? Kitabu ambacho: “kinabainisha kila kitu”[12] na “hakikupuuza wala kuacha chochote”[13] na kuna masilahi ya wanadamu wote katika kila zama: “Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi?”. Ndio maana bwana mtume Mohammad (s.a.w.w) akautahadharisha umma wake juu ya hatari hii akisema:
(لا ألفين أحدكم متكئاً على أريكته يأتيه الأمر من أمري مما أمرت به أو نهيت عنه فيقول: لا ندري ما وجدنا في كتاب الله اتبعناه)
“Nisimuone mmoja wenu hali ya kuwa ameegamia kwenye kochi lake, akajiwa na amri miongoni mwa amri nilizo amrisha au katazo nililokatazwa kisha akasema: sijui! Kwa hoja kwamba, sisi tunakubali na kufuata tulichokipata ndani ya Qur’ani.[14]”
Isipokuwa maadui wa Mwenyezi Mungu na wafuasi wa shetani, walitambua wazi kuwa Qur’ani ndio ngome yenye kuulinda umma huu wa Kiisamu kutokana na upotovu, na kwamba Ahlul-bayt (a.s) ndio wasimamizi wa Qur’ani. Na hapo ndipo walipoandaa mkakati wa kuwaweka mbali Ahul-bayt na umma ili ubaki bila mlinzi, na Qur’ani ibaki bila msimamizi, kwa njia hiyo umma ukawa ni windo rahisi kwa maadui wake na kwa wale wanaoutakia mabaya. Bila shaka mwenyewe unauona umma huo ulikofikia, umekuwa ukitikiswa na shub’ha ndogo, ukifeli katika kila fitina na kuanguka mwanzoni mwa kila jaribio. Kuwaacha Ahlul-bayt (s.a) ni pigo kubwa lililo ukumba mfumo wa Uislamu, na kusababisha elimu ya Qur’ani na namna ya tafakuri sahihi iliyokuwa ikilinganiwa na Qur’ani kusahaulika na kuachwa. Ushahidi wa hilo upo wazi kabisa, kwani inatosha kulitambua hilo kwa kuangalia uchache wa hadithi zilizo nukuliwa katika vitabu vya hadithi kutoka kwa Ahlul-bayt (a.s), na hasa ukizinagatia hadhi na heshima ya elimu ya hadithi iliyokuwa katika kipinda cha makhalifa, na shauku kubwa ya waliyokuwa nayo katika kupokea hadithi. Unaweza kustaajabu sana pindi unapo hesabu hadithi zilizo pokelewa katika zama hizo kutoka Imamu Ali (a.s), Imamu Hassan (a.s) na Imamu Hussein (a.s) katika uga wa tafsiri ya Qur’ani! Kwa mfano: hauwezi kukuta swahaba alinukuu hadithi kutoka kwa Imamu Ali (a.s)! Ama hadithi zinazohusu Qur’ani walizo nukuu walio kuja baada ya maswahaba (matabiina) kutoka kwake (a.s) zikihesabiwa hazizidi hadithi mia moja, wakati zilizo pokelewa kutoka kwa Imamu Hassan (a.s) hazifiki hata kumi, ama kutoka kwa Imamu Hussein (a.s) hakujapokelewa hadithi yoyote ile! Hivi ndivyo hali ilivyo kwa Ahlul-bayt (a.s), wakati Suyuti katika kitabu chake cha Al-Itqan ametaja kwamba jumla ya hadithi zilipokelewa kuhusu tafsiri ya Qur’ani zinafikia elfu kumi na saba. Hii ni idadi inayotajwa kupitia njia za jamhuri ya wanahadithi peke yao, na ukija kwenye fikihi utakuta hali ni kama hiyo hiyo pia”[15].
Unadhani ipi ilikuwa ni hasara ya Qur’ani baada ya kuwaweka mbali Ahlul-bayt (a.s) na nafasi yao aliyo wachagulia Mwenyezi Mungu? Angalia hasara hizi katika yafuatayo:
1. Kufichikana elimu nyingi za Qur’ani ambazo hawazifahamu isipokuwa Ahlul-bayt (a.s).
2. Qur’ani kushidwa kutekeleza jukumu lake katika kujenga nafsi na jamii, kwakuwa Qur’ani na Ahlul-bayt (a.s) ni mihili miwili isiyo tengana, hivyo Qur’ani haiwezi kuathiri maisha ya umma wa Kiislamu ispokuwa iwapo mikononi mwa Ahlul-bayt.
3. Qur’ani kuwa windo la maadui, watu wenye tamaa na wenye malengo binafsi. Utawaona kila mmoja akitumia Qur’ani kuthibitisha imani ya madai yake, hata makhawariji nao walikuwa wakitumia Qur’ani katika majadiliano yao na Ibin Abbasi ili kuthibitisha batili yao baada ya tukio la usuluhisho, ndipo Imamu Ali (a.s) alipo mkataza kuhojiana nao kwa kutumia Qur’ani; kwa kuwa ina maana zaidi ya moja[16], hatimaye maana halisi za Qur’ani zikapotea kwa sababu ya tafsiri ambazo Qur’ani imetahadharisha kuzifuata kwa kusema:
[فَأَمَّا الَّذِينَ في قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاء الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاء تَأْوِيلِهِ]
“Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake…”, lakini jawabu limetolewa na Qur’ani yeynyewe iliposema:
[وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلاَّ اللهُ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ]
“Na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu”[17]. Ahlul-bayt (a.s) ni mfano ulio wazo wa wenye elimu madhubuti.
4. Umma wa Kiislamu kusambaratika na kufarakana, kwa sababu uhifadhi na msingi wa kuuangana kwake ni Qur’ani na Ahlul-bayt (a.s) kwa mujibu wa bwana mtume (s.a.w.w) alivyoitafsiri kauli yake Mwenyezi Mungu:
[وَاعْتَصِمُواْ بِحَبْلِ اللّهِ جَمِيعاً وَلاَ تَفَرَّقُواْ]
“Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu kwa pamoja na wala msifarakane”, Alisema (s.a.w.w) kuwa: kamba hiyo ni Qur’ani na Ahlul-bayt.
Bibi Fatima Zahraa (a.s) naye pia amewazungumzia Ahlul-bayt katika hotuba yake aliyo itoa katika msikiti wa Mtume (s.a.w.w) pale Madina Munawara akisema:
(وجعل إمامتنا نظاما للملة)
“Mwenyezi Mungu kaufanya uongozi wetu kuwa ndio mfumo wa dini”[18], kwa maana kwamba kupitia Ahlul-bayt mambo ya waislamu hunyooka na huimarika. Ndio maana matokeo ya jamii ya Kiislamu kuwaweka kando Ahluli-bayt ilimekuwa kuangukia mikononi mwa watawala waovu na watumwa wa matamanio ya nafsi zao, ambao waliitumia Qur’ani hii hii kuteketeza mimea na viumbe, ambapo huambatanishwa nao kila aliyewapigia debe na kutetea vitendo vyao viovu, kama wale walio tumia kauli ya Mwenyezi Mungu:
[أَطِيعُواْ اللهَ وَأَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَأُوْلِي الأَمْرِ مِنكُمْ]
“Mtiini Mwenyezi Mungu na mumtii Mtume na wenye madaraka katika nyinyi”, kuwafanya hao watawala makafiri na wapotovu, kuwa ndio wenye madaraka na wenye kuwatawala waislamu.
[1]. Suuratul Qasas: 68.
[2]. Nahajul Balaghah, hotuba:125.
[3]. Mustadekul Wasail: ketabu salah, ab’wabu qiraatul qur’an, mlango:7, hadithi:7.
[4]. Alkhswaar:142.
[5]. Irshadul quloob:79.
[6]. Suratul Qasas: 68.
[7]. Surat Al-Maidah: 67.
[8]. Surat Ash-Shura: 23.
[9]. Surat Al-Furqaan: 57.
[10]. Surat Al-An’aam: 153.
[11]. Behaarul Anwaar: 13/24, mlango: Maimamu ndio njia, wao na wafuasi wao.
[12] . Suurat An Nah’l:89.
[13]. Suurat Al-An-a’am:38.
[14]. Al-Mizan fii tafsiril-qur’an: jz: 3, katika bahathi ya riwaya katika aya: 28-32, suurat Al-Imran, akinukuu kutoka kwa: Ahmad, Abuu Daud, Tirmidhii, Ibin Majah, Ibin Habban na wengineo mimongoni wa wanazuoni wa kisuni.
[15]. Al-Mizan fii tafsiril-quran: jz: 5, katiba bahathi ya taarikh, chini ya aya: 15-19 katika suurat Al-Maida.
[16] . Behar Al-Anwaar: 2/245.
[17]. Suurat Al-Imran: 7.
[18]. Kashful Ghummah: 2/110.