Kumuomba Msaada Mwenyezi Mungu Katika Usiku wa Nusu ya Mwezi wa Shabani

| |times read : 715
Kumuomba Msaada Mwenyezi Mungu Katika Usiku wa Nusu ya Mwezi wa Shabani
  • Post on Facebook
  • Share on WhatsApp
  • Share on Telegram
  • Twitter
  • Tumblr
  • Share on Pinterest
  • Share on Instagram
  • pdf
  • Print version
  • save

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu

Kumuomba Msaada Mwenyezi Mungu Katika Usiku wa Nusu ya Mwezi wa Shabani


        Leo hii tumo ndani ya Mwezi wa Shabani uliosheheni kheri nyingi kwa waumini. Na sasa tunaukaribia usiku wa nusu ya Shabani ambao fadhila zake nimepokelewa kutoka kwa Imamu Baaqir (a.s) aliposema:

(هي أفضل ليلة بعد ليلة القدر فيها يمنح الله العباد فضله ويغفر لهم بمنَّه، فاجتهدوا في القربة الى الله تعالى فيها، فإنها ليلة آلى الله عز وجل على نفسه أن لا يردَّ سائلاً فيها ما لم يسأل الله فيها المعصية)


(Usiku wa nusu ya Shabani ni usiku mbora zaidi baada ya usiku wa Lailatul Qadri, ndani ya usiku huu Mwenyezi Mungu (swt) huwapa waja wake neema na huwasamehe kwa huruma yake, basi jitahidini kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu ndani ya usiku huo, kwani ni usiku ambao Mwenyezi Mungu mwenye nguvu na aliyetukuka ameapa kuwa hatamrudisha muombaji ndani yake ilimradi tu hataomba jambo la maasi.)

Vile vile imepokewa kuwa usiku huo ndio uliokusudiwa katika kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

(فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ)

(Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hekima.) Surat Ad-Dukhan: 4.


Kwani ndani ya usiku huo Mwenyezi Mungu huandika umri wa viumbe na kugawa riziki za mwaka mpaka mwaka, na kuteremsha yote yanayotokea ndani ya mwaka mzima kama isemavyo hadithi tukufu ya bwana mtume Muhammad (s.a.w.w).

        Hivyo, tuitumie fursa hii  yenye baraka kwa kumfanyia maombi  na kumwombea dua ya ulinzi, ushindi, kuwezeshwa na kuharakisha faraja ya kiongozi wa Mwenyezi Mungu hapa duniani (Roho za walimwengu ziwe ni fidia yake) ili aje kuijaza dunia usawa na uadilifu kama ulivyojazwa dhuluma na uovu. Na tumuombe Mwenyezi Mungu atufariji kwa kutuondolea huzuni na machungu, na atuchugulie yale anayoyapenda na kuyaridhia tukiwa ni wenye raha na afya, na afanye hatima ya mambo yetu kuwa kheri.


       Miongoni mwa dua zilipokelewa kutoka kwa maasumina katika uga huu ni pamoja dua aliyoiomba bwana mtume (s.a.w.w) siku ya vita vya Badiri[1] na ambayo pia ndio ilisomwa na Imamu Hussen (a.s) siku ya Ashuraa[2], ambayo ni:


(اللَهُمَّ أَنْتَ ثِقَتِي‌ فِي‌ كُلِّ كَرْبٍ ؛ وَأَنْتَ رَجَائِي‌ فِي‌ كُلِّ شِدَّةٍ ؛ وَأَنْتَ لِي‌ فِي‌ كُلِّ أَمْرٍ نَزَلَ بِـي‌ ثِقَةٌ وَعُدَّةٌ، كَمْ مِنْ هَمٍّ يَضْعُفُ فِيهِ الْفُؤَادُ، وَتَقِلُّ فِيهِ الْحِيلَةُ، وَيَخْذُلُ فِيهِ الصَّدِيقُ، وَيَشْمَتُ فِيهِ الْعَدُوُّ، أَنْزَلْتُهُ بِكَ، وَشَكَوْتُهُ إلَيْكَ، رَغْبَةً مِنِّي‌ إلَيْكَ عَمَّنْ سِوَاكَ، فَفَرَّجْتَهُ عَنِّي، وَكَشَفْتَهُ، وَكَفَيْتَهُ، فَأَنْتَ وَلِي‌ُّ كُلِّ نِعْمَةٍ، وَصَاحِبُ كُلِّ حَسَنَةٍ، وَمُنْتَهَى‌ كُلِّ رَغْبَةٍ).


(Ewe Mola wangu! Wewe ndio tegemeo langu katika kila huzuni, na wewe ndio tumaini langu katika kila tatizo, na wewe ni tumaini na tegemeo langu katika kila linalonisibu.

Ni wingi wa huzuni ulioje ambazo huzidhofisha nyoyo, na ujanja hufeli, na rafiki hushindwa kusaidia, wakati adui akifurahi, nilizokufikishia na kukushitakia kwa ajili ya shauku yangu kwako na sio kwa asiyekuwa wewe ukanifariji na kuniondolea huzuni hizo na kuzizuia!

Bila shaka wewe ndio msimamizi wa kila neema, na mmiliki wa kila wema na lengo la kila ombi na hitajio.)


Miongoni mwa dua zilozopokewa pia, ni ile iliyokuwa ikiombwa na Imamu Sajjaad (a.s)  pindi anaposibiwa na jambo nzito au apatwapo na tatizo na wakati anapokuwa katika shida, ambayo ni dua ya saba katika Swahifatu Sajjadiyyah. Dua hiyo inaanza kwa kusema:

(يامن تُحلَّ به عُقد المكاره)

 (Ewe ambaye kwako hufunguka mafundo ya matatizo!)


Sayyid Ibin Twawuusi amenukuu katika kitabu cha Muhaju Ad-Da'waat kwamba Eliyasa bin Hamza Alqummii alimwandikia Imamu Al-Haadi (a.s) akimlalamikia yanayomsibu kutokana na waziri wa Khalifa wa banu Abbasi na juu ya hofu yake ya kuuwawa, Imamu akamwandikia kuwa: (Usiwe na woga wala shida, Muombe Mwenyezi Mungu kwa dua hii atakuokoa hivi karibuni na atakufariji, kwa hakika watu ya nyumba ya mtume (s.a.w.w) wamekuwa wakiomba dua hiyo pindi wapatwapo na matatizo, wadhihirikiwapo na maadui, wanapohofia umasikini na wawapo na mazito). Akaomba dua ile mwanzo wa mchana, haikupita nusu yake isipokuwa aliachiwa huru na kapewa heshima.


       Miongoni mwa matendo mengine yafanyikayo ndani ya usiku wa nusu ya mwezi Shaban ni Kumuomba msaada Mwenyezi Mungu na Kujielekeza kwake kwa kusema:

(يا غياث المستغيثين أغثني)

 (Ewe mtoa msaada kwa mwenye kuomba msaada! Nisaidie na uninusuru).

      Marehemu Sheikh Ahmad Al-Waaili amesimulia tukio linaloonyesha athari ya mnada (wito) huu kwa kusema kuwa, siku moja mfalme aliamka akiwa na huzuni kubwa na asiye na furaha, lakini hakujua sababu yake ni nini, wasaidizi na washauri wake walijaribu kufanya kila waliwezalo ili kubadilisha hali yake na kumwingizia furaha na kumwandikia ile huzuni bila mafanikio. Akawaamuru waandae jahazi ili waende wakazunguke baharini huwenda hali yake ikabadilika, wakafanya alivyotaka na kumwandalia kila alichokijitajia kisha wakaelekea kwenye safari yao baharini. Wakiwa ndani ya bahari alisikia sauti ya mtu akiomba msaada kwa Mwenyezi Mungu. Akawaamuru watu wake waingie baharini kumtafuta mtu huyo mpaka wampate na kumuokoa. Baada ya kumpata walimleta kwa mfalme. Mfalme akamuuliza nini kimetokea? Yule bwana akajibu akisema: Tulikuwa katika safina, mara bahari ikachafuka na kuwa na mawimbi makubwa, safina ilipasuka na wasafiri wote walizama isipokuwa Mimi nilikuwa nikiomba msaada kwa Mwenyezi Mungu aliyetukuka nikipaza sauti kwa kusema: (Ewe mtoa msaada kwa mwenyekutaka msaada! Nisaidie na uninusuru), ndipo mkawa mmekuja na kuniokoa.


       Yote hii ni milango ya rehema za Mwenyezi Mungu na sababu za kuteremka
kwa wema wake.

       Hivyo, tumuombeni Mwenyezi Mungu wema wake utushamili na azibadili hali zetu mbaya kwa uzuri wa hali yake, na ayaimarishe mambo ya dini na dunia yetu yaliyoharibika.

       Bila shaka miongoni mwa athari nzuri za virusi vya Corona imekuwa ni kusikika sauti za nchi za kimagharibi za kutaka kurejea kwa Mwenyezi Mungu aliyetukuka na kuacha makosa na madhabi ambayo yamemchukiza Mola mlezi[3].
Anasema Mwenyezi Mungu:

(وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَنْ تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ وَكَانَ الْإِنْسَانُ كَفُورًا)

(Na inapo kufikieni taabu katika bahari, hao mnaowaomba wanapotea, isipokuwa Yeye tu. Na anapowaokoa mkafika nchi kavu, mnageuka. Na mwanaadamu ni mwingi wa kukanusha.) Surat Al-Israa: 67.

 

Imeandikwa na:

Muhammad Yaqoobi, Najaf Ashraf
10 /Shaban /1441h
04/04/2020

Imetarjumiwa na:

Abdallah Khamisi Salum

 

 

 



[1]. Misbaahul Kaf’ami, Uk:229. Beharul Anwaar,Juz: 91, Uk: 211 kutoka katika kitabu cha Muhajud Da’waat.

[2]. Al-irshaad cha sheikh Mufiid, juz:2, uk: 96. Behaarul anwaar,juz: 45, Uk: 4. Tarekh Tabari, juz:5, uk: 423 na vyanzo vingine vilivyotajwa katika kitabu cha As-Sahihu Min Maqtali Sayyidish Shuhadaa: 655.

 

[3]. Mitandao ya kijamii hivi karibuni imesambaza hotuba ya mtu mmoja aliyekuwa akinadi kwa sauti katika moja ya barabara za New York akiwataka watu kutubia na kughairi mienendo iliyojikita kwenye ukusanyaji wa mali na mambo ya matamanio, huku akikemea maovu yao akitaja suala la ruhusa ya utoaji wa mimba na kuua kitoto kilichoko tumboni baada ya kutimiza wiki ya arobaini.