“….Wasimamisheni, kwani hao ni wenye kuulizwa….”

| |times read : 42
“….Wasimamisheni, kwani hao ni wenye kuulizwa….”
  • Post on Facebook
  • Share on WhatsApp
  • Share on Telegram
  • Twitter
  • Tumblr
  • Share on Pinterest
  • Share on Instagram
  • pdf
  • Print version
  • save

 “….Wasimamisheni, kwani hao ni wenye kuulizwa….”

(Surat Swaffat aya 24)

Sifa na alama za Kiongozi (Mwenye kuulizwa)

Imepokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saww) akisema:

“....Kila mmoja wenu ni kiongozi na mwenye kuulizwa juu ya raia wake, mtawala ambaye yupo juu wa watu ni kiongozi na mwenye kuulizwa juu ya raia wake, na Mwanaume ni kiongozi na pia mwenye kuulizwa juu ya watu wa nyumba yake, na mwanamke pia ni kiongozi na mwenye kuulizwa juu ya nyumba na familia ya mume wake....”[1]

Kama ambavyo pia imepokelewa kutoka kwa Imamu (as) akisema:

“...Mcheni Mwenyezi Mungu kupitia waja na miji yake, kwani mtakuja kuulizwa hata kunako wanyama, hivyo basi mcheni Mwenyezi Mungu na wala msimuasi katika hayo...”[2]

Kwa minajili hii sote sisi tuna majukumu na ni wenye kuulizwa, japokuwa upana na ufinyu wa majukumu haya unaweza kutofautiana, pamoja na kwamba si jambo la kujificha kwamba kila mmoja ni mwenye kuulizwa kuhusu yeye mwenyewe na nafsi yake kwanza, katika swala la kuipa mafunzo sahihi na kuitengeneza. Kisha ni mwenye kuulizwa juu ya familia yake, rafiki zake, jamaa zake wa kazini, jirani zake, jamii yake ikiwa atakuwa ni katika nafasi ya kiongozi wa kisiasa au kidini. Na hivi ndivyo inavyokuwa mpaka inafikia katika nyanja na nafasi za juu kabisa katika kuwachunga watu na kusimamia mambo yao.

Na katika riwaya zimetajwa baadhi ya sifa na mambo ambayo ili kiongozi aweze kufaulu katika majukumu yake, ni lazima aweze kushikamana na kupambika nayo, na pia ili aweze kuonekana ni mwema mbele ya Mwenyezi Mungu (swt) na apate radhi zake pia, na katika riwaya zote hizo nimeona kwamba sifa ya “Ubaba” imepewa kipaumbele mno. Na hii sifa iwe katika anuani yeyote ile kwa nafasi yeyote ile, kwa maana hata Mtume Muhammad (saww) tunakuta anatumia anuani hii kwa ajili yake na ndugu yake Imamu Ally (as) kwa kusema:

“...Mimi na Ally bin Abi Talib ni baba wa Umma huu...”[3]

Na labda niwaambie kwa uwazi kabisa kwamba sifa pekee ambayo wanaikosa  watu wenye kutawala mambo ya watu yawe makubwa au madogo ni sifa hii, na kumiliki au kuikosa sifa hii ni sababu kubwa mno katika kufaulu au kufeli kwa taasisi zetu kubwa, na si tu taasisi za kiserikali, bali hata binafsi na za kujitolea bali hata za dini na tamaduni. Sheikh Kulainiy anapokea kutoka kwa Imamu Baqir (as) kwamba amesema:

“....Mtume Muhammad (saww) amesema “..Uongozi hautakuwa bora mpaka mwenye kusimamia atakapokuwa na mambo matatu, Uchamungu ambao utamzuia kunako kumuasi Mwenyezi Mungu, Upole ambao kwao atazuia hasira zake, na mwenendo mzuri kwa wenye kuwatawala kwa kiasi awe kwao ni kama mzazi mwenye huruma...”[4]

Na katika kitabu hicho hicho pia kumepokelwa kwamba siku moja Imamu Ally (as) aliletewa tini na asali kutoka mji wa Hamadan, akaamrisha waliokuwepo kwamba wamtafutie mayatima, wakafanikiwa kuwakuta katika vichochoro na kisha Imamu akaanza kuwalambisha asali mayatima wale. Waliokuwepo wakamuuliza, ewe Imamu kwanini unawalambisha tena?, Imamu akajibu kwa kusema “...Hakika kiongozi ni baba wa mayatima, na nimewarambisha  hivi kwa anuani ya baba zao..”[5]

Sasa la muhimu hapa ni zipi hizo sifa za mzazi mwenye huruma ambazo riwaya zinataka watu wajipambe nazo?. Kwanza kabisa tuzingatie nukta hizi kabla ya kutaja sifa hizo:

1.   Tuzipambe nafsi zetu kwa sifa hizo, kwa sababu ni daraja za kitabia ambazo hupelekea mtu kuonekana bora kwa Mwenyezi Mungu (swt). Na hili ni jambo la muhimu sana ambalo watu wengi wanalisahau, na kushindwa kutambua kwamba hii ndio bora kabisa ya kuweza kumfikia Mwenyezi Mungu.

Imepokelewa kutoka kwa Mtume (saww) kwamba amesema:

“....Kwa hakika mja anaweza kufikia daraja ya juu kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa tabia nzuri yake, hata kama mbele za watu ataonekana ni mja dhaifu....”.[6]

Pia imepokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq (as) akisema:

“...Hakuna jambo pendwa zaidi ambalo muumini anaweza kulitanguliza kwa Mwenyezi Mungu baada ya faradhi zake kuliko kuwavuta watu kwa tabia njema zake...”.[7]

2.   Tutambue kwamba sisi ni wenye kuhesabiwa kunako hayo, kama ambavyo aya za Quran zinasema “...na wasimamishwe hao kwani ni wenye kuulizwa...” (Surat Safat aya 24).

“..Na kwa haki ya Mola wako, hakika tutawauliza wote, kuhusu waliyokuwa wakiyafanya...” (Surat Hijr aya 92-93)

3.   Lazima tuchukue mafunzo sahihi namna ya kuwalea watoto wetu kwa mujibu wa mafunzo ya watu wa nyumba ya Mtume Muhammad (saww), na pia tutambue kwamba kuna baadhi ya sifa tunaweza kuzipata kwa anuani ya kwamba sisi ni baba wa familia, ila tukiangalia riwaya zilizopita ikawa kwamba zinataka kila mwenye kuchukua majukumu ya kutawala mambo ya watu ajipambe na sifa za mzazi mwenye huruma. Hivyo tuchukue sifa hizi na kisha kuzitumia hata katika majukumu mengine pia.

Na sifa zenyewe ni:

1.   Mapenzi kwa wote, Mtoto kwa ngazi ya familia, au jamii kwa ngazi ya majukumu ya kijamii.

Imepokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq (as) akisema:

“...Siku moja Mussa bin Imran alisema “..Ewe Mola wangu, ni jambo gani hasa unalipenda?. Mwenyezi Mungu (swt) akamjibu, Ni kupenda watoto, kwa maana mimi nimewaumba katika maumbile ya kunipwekesha mimi, na hata nikiwafisha kwa mapenzi na huruma yangu nawaingiza katika pepo yangu....”.[8]

Pia imepokelwa kutoka kwa Mtume Muhammad (saww) kwamba amesema:

“..Pendeni watoto na waoneeni huruma..”[9]

“..Mtazamo wa mapenzi wa mzazi kwa mtoto wake ni ibada..”[10]

Pia imepokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq (as) akisema:

“...Hakika Mwenyezi Mungu anaweza kumuonea huruma mja wake kutokana tu kumpenda kwake mtoto wake...”[11]

Jambo la muhimu hapa ni kwamba mapenzi yanatakiwa kukusanya watu waote, kwani wote ni katika athari za uumbaji wa Mwenyezi Mungu na uwezo wake, na mwenye kumpenda Mungu bila shaka atapenda athari na kila chenye kuambatana na Mungu huyo.

2.   Upole:

Mwenyezi Mungu anasema:

“..Kwa rehma za Mwenyezi Mungu umekuwa mpole kwao, kwa maana kama ungalikuwa mkali na mwenye moyo mgumu basi hao wa pembeni wangalikukimbia...”

Surat Al Imran aya 159.

Pia imekuja katika barua ya Imamu Ally (as) akimtumia Malik Al Ashtar baada ya kumtawalisha Misri:

“...Onyesha hurma yako kwa raia wako, na mapenzi yako kwao, na kuwaonea kwako huruma, na wala usiwe kwao kama mnyama mkali mwenye kuwatumia kama chakula chao. Kwa maana raia wako utawakuta katika pande kuu mbili, ima atakuwa ni ndugu yako katika imani, au atakuwa ni mwenzako kimaumbile....”[12]

Na katika nukta hii ya kuzungumzia mapenzi baina ya baba na mwana, imepokelwa kutoka kwa Mtume Muhammad (saww) akisema:

“..Pendeni mno watoto na waoneeni sana huruma..”[13]

Miongoni mwa alama za mapenzi na kuwapenda watoto ni pamoja na kuwabusu, kuwafurahisha, kuwaridhisha, kuingiza raha na furaha katika nyoyo zao, kuwapapasa vichwa vyao, kuwaangalia kwa huruma na mapenzi na mengineyo.

Imepokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saww):

“...Mwenye kumbusu mtoto wake Mwenyezi Mungu humuandikia jema, na mwenye kumfurahisha basi Mwenyezi Mungu atamfurahisha siku ya kiyama, na mwenye kumfunza Quran basi siku ya kiyama atavalishwa vazi lenye nuru ambayo watu wa peponi watanawiri kwayo nyuso zao...”[14]

“...Busuni watoto wenu, kwani kwa kila busu mna daraja peponi, na baina ya kila daraja ni utofauti wa miaka mia tano...”[15]

Alipoonekana siku moja akwabusu Hassan na Hussein, Aqrai Bin Habis akasema “...Mimi nina watoto kumi, na hata siku moja sijawahi kumbusu mmoja wao..”. Mtume (saww) akasema “..Sitahusika  endapo Mwenyezi Mungu ataamua kukuondolea huruma yake...”[16]

Na siku moja pia Mtume alikuwa akiwabusu Hassan na Hussein, Aiyanah akasema “..Mimi nina watoto kumi, na sijawahi busu hata mmoja...”  Mtume akamjibu “...Hatoonewa huruma ambaye haonei huruma wengine...”[17]

Imepokelewa kutoka kwa Imamu Kadhim ambaye amepokea kutoka kwa Baba na babu zake mpaka kutoka kwa Mtume Muhammad (saww)

“...Mzazi akimtazama mwanawe na akamfurahisha, mzazi huyo anakuwa na malipo ya kuacha huru mtumwa mmoja..”. akaulizwa Mtume je, ikiwa atamuangaia mara mia tatu na sitini (nyingi)?, Mtume akajibu kwa kusema “Allahu Akbar” (Mungu ni Mkubwa).[18]

Pia imepokelewa kwamba Mtukufu Mtume Muhammad (saww) alikuwa kila akiamka basi huwa na kawaida ya kuwapapasa vichwa watoto na wajukuu wake.

Imamu Ally (as) anasema :

“...Busu la mzazi ni huruma na upendo...”[19]

Siku moja Mtume Muhammad alimtembelea Othman bin Madh Un ambaye alikuwa na mtoto mdogo wakati huo, akamkuta akiwa katika hali ya kubusu mtoto yule. Mtume akamuuliza,

Je huyu ni mwanao na unampenda?. Othman akajibu kwa kusema ndio ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume akamwambia, Je, nikuongezee jambo ambalo litakufanya umpende zaidi?. Othman akasema “..Baba na mama yangu wawe fidia kwako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, naam niongezee..”. Mtume akaanza kusema “...Kwa hakika mwenye kumridhisha mtoto wake mpaka akaridhika, Mwenyezi Mungu siku ya kiyama atamridhisha mpaka na yeye aridhike...”[20]

3.   Kusamehe: kwa maana ya kufumbia macho baadhi ya atendayo. Kwa kiasi kwamba kama vile huna habari nini amefanya, iwe kosa au lolote, lakini wakati huohuo unakuwa unafuatilia mambo ambayo huenda huwa anafanya akiwa peke yake.

Na maana hii tunaikuta katika baadhi ya riwaya za Maasumina (as), mfano imepokelewa kutoka kwa Imamu Ally amesema:

“....Nusu ya akili ni shaka, na nusu nyingine ni kufumbia macho...”[21]

Pia amesema:

“...Baadhi ya hali za watu wakarimu ni kufumbia macho mambo ambayo wanayajua....”[22]

Pia imepokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq (as) kwamba amesema:

“...Hakika theluthi mbili ya maisha na kuamiliana na watu inapatikana katika utambuzi wa mambo, na theluthi inayobakia inapatikana katika kufumbia macho mambo....”[23]

Pia imepokelewa kutoka kwa Imamu Ally bin Hussein  Sajjad (as):

“...na tambua ewe mwanangu kwamba usalama wa dunia unapatikana katika maneno mawili, Theluthi mbili za usalama wa maisha ni katika utambuzi wa mambo, na theluti moja yake ni katika kufumbia macho mambo, kwa sababu mwanadamu hafumbii macho isipokuwa jambo ambalo amelifahamu na kulitambua undani wake....”[24]

4.   Kuwaliwaza, kuwa mlaini na kuwahurumia. Jambo ambalo ni katika adabu za kuishi na kuamiliana na watu. Mtume Muhammad anasema “....Mwenyezi Mungu ameniamrisha kuwa mlaini kwa watu, kama ambavyo ameniamrisha kufanya faradhi...”[25] Pia anasema “....Kuwa mlaini kwa watu ni nusu ya imani, na kuwa nao pamoja ni nusu ya maisha....”[26]

Pia imepokelwa kutoka kwake akisema

“....Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni mpole na anapenda upole, na humpa mpole mambo ambayo hampi mwenye kutenza nguvu...”[27]

Kwa maana hiyo upole ni katika sifa za Mwenyezi Mungu, na ni katika kumpwekesha Mwenyezi Mungu kimatendo endapo mja atajisifu na sifa za Mwenyezi Mungu (swt), na kuachana kabisa na sifa za ukali katika matendo na maneno, sawa sawa iwe kuna utovu wa nidhamu umetoka kwao au la.

Kuna riwaya zimepokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saww) akisema:

“..Chukueni machache kutoka kwa watu na yakubalini, wala msiwachoshe...”[28]

“...Hakika Mwenyezi Mungu anapenda upole, na husaidia watu kuufikia..”

“...Kama upole ingekuwa ni katika viumbe, basi kusingekuwa na kiumbe bora kuliko yeye...”[29]

“...Hakika katika upole kuna baraka zenye kuongezeka, na mwenye kunyimwa upole basi anakuwa amenyimwa kheri nyingi...”[30]

“...Mwenye kuwa na upole basi hupata mambo mengi kutoka kwa watu...”[31]

Pia katika mambo ya mwisho kabisa ambayo Khidhr alimuusia Mussa (as) alimwambia:

“...Ama kwa hakika mambo pendwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu ni matatu, .........na kuwaonea huruma waja wake, na hatomwonea huruma mja mja mwezake, isipokuwa Mwenyezi Mungu atamwonea huruma pia siku ya kiyama..”

Pia jambo la huruma na upole ni katika adabu ambazo zimesisitizwa sana katika kuwalingania watu kumuelekea Mwenyezi Mungu, na hata katika jambo la kuamrisha mema na kukataza maovu. Mwenyezi Mungu anasema:

..Nendeni kwa Firauni ama hakika amechupa mipaka, mwambieni maneno laini, huenda akakumbuka au akaogopa...” (Surat Twaha aya 43-44).

Pia adabu hii ya upole ina faida nyingi mno za kinafsi na kijamii kwa ujumla, na inamuongezea mtu nafasi ya kuathiri na kukubalika kwa watu. Tofauti na ukali na nguvu ambazo humfanya mtu kukataliwa na hata kupingwa. Mwenyezi Mungu anasema katika Quran:

“...Lingania watu kuelekea njia ya mola wako kwa hekima na maneno mazuri, na jadiliana nao katika njia ambayo ni bora....” (surat Fusilat aya 34).

5.   Kusamehe, kwa mana ya kutomkemea, adhibu au kalipia.  Na ndio maana Quran pamoja na Bwana Mtume (saww) wamehimiza mno njia hii katika kulinda mahusiano ya kijamii, kuanzia ngazi ya familia na hata nje yake kwa ujumla.

Mwenyezi Mungu anasema:

“..Na wasameheane na wafanyiane upole, je hawakuwa ni wenye kupenda kufanyiwa upole na Mwenyezi Mungu, kwa hakika Mwenyezi Mungu ni mpole na ni msamehevu...”  (Surat Nur aya 22).

...Basi sameheni na fanyianeni upole...”

(ALbaqara aya ya 109”

“..na wanakuuliza bi jipi wanatakiwa kutoa, waambie ni upole tu...”

(Albaqara aya 219)

“...Na kusamehe kwenu ni karibu zaidi na uchamungu...”

(Al Baqara aya 237)

“..Na endapo mtadhihirsha au kuficha wema na kusamehe kunako mabaya, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe na mwenye nguvu...”

(..Surat Nisaa aya 149).

Ambapo Mwenyezi Mungu pamoja na uwezo wake wa kuadhibu bado anajisifu kuwa i mwenye kusamehe, na ukiangalia sisi tunalazimishwa kujipamba na sifa na adabu za Mwenyezi Mungu (swt). “...Na kwa Mwenyezi Mungu ndipo kuna mifano ya juu zaidi, na yeye ni mtukufu na mwenye hekima...” (Surat Nahl aya 60). Pia tunahusiwa kujipamba na tabia zake Mwenyezi Mungu Mtukufu.

“...Jipambeni kwa adabu za Mwenyezi Mungu...”.[32]

Miongoni mwa mambo ambayo Nabii Issa alizungumzishwa na Mwenyezi Mungu aliambiwa:

“....Ufaulu utakuwa kwako endapo utajipamba na adabu za muumba wako...”[33]

Imepokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saww) kwamba amesema:

“...Mwenyezi Mungu humuonea huruma mwenye kumsaidia mtoto wake katika mema, kwa njia ya kumsamehe makosa yake, na kumuombea mambo ambayo ni baina yake na Mwenyezi Mungu....”[34]

 

6.   Kumshauri na kumshirikisha katika rai.

Mwenyezi Mungu kuhusiana na hili anasema “...Na shauriana nao katika mambo...” (Surat Imran aya 159).

Na hata ukirejea kwa Imamu Ally (as) unakuta kuna maneno mengi mno yenye kuhusiana na jambo la kushauriana, mfano aliposema “...Kushirikiana katika rai hupelekea katika uhalisia na kupatia...” au aliposema “...Ni haki ya kila mwenye akili kuongeza juu ya rai yake rai za wenye akili wengine, na katika matendo yake elimu za wenye hekima....”  au aliposema “...Mwenye kushirikiana na watu hushirikiana nao katika akili zao pia...” au aliposema “...Hakizajaliwa kitu sahihi zaidi ya katika kushauriana...”

Na katika jambo la mahusiano ya baba na mtoto kuna ule msemo mashuhuri wenye kusema kwamba Mwanao akikua unga naye udugu, kwa maana ya kwamba mfanye ndugu yako pindi tu anapofikia kujitambua.

Imepokelewa kutoka kwa Imam Sadiq akisema kwamba Bwana Mtume Muhammad (saww) amesema “...Jipambeni sana na kusamehe, kwani kusamehe hakumzidishii mja zaidi ya utukufu, basi sameheni Mwenyezi Mungu awatukuze...”[35]

Hivyo ni juu ya kila kiongozi na mlezi kutokimbilia njia za ukali na adhabu moja kwa moja, bali ni juu yake kuweza kupima baina ya njia mbili za kusamehe na kuadhibu, kuadhibu ambapo sio njia pendwa. Na hii ni kutokana na kuangalia athari za kimalezi na kitabia ambazo zitapatikana baada ya kutumia njia husika.

7.   Kumfanyia wema mtoto na kumsaidia pia kutenda wema.

Imepokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq as kwamba amesema “....Mtu mmoja katika Ansar alimwambia Mtume saww, nimfanyie nani wema zaidi?. Mtume akamjibu  Wazazi wako. Yule sahaba akasema “Tayari wameshafariki..”. Mtume saww akasema “..Basi fanyia wema mtoto wako..”[36].

Pia amepokea Yunus bin Rabat kutoka kwa Imam Sadiq as kutoka kwa Mtume saww “...Mwenyezi Mungu amrehemu mwenye kumsaidia mtoto wake kutenda wema” Mmoja wa masahaba akauliza, ni vipi naweza kumsaidia mwanangu kutenda wema?. Mtume saww akasema “...Kukubali kidogo atendacho, na kusamehe yale anayoshindwa, na wala asimuingize katika mabaya wala kumfanyia hiyana...”[37]

Na hivi ndivyo ambavyo kiongozi anatakiwa kuwasaidia raia wake katika kumtii kwa kujaribu kutekeleza majukumu yake kama ambavyo inatakiwa na kutazamiwa.

8.   Kucheza nao michezo yao.

Kuna hadithi kemkem zenye kuhimiza mno jambo la mtoto kucheza na mtoto wake aina ya michezo yao. Kwa maana ya kwamba mzazi kujishusha katila ngazi ya utoto na kucheza naye kama vile mtoto mwenzie.

Imepokelewa kutoka kwa Mtume saww akisema “...Mwenye kuwa na mtoto basi ajifanye mtoto mwenzie kwake...”[38]

Pia kutoka kwa Imamu Ally as “...Mwenye kuwa na mtoto basi na yeye huwa mtoto...”[39]

Jabir bin Abdillah anapokea akisema “...Siku moja niliingia kwa Mtume saww, nikakuta kwamba Hassan na Hussein wapo juu ya mgongo wa Mtume saww, na yeye akiwa anacheza nao huku akisema “..Ngamia ni wenu, na nyie ni madereva wazuri kweli..”[40]

Pia Saad bin Abii Waqas anapokea akisema “...Siku moja niliingia kwa Mtume saww kwa ajili ya kupata chakula cha usiku, nikaona Hassan na Hussein wanampandia Mtume tumboni, nikasema Ewe Mtume Muhammad kwa hakika unawapenda sana. Mtume akasema “Na vipi nisiwapende na wakati wao ndio tulizo langu...”.[41]

Abuu Huraira pia anapokea akisema “...Tulikuwa tunaswali swala ya Isha na Mtukufu Mtume saww, na alipokuwa akisujudu Hassan na Hussein wanakuja wanampandia mgongoni, na alipokuwa akiinuka alikuwa akiwachukua kwa upole na kuwaweka chini, akirudi kusujudu tena na wao wanarudi mgongoni, ikawa hivyo mpaka sala ilipoisha akawachukua na kuwaweka mapajani mwake....”.[42]

Sasa kama tukitaka kuchukua maana hii kwa mtazamo wa jumla, ni kwmaba kiongozi anatakiwa kuondoa kila aina ya kizuizi baina yake na raia wake, pamoja na kushirikiana nao katika harakati zao za kimaisha, kama ambavyo kushirikiana nao katika huzuni na furaha zao. Na tunaposema vizuizi hatukusudii vizuizi vya kimaada tu, bali hata kwa kiroho na kimaana pia, kwa maana ya kwamba kuondoa wale wapambe ambao huwa i vizuizi vya raia kumfikia yeye na kumuelezea matatizo, shida na matakwa yao. Haya yote  ni katika mambo ambayo wafalme na watawala wamekuja kuyazua baada, na wala haikuwa sera ya mitume, maimamu, pamoja na waja wema. Kwani unakuta hawa wote hawakuwa ni wenye kujiweka tofauti na watu, kama ambavyo moja ya masahaba anamsifia Imamu Ally akisema “...Alikuwa miongoni mwetu kama sisi tu..”

9.   Uadilifu na kuwafanyia usawa.

Mtume Muhammd saww anasema “....Mcheni Mwenyezi Mungu pamoja na kuwafanyia usawa watoto wenu....”[43]

Pia anasema “..Hakika wao wana haki kwako ya kuwafanyia uadilifu, kama ambavyo wewe una haki kwao ya kukufanyia wema...”[44]

Pia anasema “....Fanyeni usawa katika kuwagawia watoto wenu....”[45]

Pia anasema “....Hakika Mwenyezi Mungu anapenda muwafanyie usawa watoto wenu hata katika kuwabusu...”[46]

Pia imepokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq as akisema “...Siku moja Mtume saww alimuangalia jamaa ambaye alikuwa na watoto wawili ambaye alikuwa akimbusu mmoja ya watoto wake bila kumbusu mwingine, Mtume saww akamwambia “..Je hutaki kufanya usawa baina yao?..”[47]

Pia Mtume saww anasema “...Mwenye kuwa na mtoto na hakumuudhi, hakumdhalilisha, basi Mwenyezi Mungu atamuingiza peponi...”.[48]

Na imepokelewa kutoka kwa Saad bin Saiid Ash ary akisema “...Siku moja nilimuuliza Imamu Ridhaa s, “..Niwe fidia kwako, vipi mtu ambaye mabinti zake huwapenda zaidi ya wavulana wake?..” Imamu Ridha akasema “..Kwa hakika mabinti na wavulana wapo sawa katika kupendwa, na hii ni kwa mujibu wa ambavyo Mwenyezi Mungu huteremsha kwa ajili yao...”[49].

Na katika kufanyia kazi haya ni kwamba, kila ambaye anachukua jukumu la kuwatawala mambo ya watu, basi ni juu yake kufanya uadilifu na usawa baina yao, pasi na kupenda, kuweka karibu huyu pasi na yule kutokana na mali, cheo au nafasi fulani na mengineyo.

10.  Kuwakirimu, kuwafanyia wema na kuungama nao.

Imepokelwa kutoka kwa Mtume saww akisema “...Wakirimuni watoto wenu, na pia wafanyieni wema...”.[50]

Pia imepokelewa kutoka kwake tena akisema “...Mwenyezi Mungu amrehemu mja ambaye humsaidia mtoto wake katika kutenda wema, kwa kumfanyia wema, kuungana naye, kumfundisha elimu na adabu...”.[51]

11.  Kuwapenda.

Kutoka kwa Imamu Ally as, “...Ni wajibu kwako kumpenda mwanao zaidi ya yeye anavyokupenda...”.

Na jambo hili ndilo linalotakiwa katika kuamiliana na watu wote kwa ujumla, katika hadithi Qudsi Mwenyezi Mungu anasema “...Viumbe vyote ni familia yangu, na nimpendaye zaidi ni mwenye kuipenda familia yangu...”.

Bila kusahau kwamba ni daraja ya juu kabisa ambayo mwanadamu anaweza kuipata, kiasi kwamba anakuwa ni kiumbe pendwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwa tu anawapenda viumbe wake. Na viumbe si wanadamu tu, bali hukusanya mpaka wanyama na wadudu, hao wote ni katika viumbe wake.

 

12.  Kutekeleza ahadi zako.

Imepokelwa kutoka kwa Mtume saww akisema “...Pendeni watoto na waoneeni huruma, na mnapowaahidi jambo basi tekelezeni, kwani wao hawajui zaidi ya kwamba nyinyi ndio wenye kuwaruzuku...”

Na imepokelewa kutoka kwa Imamu Ally as akisema “...Mmoja wenu anapomuahidi mtoto basi amtimizie...”

Pia amesema “....Hakuna jambo lolote ambalo litatengemaa kupitia uongo, wala mtu amuahidi mtoto na kisha asimtimizie, kwa maana uongo hupelekea uovu na uovu hupelekea motoni...”

Pia imepokelewa kutoka kwa Abul Hassan akisema “...Mnapowaahidi watoto basi watimizieni, kwa maana wao hujua kuwa nyinyi ndio mnaowapa riziki, na hakika hakuna linalomchukiza Mwenyezi Mungu kama ambavyo anachukia katika mambo ya wanawake na watoto..”

Na hivi ndivyo ambavyo kiongozi anatakiwa kutimiza ahadi zake kwa raia wake, na wala isiwe ahadi ni njia ya kuweza kupata kura zao kisha kuweka nyumba ya mgongo wake kila alicho ahidi baada ya kufikia malengo yake.

13.  Kuwatanguliza kuliko nafsi yako.

Mwenyezi Mungu anasema “...Na watanguliza mbele ya nafsi zao hata kama wenyewe watakuwa na shida..

Na ndio unakuta wazazi wanashinda njaa ili tu watoto wao washibe, wanakosa usingizi ili wao walale, na wapo tayari kupata tabu maishani kwa ajili ya kuwapatia wao maisha mazuri.

Sasa hivi ndivyo ambavyo kiongozi anatakiwa kuwa kama mzazi mwenye huruma kwa raia wake. Na hili ndilo jambo ambalo Bi Fatima Zahra alimsifia Imamu Ally katika hotuba yake maarufu.

14.  Na moja ya sifa za kiongozi ni kuwa na kifua kipana (Uvumilivu).

Katika hadithi tukufu kutoka kwa Imamu Ally as anasema “...Nguzo ya uongozi ni uvumilivu (kifua kipana).

15.  Moja ya mambo ambayo yanaambatana na uongozi ni nasaha.

Imepokelwa kutoka kwa Imamu Sadiq as akisema “...Nimeangalia uongozi wote nimekuta umekaa katika kuwapa nasaha waja wa Mwenyezi Mungu...”.[1] Sahih Muslim 20/3/1459

[2] Nahjul Balagha hituba ya 167

[3] Biharul anwar 6 9- 36

[4] Usulul Kafi Juz 1 mlango wa mambo ambayo Imamu anatakiwa kuyafanya kwa raia wake.

[5] Usulul kafi juz 1 uk 406

[6] Mizunul hikma 3/134

[7] Alkafi juz 2 uk 100 hadithi ya 4

[8] Albarqii Almahasin juz 1 uk 200

[9] Alkafi juz 6 uk 49

[10] Mustadrakul wasail juz 15 uk 170

[11] Usulul kafi juz 6 uk 50

[12] Jawahirul bihar mlango wa barua ya Imamu Ally kwa Malik Ashtar baada ya kumtawalisha Misri

[13] Alkafi juz 6 uk 49

[14] Alkafi Juz 6 uk 49

[15] Makarimul akhlaq uk 220

[16] Makarimul akhlaq uk 220

[17] Wasailu shia juz 15 uk 169

[18] Udatu Dai uk 87

[19] Makarimul akhlaq uk 220

[20] Kanzul Ummal hadithi ya 45958

[21] Ghurarul hikam 2378

[22] Nahjul balagha hekima ya 323

[23] Tuhaful uqul uk 393

[24] Alkhazar al qummi . Kifayatul Athar uk 240

[25] Alkafi juz 2 uk 117

[26] Alkafi juz 2 uk 117

[27] Alkafi juz 2 uk 120

[28] Kanzul Ummal hadithi ya 5393

[29] Alkafi hadithi ya 12

[30] Alkafi hadithi ya 13

[31] Alkafi hadithi ya 7

[32] Alkafi hadithi ya 16

[33] Altahdhib 6/163/299

[34]Biharul anwar

[35] Alkafi juz 8 uk 135

[36] Udatu dai uk 86

[37] Hidayatul ilm wa tandhi Ghurarul Hikam 311

[38] Alkafi juz 2 uk 108

[39] Alkafi juz 6 uk 49

[40] Tahdhibul Ahkam juz 8 uk 113

[41] Mustadrakul wasail juz 15 uk 168

[42] Man la yahdhuruhul Faqih juz 3 uk 483

[43] Alkafi juz 6 uk 50

[44] Sunanul kubra cha ibn Daud

[45] Hadithul Khalid hadithi ya 12

[46] Mizanul hikma juz 4 uk 3673

[47] Man la yahdhuruhul faqih juz 3 uk 483

[48] Awali lialiy juz 1 uk 181

[49] Alkafi juz 6 uk 51

[50] Mustadrakul wasail juz 15 uk 167

[51] Mustadrajul wasail juz 15 uk 167