“..Hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu..”

| |times read : 894
“..Hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu..”
  • Post on Facebook
  • Share on WhatsApp
  • Share on Telegram
  • Twitter
  • Tumblr
  • Share on Pinterest
  • Share on Instagram
  • pdf
  • Print version
  • save

 “..Hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu..”[1]

Kwa hakika dini katika matumizi ya neno hili, humaanisha mfumo, misingi na fikra ambazo mwanadamu hushikamana nazo pamoja na kila mambo yenye kuambatana na mienendo yake. Na kila mwanadamu katika dunia hii ni lazima awe ana dini maalumu, hata hao ambao huonekana kwamba wamekengeuka kupita mipaka. Na dini hiyo inaweza kuwa ni yenye kumtegemea Mungu au mambo ya kimaada ambayo hutengenezwa na wanadamu wenyewe, kwani hata hao ambao wanajiita kwamba hawana dini bado utakuta katika mambo yao kama vile uhuru bila mipaka, ndoa za jinsia moja, ni yenye kujaribu kuvunja ile thamani ya dini.

Hata ukirejea katika aya tukufu utakuta inajaribu kuelezea uhalisia huu ambao ni jambo la kimaumbile ya kibinadamu, aya haielezei kwamba kila mwanadamu anatakiwa kuwa na dini, bali inakwenda moja kwa moja katika hatua ya pili ambayo ni kutaka kumuelewesha huyu mwanadamu dini ambayo anatakiwa kushikamana nayo, na kumuelekezea huko ikiwa ni pamoja na kumpoa mwongozo wa kutenda mambo yake kwa mujibu wa dii hiyo. Na hii ni kutokana na kwamba Mwenyezi Mungu ni mwingi wa fadhila, hivyo hawezi kumuacha mwanadamu awe ni mwenye kuhangaika kila siku kwa kuzama katika makosa au kutegemea tajriba ili kuweza kufikia katika lililo sahihi, bali amemwekea njia ambayo itaweza kumfikisha katika ukamilifu:

“...Kwa hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu”.

Na lugha iliyotumika hapa ni “Hasr” kwa maana ya kukataa na kukanusha kila aina nyingine ya dini hata kama watu watapoteza nguvu zao katika kuchunga hukumu na mafunzo yake.

Neno “Uislamu” lina maana ya kujiepusha na jambo na kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu (swt), na ni anuani yenye kukusanya mengi, lakini hapa ameifanya maalumu tu kwa ajili ya dini ambayo amekuja nayo Mtume Muhammad (saww) na ikawa ni sababu ya kukamilishwa kwa dini na utume wote uliotangulia, na hii ni kwa sababu tu yenyewe ni kamili na makini zaidi katika kutumikia maana ya Uislamu “Kujisalimisha” katika kila nyanja za maisha ya moja mmoja mpaka jamii, na pia hakuna dini nyingine yeyote ambayo imepata sifa ya “....Kwa hakika leo nimekukamilishieni dini yenu, na kuwatimizia neema zangu, na nimeridhia kuwa Uislamu kwenu ni dini....”[2]   tofauti na dini ya Kiislamu.

Aya ambayo ndani yake kuna ishara ya kukubali yale ambayo wamekuja nayo mitume iliyopita “....Hatukuwa ni wenye kutofautisha yeyote katika wao, na sisi ni wenye kujisalimisha kwao...”[3]

Isipokuwa tu, kuabudu na kujikaribisha kwa Mwenyezi Mungu ni lazima kuwe kwa misingi ya dini hii ya mwisho.

Bila shaka uhalisia huu unakubalika na kila akili bila ya kuhitajia dalili ya aina yeyote ile, na hakuna ambaye atatia shaka isipokuwa i wale ambao Mwenyezi Mungu amesema “....Na wakapingana nayo hali ya kuwa nafsi zao ni zenye kukubali, na dhulma na kujikweza tu....”[4]

Na hii ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndio muumbaji wa mwanadamu, hivyo anajua hata ambayo yapo ndani ya nafsi yake na yenye kutengeneza mambo yake, basi ni kawaida sana kwake kuweza kuandaa mfumo ambao utakuwa ni sababu ya kupangilia maisha yake na kumfikisha katika ubora na ukamilifu.

Na katika sura hiyohiyo (Al Maidah), Mwenyezi Mungu anaongezea aya nyingine yenye kuashiria kwamba wanadamu wanatakiwa kushikamana na Uislamu tu na si dini nyingine, anasema “..Je, wanashikamana na dini nyingine hali ya kuwa kwake yeye kila ambacho kipo katika mbingu na ardhi kimejisalimisha kwa kupenda au bila kupenda, na kwake vyote vitarejea?...[5]

Kwa maana ya kwamba ulimwengu waote unaenda kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu, kama ambavyo unakwenda kwa mujibu wa nidhamu ambayo yeye ameiweka. Na mwanadamu si lolote zaidi ya kuwa ni sehemu ndogo sana katika huu ulimwengu, kwani anazaliwa bila ya matakwa yake, anakuwa na kuzeeka mpaka kufariki pia bila ya kuwa na maamuzi katika hayo, na huku ndiko kujisalimisha kimaumbile ambapo kunatakiwa kuendana na kujisalimisha kisheria ili harakati zake zote ziweze kuendana na ulimwengu kamili. Na kama hatofanya hivyo bila shaka ataangukia katika mabalaa na majanga mazito.

“..Na je kuna mwenye dini kamili zaidi ya mwenye kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu hali ya kuwa ni mwema?...”.[6]

Elimu za kisasa pia katika miaka ya karibuni zimeweza kugundua jambo hili, ya kwamba mwanadamu endapo ataamua kuachana na mipangilio ya kiulimwengu na tabia zake basi anakuwa ni mwenye kujitafutia maangamio, na hii ni hata katika ngazi za jamii na nchi pia.

Muhimu hapa ni hili swali katika aya hii “..Je, wanashikamana na dini tofauti na dini ya Mwenyezi Mungu...”

Kuna aina fulani ya kuuliza kulikoambatana na makemeo kwa kutoka katika nidhamu na mpangilio huu wa Ulimwengu ulio kamili, kisha jawabu linakuja baada ya aya mbili likionyesha mwisho mbaya wa kutoka na kuachana na mpangilio huu wa kilimwengu.

“...Na mwenye kushikamana na dini tofauti na Uislamu hatakubaliwa matendo yake, na siku ya kiyama atakuwa i mwenye kupata hasara pia....”.[7]

Hivyo mwenye kushikamana na dini pasi na Uislamu atakuwa amepata hasara, kwa maana anakuwa amepoteza hii tunu yenye thamani ambayo Mwenyezi Mungu (swt) amempatia, na anakuwa amebadilishana na yale ambayo hayana uhalisia ikiwa ni pamoja na kumaliza umri wake katika kufuata matamanio yake au mambo yasiyo na uhakika. Na kuhusiana na nukta hii Imamu Ally (as) anasema:

“...Mwenye kushikamana na dini pasi ya Uislamu uovu wake unadhihirika, na thamani yake inashuka, na upotevu wake unakuwa ni mkubwa, na mafikio yake huwa ni huzuni na adhabu kubwa. Nami najisalimisha kwa Mwenyezi Mungu ukweli wa kujikurubisha, huku nikimuomba anionyeshe njia ya kufikia pepo yake, na yenye kupeleka katika yale ambayo Mwenyezi Mungu anayataka....”[8]

Pia anasema sehemu nyingine:

“....Enyi watu, kwa hakika dini yenu ndiyo dini sahihi hivyo shikamaneni nayo, asije akawatoa mtu wala kuwapambieni isiyokuwa hiyo, kwani jambo baya katika Uislamu ni bora kuliko jambo jema katika dini nyingine, kwa sananu jambo baya huku husamehewa, lakini jema la kule halikubaliwi....”[9]

Hivyo basi tuiangalie kwa umakini mno nafasi hii maadamu bado tupo katika ulimwengu huu, na itambulike kwamba milango ya kutendea kazi fursa hii bado ipo wazi. Tushikamane na dini yetu pamoja na kuifanya kuwa ndio jambo la muhimu sana kwetu, na kama si hivi basi uhakika huu utakuja gundulika siku ya kiyama, siku ambayo hakuna majuto yatakayofaa. “..Na yeye siku ya kiyama atakuwa ni mwenye kupata hasara”.[10]

Siku ambayo wale wenye kupinga dini watakuja kujua ni nani hasa ndiye mwenye kunufaika siku hiyo?.

Pia ni lazima tutambue ya kwamba Uislamu si tu kutamka shahada mbili, na wala si tu kuishia katika kutekeleza ibada zako za wajibu, kwani maana halisi ya kutii haipatikani katika hayo tu, bali inatakiwa kushikamana na kuiweka dini katika kila nyanja ya maisha yako yote, na huu ndio Uislamu na sio dhahiri ya mtu na kujiweka kwake pembeni na watu na kujificha mapangoni. Kwa sababu moja ya alama kubwa za dini ni kujipamba nayo na kisha kuwavuta watu kwayo. Imepokelewa kutoka kwa Imam Baqir (as):

“...Hana dini mtu ambaye hamwenezi Mwenyezi Mungu katika kuamrisha mema na kukataza mabaya...”[11]

Na hata Imamu Ally (as) unakuta anawakemea vibaya sana wale wenye kufanya dini yao ni matamanio yao ya pesa na mali anasema:

“...Na ikafikia dini ya mmoja wenu ikawa ni pambo katika ulimi wake, matendo yake ni kama matendo ya mtu aliyemaliza kabisa matendo yake, na ameshateka moyo wa bwana wake....”[12]

Kwa maana ya kwamba kutilia kwenu umuhimu dini yenu kunakuwa kana kwamba tayari mmeshamaliza majukumu yenu yote kwa Muumba wenu na kuchukua kiwango cha juu kabisa katika ridhaa yake, na kwamba hamhitajii kabisa jambo lolote kutoka kwake, hapana kabisa mambo si hivyo.

Pia mepokelewa tena kutoka kwake Imamu Ally (as) akisema:

“....Ikiwa utafanya dini yake ifuate dunia yako basi utakuwa umekosa dini na dunia kwa pamoja, na bado siku ya kiyama hautakuwa katika wenye kufaulu....”[13]

Na hata Quran unakuta imetoa kipaumbele sana kwa dini kwa kuitanguliza mbele ya kila kitu, Quran inasema “....Na fitina ni mbaya kuliko kuuwa” (Baqara aya 191) pia inasema “...Na fitina ni kubwa kuliko kuuwa...” (Baqara 217). Kwa maana ya kwamba kujitolea nafsi yako katika dini kwa lengo la kushikamana nayo ni moja ya maana za kutoifanyia fitina dini ile.

Pia imepokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq (as) katika kufasiri aya ya Quran isemayo “...Na Mwenyezi Mungu akawaepushia mabaya yote ambayo waliwapangia...” (Surat Ghafir aya 45) anasema:

“....Kwama alikuwa ni yule muumini katika kaumu ya Firauni, ambaye walimkata vipande vipande lakini Mwenyezi Mungu akamwepusha na kufitiniwa katika dini yake...”[14]

Na pia katika nukta hii kuna riwaya nyingi kutoka kwa Maasumina (as), imepokelewa kutoka kwa Imamu Ally (as) kwamba amesema:

“...Kama kutatokea balaa lolote basi wekeni nfasi zenu na si dini yenu, na tambueni ya kwamba mwangamiaji ni yule ambaye imeangamia dini yake, na mpigwa vita mkubwa ni mwenye kupigwa vita dini yake....”[15]

Na hata ambao Mwenyezi Mungu amewaafikisha kupata radhi zake, wamefikia katika hali ya kutambua umuhimu huu na wakabakia katika dini zao pamoja na kuwepo vikwazo ambavyo vimejitokeza mbele yao, na magumu ya kila aina ambayo yangeweza kuwa tishio katika hilo.

Quran inasimulia visa vyao ikiwa baadhi yao ni kama vile kuwaonea huruma, mfano ni wahanga wa mahandaki, ambao walichimbiwa hayo mashimo na kisha kuwashiwa moto na kutumbukizwa lakini bado hawakumpa nafasi dhalimu ya kuweza kuichukua dini yao. “..Na hawakuwa ni wenye kuwafanyia maudhi isipokuwa i kwamba tu walikuwa ni wenye imani na Mwenyezi Mungu mtukufu na mwenye sifa...”[16]

Au kama mfano wa wale wachawi wa Firauni ambao walitishiwa kukatwa mikono na miguu kisha kuuliwa, jibu lao lilikuwa ni:

“...Hukumu vyovyote vile, kwa hakika hutohukumu isipokuwa maisha ya duniani tu, kwani sisi tumemuamini mola wetu ili atusamehe makosa yetu....”[17]

Au mfano wa mke wa Firauni  ambaye hakujisalimisha kwa Firauni na mateso yake ya kinyama, bali mtazamo wake kwa Mwenyezi Mungu ulikuwa ni:

“...Ewe Mwenyezi Mungu, nitengenezee makazi huko peponi, na uniepushe na Firauni pamoja na vitendo vyake...”[18]

Au mfano wa Ashabul Kahf, ambao vyeo vyao havikuwazuia kitu, na wala hawakujali vitisho vya wakubwa wa Roma kipindi hicho:

...Walipoamua kusimama na kusema kwamba Mola wetu ni Mola wa mbingu na Ardhi na wala hatutamuomba mwingine tena, kwani tutakuwa tumesema yasiyo na maana...”[19]

Na kwa upande wa pili wa wale ambao Shetani aliwadanganya na wakaifuata dunia pia kuna mifano yao, kama vile Hakimu mkuu wa Dola ya Abbasiya, ambaye alichukua jukumu la kumuua Imamu Jawad kwa husuda tu.

Au kama vile Hamid bin Qahtaba, kiongozi na mtawala wa Dola ya Abbasiya ambaye katika pokezi inayokuja tutaona baadhi ya unyama na ubaya wao pamoja na chuki zao kwa watu wa nyumba ya Mtume (saww), na namna ambayo hawa mashetani watu walivyokuwa wanajitahidi kuwatoa watu katika dini zao, na hakuna zaidi ya hilo ambalo wangeridhika nalo.

Katika kitabu cha Akhbarul Ridhwa cha Sheikh Swaduqi akipokea kutoka kwa Ubaydullah Al Bazzar Al Nisabuuriy anasema:

“...Baina yangu na Hamid bin Qahtaba kulikuwa na muamala fulani, nikafunga safari kumuelekea siku moja na yeye akajiwa na habari ya ujio wangu, hivyo akanipokea bila hata ya kupumzika wala kubadili nguo zangu na ilikuwa ni mwezi wa Ramadhani mida ya adhuhuri. Basi nilipoingia nikamkuta akiwa katika nyumba yake nami nikamsalimia na kisha kukaa. Kukaja birika na bakuli la kunawia na kisha chakula kikatengwa, nami kwa kusahau kama nilikuwa nimefunga nikataka kuanza kula lakini kabla ya kuweka mdomoni nikakumbuka na kujizuia, Hamid akaniuliza “..Vipi mbona hauli?”. Nikamjibu “...Ewe kiongozi huu ni mwezi wa Ramadhani, nami si mgonjwa wala mwenye udhuru wenye kunifanya nifungulie, huenda kiongozi ukawa na udhuru wenye kukupa ruhusa ya kufuturu...”. akasema “...Sina ugonjwa wala udhuru bali ni mzima kabisa...” kisha akatokwa na machozi mno.

Baada ya kumaliza chakula chake nikamuuliza, ni kipi kilikuliza ewe Kiongozi?. Akasema “..Siku moja Harun Rashid alipokuwa mjini Tusi alinitumia ujumbe kwamba nihudhurie, nilipofika nilimkuta akiwa amewasha mishumaa na mkononi mwake ana upanga ulionolewa vizuri kabisa, na pembeni yake kulikuwa na kijakazi. Akaniluliza “...Ni vipi unamtii kiongozi wa waumini?”  nami nikamjibu kwamba ni kwa nafsi yangu na mali zangu. Akatikisa kichwa na kisha kuniruhusu kuondoka.

Nilipofika nyumbani sikukaa sana mara akaja tena mjumbe kutoka kule kule na kunitaka niene tena kumjibu kiongozi wa waumini. Nikajisema moyoni ya kwamba nahofia isiwe kiongozi alikuwa na azma ya kuniua, lakini aliponiona akapatwa na haya kidogo.

Basi nikamwendea na kukaa mbele yake na kisha akaniuliza tena “...Vipi unamtii kiongozi wa waumini?”. Nikasema kwamba ni kwa nafsi, mali, familia na hata watoto wangu. Basi akatabasamu na kucheka sana, na hii ni kwa sababu kiongozi alijua fika kwamba Qahtaba alikuwa ameshajua ni nini kinatakiwa kutoka kwa kiongozi yule na kwamba i jambo kubwa zaidi ya hilo.

Basi baada ya hapo akaniruhusu kuondoka nami nikaondoka, kwa mara nyingine tena sikupumzika akaja mjumbe na kunitaka niende tena kwa kiongozi, nami nikakubali wito na kisha kuelekea kwake. Nilipofika akaniuliza tena “....Ni kwa kiasi gani unamtii kiongozi wa waumini?”. Nikamwambia ni kwa kiwangi cha nafsi, mali, familia, watoto na hata dini yangu. Basi akacheka sana na kisha kusema “...Chukua huo upanga hapo na kisha ufanye atakachokuamrisha huyo kijakazi”. Basi yule kijakazi akachukua upanga na kunipatia na kisha kuongozana nami mpaka katika nyumba ambayo mlango wake ulikuwa umefungwa, akaufungua mara tukakuta ndani yake kuna kisima. Na pembeni kulikuwa na nyumba tatu nyinginezo ambapo alifungyua moja yake ambapo ndani yake kulikuwa na wazee kwa vijana waliofungwa, kisha yule kijakazi akaniambia “...Kiongozi anakuamuru umauwe hawa watu..”.

Na wote walikuwa ni katika kizazi cha Ally na Fatima, basi mmoja mmoja akwa akitoka namkata na upanga na kisha tunamtupa katika kile kisima. Kisha akafungua tena nyumba nyingine ambapo ndani yake kulikuwa na watu ishirini wengine katika kizazi cha Ally na Fatima, nao nikawa nakata na upanga mmoja mmoja na kisha kutupia katika kile kisima. Mpaka ilipofikia mtu wa kumi na tisa ambaye alikuwa ni mzee mwenye nywele nyingi, aliniambia “...Umeangamia ewe usokuwa na haya, hivi utakuwa na udhuru gani siku ya kiyama utakapokutana na babu yetuMtume Muhammad (saww)hali ya kuwa umeshaua katika kizazi chake watu wapatao sitini ambao ni katika izazi cha Ally na Fatima (as)?”.

Basi mkono wangu ukaanza kutetemeka na yule kijakazi akaniangalia kwa hasira sana, basi nikamwendea yule mzee pia nikampiga upanga na kumuua kisha kumtupa katika kile kisima.

Sasa kama itakuwa haya ndio matendo yangu, nimeshaua watu sitini katika kizazi cha Mtume (saww) unadhani funga na sala zangu zitanisaidia nini?, kwa maana sina shaka kwamba mimi ni wa kudumu motoni....”[20]

Na mfano wa pili ni Umar bin Saad bin Abi Waqas ambaye pia alikuwa na ukaribu na Imamu Hussein (as), na anamtambua vizuri tu, lakini kujiona kwake na tamaa zake juu ya utawala wa Rei na Gorgan ikapelekea kutenda kosa kubwa ambalo limepelekea kukosa dunia na akhera. Na hata mwenyewe katika usiku ambao alitakiwa kutoa maamuzi alikuwa akisema:

“...Je, niachane na utawala wa Rei wakati ndio lengo langu?, au nibakie ni mwenye dhambi kwa kumuua Imamu Hussein?.

Najua kuwa Hussein ni mwana wa Mjomba wangu, na mengine mengi, lakini naapa kwamba Rei ndio tulizo la moyo na macho yangu....”



[1] Surat Imran aya 19

[2] Surat Maidah  aya 3

[3] Al Baqarah aya 136

[4] Surat Naml aya 14

[5] Surat Al Imran aya 83

[6] Surat Nisaa aya 125

[7] Surat Imran aya 85

[8] Nahjul Balagha 161, katika hotuba yake yenye kumsifia Mtume Muhammad pamoja na kuhimiza watu kunako uchamungu.

[9] Alkaafi juz 2 uk 464

[10] Al Imran aya 85

[11] Biharul anwaar juz 100 hadithi ya 59

[12] Nahjul Balagha hotuba ya 113

[13] Ghurarul hikam 3751

[14] Biharul anwar juz 13 hadithi ya 5

[15] Alkaafi juz 2 haduthi ya 2

[16] Surat Buruj aya 8

[17] Surat Twaha aya 72-73

[18] Surat tahrim aya 11

[19] Surat Kahaf aya 14

[20] Uyunu akhbarul ridha juz 1 uk 108

   Biharul anwar juz 48 uk 178