Ayatollah Yaaqubiy ahimiza waumini kumzuru Imamu Ally (as) katika siku ya Ghadeer

Ayatollah Yaaqubiy ahimiza waumini kumzuru Imamu Ally (as) katika siku ya Ghadeer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu
Kwa mnasaba wa siku ya Ghadeer, tunapenda kuwahimiza waumini wote katika jambo la kumzuru Imamu Ally (as) katika mji mtukufu wa Najaf, na hii yote ni katika kuitikia wito wa maimamu watukufu kwa kupitia ulimi wa Imamu Ridha (as) akimuhutubia mmoja ya masahaba zake kwa kumwambia “...Ewe Ibn Abu Basir, popote utakapo kuwepo basi siku ya Ghadeer jitahidi ufike kwa Imamu Ally (as), kwani Mwenyezi Mungu humsamehe muumini awe wa kike au wa kiume madhambi ya miaka 60, na -katika siku hii- huepushwa na moto idadi zaidi ya ambao huepushwa ndani ya mwezi wa Ramadhani, usiku wa Lailatul Qadr pamoja na usiku wa Eid Fitr, na kuwapa ndugu zako japo kidogo katika siku hii kuna malipo makubwa mno...”.
Wito huu umetumia neno “popote utakapokuwepo” ambalo linakusanya kila mmoja na popote alipo, Mashariki au Magharibi bila ya kuchagua, isipokuwa tu yule ambaye atakuwa na udhuru katika hilo ambaye naye ataifanya ziara hiyo baada ya kuondokewa na udhuru.
Kwa hakika siku hii inahitajia kila aina ya umuhimu kwani ndiyo siku ambayo dini na neema za Mwenyezi Mungu vilikamilika kwa mujibu wa Quran tukufu “...Kwa hakika leo nimewakamilishia dini yenu, na kuwatimizia neema zangu, na kuridhia kuwa Uislamu ndio dini...”[1]
Na kukamilika huku kwa dini na kutimiziwa neema ni kutoka na kitendo cha kutawazwa Imamu Ally kuwa kiongozi na khalifa wa Mtume (saww), na baada yake watoto wake kuwa ndio waendelezaji wa hilo. Hivyo hakuna ajabu kwa siku hii kuwa ni Eid kubwa katika Uislamu.
Na hata katika riwaya kutoka kwa Imamu Ridha anasema “....Kwa hakika siku ya Ghadeer ni mashuhuri mno mbinguni kuliko hata ardhini...”.
Bila shaka Mtume na kizazi chake kitukufu kwa pamoja wanafurahika kwa kitendo cha watu kukusanyika kwa wingi katika Haram ya Imamu Ally (as), kwani kitendo hicho kinabadili kabisa muono wa ulimwengu kulielekea tukio hili ambalo limechora mwenendo mzima wa umma na kuuwekea misingi madhubuti kwa kipindi kile tu kichache katika historia, ili baada ya kuondoka kwa Mtume (saww) umma usije ukapotea na kwenda kinyume kama ambavyo imepotea na kwenda kinyume umma nyinginezo.
Tunaona namna ambavyo umma unakusanyika kwa wingi katika tukio zima la Arobaini ya Imamu Hussein (as), mpaka kupelekea watu wa mataifa na dini mbalimbali kujiuliza na kutaka kujua kunako tukio hili la ajabu. Ila bado matunda na malengo ya tukio hili hayajafahamika vizuri, kwani vyombo vya habari pinzani vimebadili malengo na kufanya tu kuwa ni tukio la huzuni, vilio na kujiweka mbali na muhusika wa mauaji ya Imamu Hussein (as) ambaye ni Yazid bin Muawiya.
Sasa kama mkusanyiko kama huu utapatikana katika tukio zima la Ghadeer -hata kama itakuwa baada ya miaka mingi- kiasi kwamba fikra za watu zikazinduka na kuliangalia tukio hili, bila shaka itakuwa tunamnusuru mtukufu Mtume Muhammad (saww), na litakuwa ni jibu kwa wale wenye kuamini imani yenye kupingana kabisa na hekima au mwenendo wa wenye akili ya kwamba Mtume alifariki bila ya kuacha kiongozi na khalifa.
Kama ambavyo pia mkusanyiko huu utakuwa ni kumtendea haki Imamu Ally (as), na kuondoa baadhi ya sintofahamu kuhusu yeye, pia kuwa mashahidi wa haki yake ambayo inapotezwa. Kama ambavyo pia itakuwa ni kuinua utajo wa watu wa nyumba ya Mtume (saww) na kuandaa mazingira kwa ajili ya kudhihiri Imamu Mahdi (atfs) ambaye ndiye mpokezi mkuu wa wenye kumzuru Imamu Ally (as) huku akiwaombea dua njema na mafanikio.
Hivyo basi msipoteze fursa hii adhimu, sajilini majina yenu na uwa kati ya wale wenye kumnusuru Mwenyezi Mungu (swt), Mtume (saww), Imamu Ally (as) pamoja na maimamu wote (sala na amani ziwe juu yao).
Kama ambavyo tunaomba kwa kile wenye kujiweza na wenye vituo vya kupokea wenye kuzuru, kuandaa vyakula, na kila chenye kuhitajika kwa ajili ya mazuwaar -wenye kumzuru Imamu Ally- watukufu.
Mas ala ya kisheria:
Kuna ambao wanaweza kutoa udhuru kunako kumzuru Imamu , kwa kusema kwamba wanahitajia kufunga siku hii kutoka na malipo yake makubwa, na hawawezi kusafiri huku wakiwa na funga.
Hapa lazima tuweke wazi kwamba malipo ya kumzuru Imamu ni makubwa zaidi, pia huyu mwenye kuzuru anaweza kujizuia na vyenye kufunguza akiwa katika safari yake hiyo, na akiwa anarejea mjini kwake atajadidi nia yake ya funga hata kama itakuwa ni karibu na jua kuzama, kwa maana hakuna sharti katika funga ya sunna kwamba mfungaji awepo katika mji wake wakati wa kukengeuka kwa jua.
Ayatollah Sheikh Mohammad Yaaqubiy
Najaf- Asharaf
16/Dhulhijja/1440
18/8/2019
[1] Surat Maidah aya 3