Virusi vya Corona vyabadirisha ulimwengu na kuupa nidhamu mpya.

| |times read : 665
Virusi vya Corona vyabadirisha ulimwengu na kuupa nidhamu  mpya.
  • Post on Facebook
  • Share on WhatsApp
  • Share on Telegram
  • Twitter
  • Tumblr
  • Share on Pinterest
  • Share on Instagram
  • pdf
  • Print version
  • save

Virusi vya Corona vyabadirisha ulimwengu na kuupa nidhamu  mpya.

 

 


Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu


1. Matukio mengi yanayotokea na kusababisha madhara, yanaweza yakawa na matokeo hasi na mabaya kwenye maisha ya mtu mmoja  au maisha ya jamii, kama ambavyo yanaweza yakawa na athari chanya na zenye manufaa iwapo yatatazamwa kwa upande wa pili. Na maana hii unaipata katika maneno yake Mwenyezi Mungu yasemayo:

(له باب باطنه فيه الرحمة و ظاهره من قبله العذاب)

 (Ukuta wenye mlango, ndani yake mna rehema, na upande wake wa nje kuna adhabu)[1] Surat Al-Hadid: 13.


2. Hakika kuyatazama mambo kwa mtazamo chanya husaidia kuleta utulivu wa nafsi na matumaini ya moyo, kwa kuyaridhia yatokeayo na kuepukana na hofu na wasiwasi ambazo huharibu maisha na kupelekea kukata tamaa na kufeli na hatimaye kumsukuma mwanadamu kupinga na kutojali. Wakati huohuo kwa upande wa afya kama wasemavyo wataalamu, kuwa na mtazamo hasi katika matatizo husababisha udhaifu wa kinga ya mwili na kuongezeka uwezekano wa kupatwa na maradhi.


3. Na kwa mtazamo huu chanya, virusi hivi vya Corona vinaweza kugeuka badala ya kuwa ugonjwa vikawa ni tiba ya maradhi mengi ya kinafsi, kijamii, kisiasa na kifikra. Hakika virusi hivi vya Corona kutokana na hofu iliyosababishwa na virusi hivi katika nafsi za wanadamu, imeweza kuwatoa watu katika hali ya kughafilika na ukaidi wa amri za Mwenyezi Mungu, na kuwapeleka kwenye utiifu na kusalimu amri mbele ya uwezo wa Mwenyezi Mungu peke yake,  ili yeye ndio awaondoshee balaa hili[2].


4. Bila shaka virusi vya Corona vimeuweka wazi ukweli wa aya hii tukufu ya kwamba:

(مثل الذين اتخذوا من دون الله أولياء كمثل العنكبوت اتخذت بيتاً وإن اوهن البيوت لبيت العنكبوت)

 (Mfano wa wale ambao wamewafanya waungu badala ya Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa buibui aliyejitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu zaidi ni nyumba ya buibui) Surat Al-Ankabut: 41.

Vimedhihirisha udhaifu wa nguvu za kimada na kidunia zinazotawala, nguvu zilizodhaniwa kuwa zina uwezo juu ya kila kitu na kwamba hakuna chochote kiwezacho kutoka nje ya mamlaka yake, mara majeshi yao, viongozi wao na teknolojia zao walizoziandaa kwa ajili ya vita vya anga, ukiachilia mbali vya ardhini, vyote vimeshindwa kufanya chochote ili kuzuia kuenea virusi hivyo. Corona imebadilisha fedha nyingi walizokuwa wakizitumia kwa ajili ya maghala ya silaha za kijeshi, na zile zilizokuwa zikitumika kufanya uadui kwenye mataifa mengine, na kuzifanya zitumike katika huduma za kiafya na kuwasaidia raia wao. Hali kadhalika, virusi hivi vya Corona vimesimamisha makongamano yao ambayo yalikuwa yafanyike ili kupanga mikakati yakikhabithi ili kuwadhulumu mataifa na kupora mali zao.


5. Hakika balaa hili la virusi vya Corona limekuwa ni uga wa kudhihirisha maadili ya mataifa na itikadi (aidolojia) zao mbalimbali wanazoziamini ikiwa ni pamoja na kuweka wazi misingi na mihimili yao, katika kipindi ambacho wahisani wengi katika nchi zetu wanashindana kujitolea kuwahudumia waliopata maambukizi ya virusi vya Corona na kuwasitiri waliofariki kwa heshima, ikiwa ni pamoja na kuwapatia msaada familia ambazo vyanzo vyao vya riziki vimesimama, kwasababu ya zuio lililowekwa la kutotoka nje, na kuwapatia vifurushi vya vyakula bure. Kama ambavyo wamekuwa wakijitolea kutoa huduma za kupulizia dawa katika maeneo ya mikusanyiko ya watu na mabarabara, huku ukizikuta baadhi ya serikali za kimagharibi zikiwataka wananchi kutochukua hatua za lazima za kujikinga,  ili kuwalinda raia wake na kuviacha virusi hivyo vikiendelea kuwashambulia watu, wakuokoka aokoke kwa kinga yake ya mwili wake mwenyewe na kuwaacha wazee na wale wenye maradhi yemelezi bila kuwaandalia vifaa maalumu wala kuwapatia huduma zozote zile za msingi kwao, ili mpaka virusi hivyo vinamalizika vimalizike kwa kupunguza kinga ya watakaopona na kwa kufariki wale wasio kuwa na kinga ya kutosha, ili kwa njia hiyo serikali hizo ziwe zimeepukana na kulipa pesa za huduma ya jamii kwa watakaokuwa wamekufa ambao wamekuwa ni mzigo mkubwa kwa serikali hizo kwa mitazamo yao, wakati huduma hizo ni matunda ya kodi walizokuwa wakizitoa kipindi wakifanya kazi zao. Hivyo utaona ni namna gani heshima ya mwanadamu ilivyoporomoshwa na hasa hasa kwa watu wenye umri mkubwa ambao katika sheria yetu ya Kiislamu wanastahiki kila aina ya heshima.


6. Hakika kila kilichotokea au kinachoendelea kutokea kinawataka wanadamu kutathimini fikra, mienendo, misingi na vipaumbele inavyoviamini, kama ambavyo kinawataka wanafikra, wanafalsafa na wana nadharia kuharakia kufanya mabadiliko makubwa wakinufaika na uzoefu wa virusi hivi vya Corona, sababu zake na matokeo yake kabla ya muda kupotea, kwa sababu ukweli ni kwamba mpaka sasa hatuna salama ya kutokumbwa na jambo lingine litakaloshindikana kukabiliana nalo hata kwa kutumia zile njia ambazo zimefanikiwa kuidhibiti Corona walau kwa kiwango kidogo.


7. Balaa hili la virusi vya Corona ni moja kati ya matokeo mabaya ambayo mwanadamu hujisababishia mwenyewe na jamii yake kwa matendo yake maovu[3]:

(وما أصابكم من مصيبة فبما كسبت أيديكم ويعفو عن كثير)

 (Na misiba inayowasibu ni kwa sababu ya yalitendwa na mikono yenu. Naye anasamehe mengi) Surat Ash-Shura:30.
Na Mwenyezi Mungu aliyetukuka huwaepushia viumbe wake mabalaa mengi sana kama asemavyo:

( له معقبات من بين يديه ومن خلفه يحفظونه من امر الله)

(Kila mtu ana yanayomfuatilia (malaika) mbele yake na nyuma yake yanamhifadhi kwa amri ya Mwenyezi Mungu.) Surat Ar-Ra'd: 11.

)إِنَّ رَبِّي رَحِيمٌ وَدُودٌ(

(Hakika Mola wangu ni mwenye kurehemu, mwenye upendo.) Surat Hud: 90.


8. Huu ndio uhusiano wa dhati uliojengeka juu ya rehema baina ya Mwenyezi Mungu na viumbe wake, ingawaje ukweli ni kwamba uhusiano huo ni wa upande mmoja ambao ni upande wa Mwenyezi Mungu aliyetukuka, kwani mwanadamu hauthamini upendo huu wala hampatii Mwenyezi Mungu haki yake[4]:

)وَمَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ(

 (Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadiri yake) Surat Al-An'am: 91.

Lakini Mwenyezi Mungu anaweza akaona kuwa masilahi kwa mja wake ni kumuacha mwenyewe na aliyoyachuma kwa mikono yake, na asiingilie kumuokoa na malaika wakaondoa zile kinga ambazo humlinda mwanadamu baada ya kugeuka kwake na kupinga kwake kwa muda mrefu na  kuwa ni madhara kwa ajili ya nafsi yake na madhara kwa wengine. Akamuacha akabiliane na matokeo ya matendo yake kwa ajili ya masilahi yake mwenyewe, kwa matarajio kuwa anaweza kurudi kwenye uongofu na anarekebisha mambo yake yaliyoharibika[5].


9. Hivyo, ni wajibu wa waumini wawaidhike na kuzuiwa kwao kuizuru nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu mtukufu, msikiti mtukufu wa bwana Mtume (s.a.w.w) na haramu takatifu za maimamu maasumina (a.s). Hali kadhalika wawaidhike na uwazi ulipo katika misikiti ya sala za jamaa, ambayo sasa imekuwa wazi na dhikiri na dua, na wachukue tahadhari wasije wakawa ndio walengwa wa kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

(وان تتولوا يستبدل قوماً غيركم ثم لا يكونوا امثالكم)

(Na mkigeuka atawaleta watu wengine badala yenu, nao hawatakuwa kama nyinyi.) Surat Muhammad: 38.


Imeandikwa na:

Muhammad Yakoobi- Najaf Ashraf
28 Rajab 1441H, sawa na
23/03/2020

Imetafsiriwa na:

Abdallah Khamisi Salum

 



[1]. Rejea: Tafsiri ya aya hiyo katika kitabu cha Mausuat Khitwab, Juz: 8, UK: 164 na katika Tafsiri Min Nooril-Marhalah: Juz:1, Uk: 272 chini ya anuwani ya Mawaidha ya Qur'ani, Juz/ Surat Al-Hadid.

[2]. Baadhi ya nchi za Ulaya zilizokuwa zikiziwia kutolewa adhana kwa sauti kama vile Italia, Ispania na Ujerumani zimeruhusu itolewe kwa sauti na kwa kutumia vipaza sauti ili kuleta utulivu na amani kwa wakazi wake, kama ambavyo raisi wa Marekani ndugu Donard Trump aliitangaza siku ya Jumapili 15/03/2020 kuwa ni siku ya maombi kitaifa. Aidha, 19/03/2020 vyombo  vya habari vimenukuu kauli ya waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte akisema:  "Hakika tumepoteza matumaini, virusi vimetuuwa kinafsi, kimwili, na kiakili, sasa hatufahamu tena nini cha kufanya, mbinu zetu zote za ardhini zimekwisha, sasa tumwachie Mungu".  Ikizingatiwa kwamba Italia ni miongoni mwa nchi zilizoathirika kwa kuwa na wafu wengi wa Corona. Kuna baadhi ya vyombo vya habari vilijaribu kukanusha maneno haya kutoka kwa waziri Mkuu Conte rasmi baada ya siku kadhaa, na kwamba Italia haijatangaza kusalimu amri kushindwa kukabiliana na virusi vya Corona. Huwenda kweli yalikuwa maneno ya kuzingishiwa na  kwamba katika maneno yake hakukuwa na mambo yanayoweza kuzua chuki. Ingawaje kung'ang'ania kukanusha hakuna maana isipokuwa habari hiyo itakapokuwa ina hisia za mwamko wakidini.

[3]. Rejea: Mausuatu Khitwab Al-Marhalah: Khitwabul-Marhalah: 11, Uk: 201, na katika Tafsiri Min nuril Qur’an, Juz: 4, Uk: 272 kwa ufafanuzi wa aya hii tukufu.

[4]. Rejea: Mausuatu Khitwab Al-Marhalah: Khitwabul-Marhalah: Juz: 9, Uk: 472, na katika Tafsiri Min nuril Qur’an, Juz: 1, Uk: 224  katika tafsiri ya kauli ya Mwenyezi Mungu iliyopo katika surat Al-Hajj: 74.

[5]. Rejea: Mausuatu Khitwab Al-Marhalah: Khitwabul-Marhalah: 9, Uk: 171, na katika Tafsiri Min nuril Qur’an, Juz: 1, Uk: 85 kwa ajili ya ufafanuzi wa fikra hii wakati ikitafsiriwa kauli yake Mwenyezi Mungu: (له معقبات من بين يديه له معقبات من بين يديه) iliyotajwa huko nyuma.